Loading...
Saturday

Viongozi wakubwa walitetea wauza madawa? Shikuba, Chonji na Mama Leila nilikuwa nasumbuka nao - Nzowa

SIKU moja baada ya vyombo vya habari kuripoti hatua ya Marekani kutaifisha mali za mfanyabiashara wa dawa za kulevya, Ali Khatib Haji Hassan, maarufu kama ‘Shikuba’ pamoja na mtandao wake wa kimataifa, aliyekuwa Kamishina wa Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, amesema alitikiswa na bilionea huyo.

Nzowa alitoa kauli hiyo baada ya kutafutwa na gazeti la MTANZANIA ili kupata maoni yake, hasa ikizingatiwa kwamba ndiye aliyeongoza kikosi kilichomkamata Shikuba akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), baada ya kusakwa kwa miaka miwili hapa nchini akituhumiwa kusafirisha dawa aina ya heroin kiasi cha kilogramu 212.

Kamishna huyo mstaafu, Nzowa, alisema kwa muda wa miaka 16 aliyofanya kazi katika kitengo hicho alisumbuliwa na watu watatu ambao aliwaita vinara wa dawa za kulevya.

Aliwataja vinara hao kuwa ni pamoja na Shikuba, Mwamalela na Chonji.

“Kwa muda wa miaka 16 ya kitengo changu huyu Shikuba, Chonji (Muharami Abdallah) na Mama Leila (Mwanaidi Mfundo) ambaye naye Marekani walitangaza kama hivi, ni wakubwa. Na kila mara nilikuwa nasumbuka nao,” anasema Nzowa.

Katika moja ya taarifa ambazo ziliwahi kutolewa na gazeti moja la wiki, zilisema Mwanaidi anafahamika nchini Kenya na Marekani kwa jina la Naima Mohamed Nyakinywa au Naima Nyakinywa.

Taarifa hiyo ilidai kuwa, Mei 2011, Rais wa Marekani, Barack Obama, alimtangaza Mama Leila kuwa muuza ‘unga’ mkuu duniani, hivyo akapigwa marufuku kuingia nchini Marekani.

Katika mahojiano hayo, Nzowa alisema anakumbuka Januari 2012 ambayo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mtego wao kunasa na kukamata mali zilizodaiwa kuwa ni za Shikuba ambazo ni dawa za heroin kilo 212 zilizokuwa na thamani ya zaidi ya Sh bilioni 10.

Katika kamata hiyo, iliyofanyika mkoani Lindi, Nzowa anasema Shikuba alifanikiwa kutorokea Afrika Kusini, lakini walifanikiwa kukamata gari lake la thamani aina ya Jeep.

“Baada ya kutukimbia ‘niliji-commit’ mahakamani kuwa huyu mtu ni hatari achunguzwe na ndipo alikamatwa na hivi sasa yuko mkoani Lindi chini ya ulinzi ambako ana kesi ya kujibu kuhusu tuhuma hizo. Hilo gari lake linatumika kama kielelezo,” alisema Nzowa.

Alisema anaishukuru Marekani kwa kuona mali hizo na kuzitaifisha, kwani hata katika vikao vilivyoshirikisha nchi mbalimbali duniani alivyohudhuria kama mwangalizi walizungumzia suala la kuwakamata watu wa aina hiyo na kutaifisha mali zao.

“Tulivyokwenda Roma- Italia na Moscow –Urusi tulizungumzia hilo. Mimi nilikuwa nakwenda kama Observer (mwangalizi) katika mikutano hiyo kwa kuwa sisi siyo wanachama, lakini walikuwa wanatualika kutokana na jitihada zetu katika kupambana na dawa za kulevya,” alisema Nzowa.

Nzowa alisema walianza kukamata wafanyabiashara wadogo mwaka 2010 na waligundua kiasi kidogo tu walichokamata kiliwahusisha mamia ya watu.

“Katika kete tano tulizozikamata zilikuwa zikiwahusisha watu zaidi ya 200, baada ya hapo tuligundua mtandao ni mpana na tunapaswa kujielekeza kwa hao wakubwa zaidi kuliko wadogo, hivyo tukaanza kazi na hao wakubwa,” alisema Nzowa.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha ya Marekani kupitia ofisi yake ya Udhibiti wa Mali Haramu za Raia wa Kigeni (OFAC) na kuchapishwa jana na gazeti hili ilieleza Shikuba na taasisi yake wameangukia katika sheria za nchi hiyo za kudhibiti mapapa wa unga wa kigeni (Kingpin Act).

