Loading...
Monday

Serikali kupunguza mifuko ya hifadhi ya jamii ibaki miwili tu!

Serikali iko mbioni kupunguza idadi ya mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo nchini ili hatimaye ibaki miwili itakayogawana majukumu ya kuhudumia sekta ya umma na binafsi.

Kadhalika, mifuko hiyo itasaidia kuwabaini wanaokwepa kuwasilisha makato yatokanayo na michango ya wafanyakazi na pia kudhibiti malalamiko yanayojitokeza mara kwa mara.

Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Wizara ya Fedha, Ingiahedi Mduma, alisema serikali iko katika mchakato wa kuanzisha mifuko hiyo mipya ambayo pia itaisaidia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kuwa na wigo mpana wa kupanga kiwango sawa cha makato kitakachookoa gharama zisizokuwa na ulazima.

“Hivi sasa mifuko ya jamii iko mingi na kwakweli inawabana wafanyakazi kupitia makato ambayo baadhi yao hawana taarifa nayo na hivyo kuibua malalamiko kutoka kwa baadhi yao… serikali iko katika mchakato wa kuangalia namna ya kulitafutia ufumbuzi suala hilo,” alisema Mduma.

Baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo nchini hivi sasa ni pamoja na NSSF, PSPF, GEPF, NHIF (afya) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) unaotarajiwa kuanza kazi rasmi Julai, 2016.
 
Toggle Footer
TOP