Tamko la Wanahabari kuhusu kutekwa kwa Salma Said Humud

Mfanyakazi wa kujitegemea wa Deutsche Welle nchini Tanzania, Salma Said, alizuiliwa kwa muda wa siku mbili na watu waliomteka nyara katika eneo moja lisilojulikana. Kwa mujibu wa polisi, hatimaye aliachiwa huru jijini Dar es Salaam siku ya Jumapili ya Machi 20.

Mwandishi huyo alitekwa nyara Ijumaa ya Machi 18 katika Uwanja wa ndege wa Dar es Salaam akitokea Zanzibar, ambako alikuwa aripoti juu ya uchaguzi wa marudio uliofanyika Jumapili ya Machi 20, lakini kutokana na taarifa alizozipata kwamba usalama wake uko hatarini na baada ya kuzungumza na Idara ya Matangazo ya Afrika ya Deutsche Welle mjini Bonn, alishauriwa aondoke visiwani Zanzibar na akaelekea jijini Dar es Salaam. Kulingana na familia yake, Salma hakufika jijini humo.

Kwa mujibu wa polisi jijini Dar es Salaam, sababu za kutekwa nyara kwake, mahala alipokuwa akizuiliwa au ni kina nani waliofanya kitendo hicho, ni mambo ambayo bado yanachunguzwa. Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro aliiambia DW kwamba: "Tumo katika kuchunguza na tutatoa taarifa kuhusiana na tukio hilo na nani walihusika hapo baadaye."

Mkurugenzi Mkuu wa Deutsche Welle, Peter Limbourg, alisema baada ya kupokea taarifa ya kuachiwa huru Salma Said kwamba: "Fikra zetu ziko pamoja naye na tuna furaha kwamba mwenzetu yuko huru. Heshima ya wafanyakazi wetu ni muhimu zaidi, hasa katika nchi ambako uhuru wa vyombo vya habari na wa kutoa maoni unaekewa vipingamizi. Tunataraji kwamba uchunguzi juu ya kisa hiki utakamilika na kuwekwa wazi."

Salma Said ni mwandishi na ripota maarufu. Mwandishi huyu wa habari mwenye umri wa miaka 45 amekuwa akifanya kazi kama mwandishi wa kujitegemea wa Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle tokea mwaka 2000. Pia huyaandikia magazeti kadhaa ya ndani nchini Tanzania na mitandao kadhaa ya kijamii. Aliwahi kushambuliwa mnamo miaka ya nyuma. Mwaka 2012, alishambuliwa na kikundi cha watu alipokuwa akitoka kuripoti juu ya mkutano wa hadhara wa chama cha upinzani mjini Unguja.

Imetolewa na:
Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle
Bonn

UjerumaniKamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna wa Jeshi la Polisi (CP), Simon Siro leo Jumatatu, Machi 21, 2016 amesema kuwa mwandishi wa habari, Salma Said aliyetekwa Zanzibar hivi karibuni hajakutwa na jeraha lolote katika mwili wake.

Amesema kuwa wamechukua malalamiko ya mwandishi huyo na wanayafanyia uchunguzi na baada ya upelelezi watachukua hatua stahiki.

Amesema kuwa kwa sasa Salma yupo kwenye matibabu katika hospitali ya Regency ya jijini la Dar es Salaam.

Habari zilizopatikana jana jioni na kuthibitishwa na mumewe, Ali Salim Khamis na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi, Simon Siro zilisema Salma alisajiliwa jana mchana katika hospitali hiyo.

Ali aliyekuwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, alisema kwa ufupi kuwa amepata taarifa hizo na kufika Dar es Salaam kuzifuatilia.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na MwanaSpoti, Francis Nanai alisema wanaendelea kufuatilia kwa makini suala hilo.

“Taarifa za kutoweka kwa Salma zilitufikia Ijumaa mchana Machi 18, 2016 kupitia kwa mume wake, mpaka sasa hakuna taarifa yoyote inayoonyesha ni nani au chombo gani kinamshikilia au kumhifadhi, hali hii inatutia wasiwasi mkubwa kama kampuni na wadau wa habari nchini,” alisema Nanai.

Wakati huo huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika tamko lake ililolitoa jana ilieleza kuwa kutekwa kwa mwanahabari huyo kumezua maswali mengi kwa wananchi, familia yake, wadau na wanahabari wa ndani ya nchi na wale wa jumuia za kimataifa.

“Kutekwa kwa Salma kunatokana na kazi yake ya uanahabari, ndiyo maana ushahidi wa awali uliopatikana kwa njia ya ujumbe wa sauti ukiwa na sauti inayoaminika kuwa ni yake, ulieleza wazi kutekwa kwake kunatokana na yeye kuripoti dosari zinazoendelea katika uchaguzi wa marudio Zanzibar,” alisema Joseph Mbilinyi, Waziri Kivuli wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo wa Kambi ya Upinzani.

Mbilinyi ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini (CHADEMA) alidai kuwa matukio mbalimbali yanayoendelea Zanzibar yakiwamo ya matumizi ya nguvu, vitisho na hata vitendo vya kikatili dhidi ya wanaosimamia haki, vinaendelea kuitia Serikali ya CCM doa, Taifa na dunia nzima.

Kamanda Sirro alisema: “ Tumefungua jalada la uchunguzi wa tukio hili juzi,” alisema Sirro na kuongeza. “Wapelelezi walizungumza na mume wa Salma na kuna mambo amewaeleza lakini hatuwezi kuyaweka wazi kwa sasa, hadi uchunguzi utakapokamilika, tumeipata namba ya simu aliyowasiliana nayo na mumewe akiwa huko kunakoaminika amefichwa,” alisema.

TAMKO LA UMOJA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA JUU YA KUTEKWA KWA MWANDISHI WA HABARI WA SAUTI YA UJERUMANI ( DW ) SALMA SAID.


Salma Said mwandishi wa DW Zanzibar ametoweka baada ya kutekwa na watu ambao hawajafahamika jijini Dar es salaam, hali ambayo imeleta fadhaa na mshtuko kwa waandishi, jamii na familia yake hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa marejeo Zanzibar.

Ifahamike kuwa Kazi ya mwandishi wa habari ni kutoa habari juu ya kila kinachoendelea katika jamii , hivyo kama kuna dosari , dosari hiyo ni ya jamii na sio ya anayeieleza dosari .

UTPC inalaani na kupinga utekaji uliofanywa ambao sababu zake bado hazijulikani, hivyo tunaitaka serikali kuhakikisha Salma Said anatafutwa, kupatikana na anaachiwa huru mara moja kwa kuwa Serikali ndio yenye jukumu la kulinda raia wake.

Kama utekwaji wa Salma umefanywa kutokana na kazi yake ya uandishi habari tunalaani vikali hatua hiyo, vitendo hivi havipaswi kuendelea katika nchi inayoheshimu misingi haki na Demokrasia, Vitendo vya namna hii vinadumaza na kufifisha uhuru wa habari .

Tunapinga kwa nguvu zetu zote waandishi wa habari kukamatwa na vyombo vya dola au makundi ya kihalifu kwa visingizio ama vya uchochezi au maslahi ya taifa.

Waandishi tutaendelea kufanya kazi zetu bila kujali vitisho vya aina yoyote ile kutoka kwa mtu yoyote au Serikali.

Imetolewa na
DEOGRATIUS NSOKOLO
RAIS WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA -UTPC.
March 19, 2016.