Mbali na wakurugenzi hao, mwingine ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria PPRA, Bertha Soka.
Washtakiwa hao walisomewa mashitaka yao jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.
Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis, akisaidiana na Waendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Peter Vitalis, Joseph Kiula na Stanley Luoga.
Timon alidai kuwa Oktoba 9, mwaka 2007, Mattaka wakati akitekeleza majukumu yake kama Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, alitumia madaraka yake vibaya kusaini mkataba wa kukodisha ndege aina ya Airbus.
Ilidaiwa kuwa mkataba huo ni kati yake, kampuni ya Wallis TradingInc kama mkodishwaji na ATCL kama mkodishaji bila kufuata Sheria ya Ununuzi ya Umma ya mwaka 2004 na kanuni za Ununuzi ya Umma ya mwaka 2005.
Shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Oktoba 27, mwaka 2007 katika ofisi za ATCL zilizopo Ilala, Mattaka akiwa kama Mkurugenzi Mtendaji na mtumishi wa umma wa shirika hilo, alitumia vibaya madaraka yake kwa kusaini mkataba wa kukodisha ndege hiyo bila kujali ushauri wa kiufundi.
Katika shitaka la tatu, ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 27, 2007 na Aprili 24, 2008, Mattaka akiwa mwajiriwa kama Mkurugenzi Mtendaji, aliruhusu ATCL kukodi ndege hiyo na kuisababishia serikali hasara ya Dola 772,402.08 za Marekani (sawa na Sh. bilioni 1.69) baada ya kuilipa kampuni ya Aeromantenimiento kama gharama za matengenezo ya ndege hiyo.
Upande wa Jamhuri uliendelea kudai katika shitaka la nne kuwa kati ya Oktoba 27 na Novemba 29, 2007, Mattaka akiwa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, alitumia vibaya madaraka yake kwa kusaini cheti cha kukubali ukodishaji wa ndege hiyo bila kuzingatia ushauri wa kitaalam na kuisababishia ATCL hasara ya Dola 35,984.82 za Marekani zilizolipwa kwa kampuni ya Lantal Textiles Inc kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za ndege ukiwamo kapeti.
Ilidaiwa katika shitaka la tano, kati ya Oktoba 9, 2007 na Oktoba 26, 2011, Mattaka akiwa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, kwa uzembe, alisaini mkataba wa makubaliano ya kukodisha ndege kati ya kampuni ya Wallis Trading Inc ya Liberia na ATCL na kuisababishia serikali kupata hasara ya Dola 42,459,316.12 za Marekani (sawa na Sh. bilioni 92.99).
Katika shitaka la sita, ilidaiwa Machi 19, 2008 katika ofisi za PPRA zilizopo Wilaya ya Ilala, Dk. Mlinga na Soka, walighushi mwenendo wa kikao wa tarehe hiyo, wakionyesha kwamba mamlaka hiyo ilikaa kikao na kujadili maombi ya kuidhinisha ATCL kukodisha ndege.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi hadi upelelezi utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na haukuwa na pingamizi la dhamana kwa mshtakiwa wa pili na wa tatu kwa kuwa shitaka linalowakabili lina dhamana.
Hakimu Mwijage alisema mshtakiwa wa pili na wa tatu watakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini hati ya dhamana ya Sh. milioni 10 kila mmoja.
Alisema mshtakiwa wa kwanza dhamana yake inatolewa na Mahakama Kuu kwa mujibu wa masharti itakayopanga.
Mbali na kesi hiyo, Mattaka pia anakabiliwa na kesi nyingine ya matumizi mabaya ya madaraka.
- via NIPASHE