TTCL yajiandaa kuomba fedha ya kuwalipa wafanyakazi zaidi ya 400 watakaopunguzwa


Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ipo kwenye maandalizi ya kupunguza wafanyakazi wasiohitajika kwa sasa kutokana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
TTCL inayotoa huduma za simu na pia kutoa mitandao kwa kampuni zilizo na leseni ya huduma hizo, itapunguza wafanyakazi 400 ili kuongeza ufanisi na hivyo kumudu ushindani katika sekta ya mawasiliano dhidi ya kampuni binafsi.

Mapema mwaka jana, Serikali iliamua kununua asilimia 35 ya hisa za TTCL zinazoshikiliwa na kampuni kubwa ya huduma za simu nchini India, Bharti Airtel na baadaye mwezi Mei, 2015 aliyekuwa Naibu Waziri wa Sayansi na Mawasiliano, January Makamba aliliambia Bunge kuwa Serikali iko katika maandalizi ya mwisho ya kumiliki hisa zote za kampuni hiyo kubwa kwa huduma za simu za mezani nchini.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya kampuni hiyo kinaeleza kuwa kati ya wafanyakazi 1,500 wa TTCL, zaidi ya 400 watapoteza ajira katika mpango huo wa kudhibiti gharama za uendeshaji.

“TTCL itaomba fedha ili kuwalipa wafanyakazi zaidi ya 400 wanaotakiwa kupunguzwa,” alisema mtoaji habari huyo ambaye aliomba jina lake lisitiriwe.

“Kuna wafanyakazi wanaingia asubuhi na kutoka jioni bila kufanya kazi yoyote ile na mwisho wa mwezi anakula mshahara zaidi ya Sh800,000. Kumuachisha kazi inakuwa vigumu sana, lakini kama TTCL itasaidiwa na Serikali kufanikisha hilo, itakuwa imejikwamua kwa kiwango fulani.”

Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk Kamugisha Kazaura alisema maandalizi ya kupunguza wafanyakazi yataanza mwezi Aprili kupitia ukaguzi maalumu wa rasilimali watu.
Alisema hatua ya awali kwa sasa ni kuangalia mpango mkakati wa kampuni hiyo jinsi gani inaweza kujijenga upya kutokana na changamoto ya ushindani wa kibiashara.

“Kwa sasa siwezi kusema ni wafanyakazi wangapi wanatakiwa kupunguzwa kutoka miongoni mwa 1,500 kwa kuwa kila mmoja amekuwa akiwasilisha taarifa yake mwisho wa mwaka na wapo wanaotimiza na wengine wanashindwa kutimiza malengo ya kampuni, mchango wao unakuwa kidogo,” alisema.

Dk Kazaura alisema katika lengo la mpango huo ni kuangalia jinsi gani watalaamu waliopo wanatumika kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

Alisema kuna wataalamu waliopo kwa sasa ambao hutumika katika shughuli za uzalishaji, lakini kulingana na mabadiliko ya kazi nyingi kufanywa na teknolojia mpya na nafasi ya kazi nyingi katika taaluma zao zimepungua.

“Pamoja na hivyo lakini itakuwa vigumu kuwafahamu ni wangapi ambao hawazalishi katika kampuni hadi kazi hiyo ya HR auditing (ukaguzi wa rasilimali watu) itakapokamilika. Itakuwa tathmini itakayotoa mwelekeo mpya wa kampuni,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu mpango wa TTCL kuomba msaada serikalini, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema hana taarifa yoyote.

Hata hiyo, alisema TTCL ina mamlaka yake ya kujiamulia kuajiri au kupunguza wafanyakazi bila kuingiliwa na Serikali.