TSN Supermarket Ilivyogeuka kipenzi cha watumiaji wa Twitter

Wataalam wa masuala ya masoko wanasema biashara haitaji kutumia mamilioni ya fedha katika kujitangaza bali kampeni ndogo tu ambayo itagusa hisia za watu wengi kwa wakati mmoja. Huenda wakati TSN wakifanya hiki hawakutegemea muitikio wa watu utakuwa chanya kiasi hiki lakini ndivyo ilivyotokea.

Ahmed Albaity
Kwa muda wa takribani miaka 10 kijana Ahmed Albaity amekuwa mgonjwa mara baada ya kupooza sehemu kubwa ya viungo vya mwili wake wakati akiwa katika bwawa la kuogelea. Picha za Ahmed ambaye ni kijana mdogo mwenye sura ya kuvutia zilisambazwa na ndugu zake ambao wamekuwa wakimuombea msaada wa matibabu na kupelekea maelfu ya watumiaji wa mitandao ya kijamii hasa Facebook na Instagram kuguswa na kuanza kuchangishana.  

Ujumbe wa Ahmed kuhusu matumaini mapya ya matibabu

Wiki chache zilizopita Ahmed alisambaza ujumbe kupitia Whatsapp kuhusu matumaini mapya ya matibabu ambayo yanaweza kuumaliza ugonjwa wake na kuwaomba msaada wasamalia wema ili aweze kufikisha kiasi cha $50,000 (dola elfu hamsini za Kimarekani) ambazo kwa sasa zina wastani wa kama Sh 110,000,000.

Ujumbe huu unaotia matumaini uliwashawishi watu wengi ambao wamekuwa wakifuatilia maendeleo ya Ahmed kuanzisha harambee ya kuchangia matibabu ambapo mmoja ya marafiki zake walilileta suala hili katika mtandao wa Twitter ambako wengi walikuwa hawamfahamu Ahmed lakini baada ya kusoma ujumbe huo waliguswa na kuanza kuusambaza na hashtag ya #AhmedAamke kuanzishwa ili kusaidia kueneza ujumbe. 

Watanzania walioko Twitter kwa muda mrefu wamekuwa na sifa ya kufanya michango ya kijamii na michango ya pole kwa wale waliopata matatizo ambapo itakumbukwa namna walivyoweza kuchangia madawati zaidi ya 200 kwa shule za msingi Mjimwema ya Kigamboni na shule ya Msinune Bagamoyo pia wakiendesha mchango wa Catheter zilizosambazwa katika hospitali za Dar es Salaam na Morogoro, misaada kwa waathirika wa mafuriko na hata rambirambi pale mmoja anapopatwa matatizo.

Kusambaa kwa hashtag ya #AhmedAamke ilipelekea baadhi ya watumiaji wa Twitter kuanza kuyaomba makampuni yaliyopo kwenye mtandao huo kuchangia ambapo mengi yalitia jicho la upofu huku baadhi yakitoa majibu ambayo yalipelekea hasira kwa waliosoma.

Ni katika wakati huu ambapo TSN Supermarket ambayo ilikuwa haina muda mrefu tangu ijiunge Twitter ilitoa ahadi ya kuchangia kiasi cha Sh 2,200,000 (milioni mbili na laki mbili) ambazo kwa sasa ni sawa na $1000 (dola elfu moja za Kimarekani). 


Pengine TSN walifanya hivi wakiwa kama mmoja ya Watanzania walioguswa lakini kilichotokea huenda kiliwashangaza hata wamiliki wake.  Saa moja baada ya tweet ya kutoa ahadi ya mchango TSN ilijikuta ikitajwa na zaidi ya watu 1,000 huku tweet yake ikipata Retweets zaidi ya 100. Wakati ikitoa ahadi hii ilikuwa na wafuasi 11 tu lakini baada ya masaa 12 wafuasi wake walipanda hadi kufikia 300 na mpaka tunaandika hii idadi ilikuwa inaongezeka. Kingine cha kufurahisha ni namna watu wengi walivyoahidi kuanza kununua bidhaa katika Supermarket za TSN huku baadhi wakipiga selfie wakiwa ndani ya supermarket hizo masaa machache baadae.


Michael Mlingwa mmoja ya wapiga picha maarufu jijini akionyeshwa kuguswa

Mchekeshaji Masanja Mkandamizaji akiwashawishi mashabiki wake kuifuata TSN


Habari njema, mteja mpya wa TSN
Hii inaweza kuwa fundisho kwa makampuni mengine kuwa yanatakiwa kuitumia mitandao ya kijamii kama wanajamii badala ya kuwa kama robot wanaotangaza biashara zao. Unapokuwa sehemu ya suluhisho la matatizo ya wanajamii wanaokuzunguka bila kuombwa unatengeneza ufuasi wa kudumu “brand loyalty” kwa biashara yako.

Kufahamu kwa undani kilichomkuta Ahmed hadi kufikia hali hii tazama video hii