Loading...
Monday

Serikali ya Kenya yazuia sherehe ya ngono 'Project X'


SERIKALI imezima sherehe ya ngono iliyotarajiwa kufanyika usiku wa Jumamosi ijayo ambayo ilikuwa imeandaliwa na kundi linalojiita “Project X” katika mtaa wa Kileleshwa, Nairobi.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kudhibiti Filamu nchini (KFCB) Ezekiel Mutua Jumatatu alisema bodi hiyo inashikirikiana na polisi kuhakikisha kuwa waandaji wa sherehe hiyo wanatiwa mbaroni na kuhojiwa.

Kundi hilo jana lilitoa mabango mtandaoni likisema kuwa limefutilia mbali sherehe hiyo ya ngono iliyozua mjadala mkali nchini.

“Bodi ya KFCB pamoja na maafisa wa usalama tutahakikisha kuwa tamasha hiyo haifanyiki,” akasema Bw Mutua.

Kulingana na Bodi ya KFCB, sherehe sawa na hizo zimekuwa zikiandaliwa katika maeneo ya Mombasa, Malindi na Nairobi.

Kulingana na KFCB, matamasha ya ngono yamekita mizizi katika mitaa ya matajiri jijini Nairobi kama vile Kileleshwa, Lavington, Kilimani na Runda.

“Tamasha la Project X limeandaliwa na watu walaghai wanaonasa video za vijana wakati wanajihusisha na ngono baada ya kulewa. Baadaye watu hao wanatishia kufichua hadharani video hizo iwapo familia zao hazitakubali kutoa fedha,” akasema Bw Mutua.

Alisema kuwa sherehe hizo zinafadhiliwa na makundi ya wanaharakati ambayo yamekuwa yakitetea haki za mashoga.

Wikendi iliyopita, msemaji wa Polisi Charles Owino alisema kuwa maafisa wa usalama wanaendelea na uchunguzi ili kubainisha waandaaji na lengo la tamasha hilo linalohofiwa kuchochea mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana.

Wikendi iliyopita, waandaaji wa tamasha hilo ambalo pia linafahamika kama Sodoma na Gomora, walikuwa wakisambaza mabango ya matangazo ya kuwataka vijana kuhudhuria sherehe hiyo.
 
Toggle Footer
TOP