Wagoma kuchukua barua za kufutwa kazi wakisubiri ushauri wa kisheria

Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) waliofutiwa mikataba ya kazi, wamegoma kupokea barua za kuachishwa kazi wakidai kwamba hawajui kilichoandikwa kuhusu hatima ya madai yao.

Wafanyakazi hao walikutana jana Dar es Salaam na kiongozi wao, Seif Kibangu alisema wamekubaliana kutochukua barua hizo hadi pale watakapopata ushauri kutoka kwa wanasheria.

“Licha ya mishahara ya miezi mitatu tuna madai yetu mengine ikiwamo makato ya mafao yetu yaliyotakiwa kupelekwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, pia tumekuwa tukikatwa bima ya afya asilimia tatu ya mishahara yetu hatujui hatma yake. Sasa leo wanataka tuchukue barua hizo tena kwa kusaini kabla ya kujua kilichoandikwa hapana tuendelee kuvumilia haki yetu tutaipata,” alisema Kibangu.

Aliwakosoa waliochukua barua hizo akisema waliajiriwa kwa makundi, ingawa pia wapo waliopewa kazi hiyo kwa vimemo.

“Hili ni jasho letu, hatuibi cha mtu kwa hiyo tunastahili kupata haki zetu zote, mishahara tunayodai kwa miezi mitatu, acha hayo madai mengine... Tunadaiwa huko tunapoishi kwa kweli tunaomba wahusika waingilie kati jambo hili linatuumiza na kuyumbisha maisha yetu,” alisema. Akizungumza kwa niaba ya madereva wenzake, George Mmari alidai kuna gharama nyingi walizoingia ambazo Nida inapaswa kuzilipa ikiwamo malipo ya kuegesha na kuosha magari waliyokuwa wakiendesha.

Akizungumzia madai hayo, Ofisa Habari Mwandamizi wa Nida, Rose Mdami alieleza kushangazwa na hatua ya wafanyakazi hao kugoma kuchukua barua zao badala ya kuzipokea ili wajue kilichoandikwa ili kama wana madai waandike barua na kuyaorodhesha.
  • via Mwananchi

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambao wamisitishiwa mkataba wa kufanya kazi kutokana na ukata ulioikumba mamlaka hiyo, wamegoma kupokea barua rasmi zinazoonyesha kusitishwa kwa mikataba yao.

Mmoja wa wafanyakazi hao, Mpaji Isaya aliiambia Nipashe jana kuwa, waliambiwa wafike kuchukua barua hizo jana, ili kuthibitisha rasmi kufutwa kwa mikataba yao.

“Baada ya kutangaziwa na Kaimu Mkurugenzi kuwa mikataba imefutwa, walisema tufike leo NIDA kuchukua barua za uthibitisho," alisema Isaya.

"Lakini cha ajabu wanataka tusaini fomu kuthibitisha tumepokea barua na tuondoke, wakati kilichoandikwa ndani ya barua hatukijui.
"Sasa kama stahiki zetu tumepunjwa tutajuaje?”

Isaya alisema NIDA ilitakiwa iwape muda wa kuzisoma barua hizo kama ilivyokuwa awali wakati wa kuajiriwa ambapo walipewa muda wa siku tatu kuusoma na kuuelewa mkataba ndipo wakasaini.

Kaimu Mkurugenzi wa NIDA Modestus Kipilimba, alisitisha mikataba ya wafanyakazi 597 wiki iliyopita kwa maelezo ya ukosefu wa fedha za kuwalipa wafanyakazi hao kwa sasa.

Kaimu Mkuu wa kitengo cha Uhusiano wa NIDA, Rose Mdami, alipotafutwa na Nipashe ili kutolea ufafanuzi suala hilo, alisema waliwapa taarifa wafanyakazi hao kufika jana kwa ajili ya kuchukua baraua zao.

“Taarifa za kuja leo (jana) ofisini NIDA wafanyakazi ni za kweli, walikuja kufuata barua zao lakini kwa maelezo mengine ufike ofisini kwetu,” alisema Mdami.

NIDA ilisema haina fedha za kuwalipa malimbikizo ya mishahara ya miezi miwili wafanyakazi wa 597 waliositishiwa mikataba yao ya muda huku menejimenti ikisema inaendelea kujipanga ili kuhakikisha inawalipa kwa wakati bila usumbufu wowote ijapokuwa ofisi hiyo haina fedha kwa sasa.

NIDA ilisema inaendelea kufanya uhakiki wa mikataba ya wafanyakazi wote 597 na kusubiri pesa kutoka hazina kwa ajili ya kuwalipa kwa mujibu wa sheria.