Mbali na sababu hizo za kisheria, Marekani ilisema bilionea huyo amekuwa akitumia faida haramu kutokana na biashara zake chafu kuhonga maofisa wa serikali ya Tanzania ili asikamatwe na kushtakiwa.

Kwa sababu hiyo, mali zote za Shikuba na taasisi zake zilizo ndani ya mipaka ya Marekani au ambazo ziko chini ya raia wa taifa hilo, zimetaifishwa huku raia wa Marekani wakionywa kuhusiana nazo.

Kutokana na tuhuma za kuhongwa maofisa hao, gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kanda na Kimataifa, Balozi Augustino Mahiga, ambaye alisema hawezi kuzungumzia hilo kwa madai kuwa linaweza kujibiwa vyema na Wizara ya Mambo ya Ndani.

“Unajua wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani wana habari zaidi, mimi wa nje sina taarifa za ndani, huyo jamaa nimesoma habari zake amekuwa akijishughulisha ndani ya miaka 10, unajiuliza ilikuwaje? Mtu kupata International Criminal lazima una mtandao,” alisema Mahiga.

MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, pasipo mafanikio.

Hata alipopigiwa simu zaidi ya mara tatu na zaidi akitumiwa ujumbe mfupi wa maneno ili kupata kauli yake, bado hakuweza kujibu.

Shikuba alikamatwa mwaka 2014 katika Uwanja wa JNIA baada ya kusakwa kwa zaidi ya miaka miwili na polisi kutokana na tuhuma za dawa za kulevya, huku akidaiwa kuwa na mtandao mkubwa Afrika Mashariki, China, Brazil, Canada, Japan, Marekani na hata Uingereza.

---------- MWISHO WA TAARIFA YA GAZETI LA MTANZANIA -------------

Kiongozi wa Wizara amtetea Shikuba, ‘bilionea wa dawa za kulevya’


Baadhi ya viongozi wakubwa katika Serikali ya Rais Kikwete wametajwa kuwa ndiyo chanzo cha kudhoofisha juhudi za kupambana na vita dhidi ya mihadarati kwa kuwakumbatia watuhumiwa waliokamatwa.

Mmoja wa vigogo hao anayefanya kazi katika wizara nyeti, ametajwa 'kumpigania' bilionea aliyekamatwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam akituhumiwa kuhusika na shehena ya kilo 210 za dawa za kulevya aina ya heroin zinazokisiwa kuwa na thamani ya Sh bilioni 10 ambazo zilikamatwa nchini mwaka 2012 mkoani Lindi.

Tayari bilionea huyo, Ali Khatib Haji 'Shikuba' ameshafunguliwa mashitaka, kesi yake ikiunguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Lindi.

Kwa mara ya kwanza alipandishwa kizimbani Machi 13 mwaka huu akiunganishwa na watuhumiwa wengine, Maureen Liyumba, Othman Mohammed Nyamvi au maarufu kwa jina la Ismail Adam na Upendo Mohammed Cheusi ambaye kwa sasa ni marehemu.

Kwa mara ya pili wanatarajiwa kupandishwa kizimbani kesho mbele ya Kaimu Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Lindi, Allu Nzowa.

Habari za uhakika ambazo mwandishi amezipata zinasema tangu kukamatwa kwa Shikuba, kigogo huyo amekuwa akihaha kutaka kumnusuru mfanyabiashara huyo maarufu dhidi ya kesi inayomkabili.
Kukamatwa kwa Shikuba kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Kudhibiti Dawa za Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa.

"Ni kweli tumemkamata. Juhudi zetu zimefanikiwa kukamata mmoja wa watu wazito wanaohusishwa na biashara hii," alisema.

Ingawa `mzigo' anaohusishwa nao Shikuba ulikamatwa mwaka 2012, inaelezwa hakukamatwa kutokana na mfanyabiashara huyo kuwa mafichoni nchini Afrika Kusini na kwamba akiwa huko, alitumia hila na kupata hati nyingine ya kusafiria iliyotolewa Februari 28, mwaka huu, hivyo kurejea nchini alikokumbana na vijana wa Nzowa mara baada ya kutua kwa ndege ya shirika la Ndege la Afrika Kusini, South African Airways.

Mara baada ya kumkamatwa, alisafirishwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi hadi mkoani Lindi.

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP