Wale Wachina waliokamatwa na Kagasheki wakiwa na vipusa vya ndovu wamehukumiwa jela miaka 30

Kutoka kulia ni na Xu Fujie na Huang Jing
Raia wawili wa China wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 au kulipa zaidi ya sh. bilioni 54 kila mmoja kwa kukutwa na hatia ya makosa mawili.

Washitakiwa hao katika kosa la kwanza walikutwa na hatia ya kukutwa na nyara za serikali, vipande 706 vya vipusa vya tembo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tano wakati kosa la pili ni la kushawishi kwa kutoa rushwa kwa askari kiasi cha shilingi milioni 30/=.

Washitakiwa hao Huang Jing pamoja na Xu Fujie wameanza kutumikia kifungo hicho leo baada ya kushindwa kulipa faini.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Cyprian Mkeha alitoa hukumu kwa watuhumiwa hao na kusema wanaweza kukata rufaa katika Makahakama Kuu.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi aliomba mahakama iwape adhabu kali kutokana na kosa waliolifanya na kudai kuwa kutokana na kukamatwa kwao vitendo vya uhalifu kwa wanyamapori vimepungua.

Wakili upande wa washitakiwa, Nehemia Mkoko aliomba mahakama kuwaonea huruma kwa adhabu wataoipata ili waweze kutoka na kuweza kujumuika na familia zao. 
  • Taarifa ya Chalila Kibuda/Michuzi blogWatuhumiwa walivyokamatwa

Raia wa China wamekamatwa jijini Dar es Salaam huko Mikocheni wakiwa na shehena ya vipande 700 vya meno ya tembo.

Wakazi wa eneo hilo wanaowafahamu Wachina hao wamesema huwa wanawaona wakiuza ndimu na vitunguu.

Waziri Kaghasheki amesema inakadiriwa kuwa ni zaidi ya tembo 200 waliouawa ili kupata meno hayo. Akasema amemweleza mmoja wa Wachina hao kuwa ingelikuwa amekamatwa nchini kwao China, hukumu ambayo ingempasa ni kifo. Waziri pia alisema anahisi huenda watu hawa wakawa wanafahamu ama kuhusika na moja ya makontena yaliyokamatwa nchini China yakiwa na meno ya tembo.

Habari zaidi, tizama video ifuatayo ya taarifa ya ITV.