Loading...
Sunday

Wametafuta Savimbi na Mabutu wao huko Zanizbar ili wafanye kazi


KARAGOSI ni kinyago kinachoning’inizwa kwenye uzi na kuchezeshwa kwa kuvutwa uzi. Karagosi huchukua sura ya mnyama au binadamu. Kawaida yule mwenye kumwendesha huyo karagosi huwa haonekani. Akitaka kucheka au kununa mwenye uzi aliyenyuma ya pazia ndiye anayeamua. Akitaka karagosi ainame au atembee siyo karagosi mwenye kuamua bali aliyeshika uzi ndiye anayeamua.

Hata maneno anayosema karagosi huwa siyo maneno yake bali ni maneno ya kutumwa. Akiamua kuimba ingawa karagosi ndiye atafunua kinywa na kujidai kuimba kwa mbwembwe na pozi lakini maneno si yake ni ya mwenye kushika uzi wa kuchezesha karagosi. 

Katika uwanja wa siasa karagosi hatafautiani na kibaraka. Huyu ni mwanasiasa anayetumiwa na mwingine kwa manufaa ya anayefanya shughuli hiyo bila kujali madhara anayopata wenzake katika jamii. 

Wapo viongozi vibaraka katika vyama vya siasa. Hawa huwa wanatumwa na mabeberu kwa masilahi yao bila kujali madhara wanayopata wananchi au taifa. Hawa hujivika sura ya uanasiasa usoni ili waonekane wazalendo, watetezi na wapenda nchi na wananchi. Hupewa fedha, maelekezo na misaada huko ughaibuni. Huitwa Ulaya, Arabuni au Marekani kufadhiliwa. 

Karagosi wakirudi nchini hutumiwa kuharibu shughuli nchini mwake kwa kutumia kuviza maendeleo, kuitisha migomo, hujuma hata kuendesha ugaidi. Mara zote karagosi ndiye anawaambia hao wenye kushika uzi wa kumchezesha azuiye misaada na mikopo isiletwe nchini mwake. Ukaragosi wake unamfanya asijali madhara yanayowafika watu wa nchi yake. 

Afrika imekuwa na vibaraka aina ya karagosi tokea wakati wa harakati za kudai uhuru hadi sasa. Kule Angola, alikuwepo Savimbi na chama chake cha UNITA. Huyo alifadhiliwa na kusaidiwa na mabeberu ili wazalendo na chama MPLA kisishike serekali. Watu waso na hatia kwa maelfu waliuwawa wakiwemo watoto na wanawake. Karagosi Savimbi alikuwa akipewa msaada wa fedha, silaha na mbinu za mikakati na mabeberu. Angola ilichelewa kupata uhuru wake kwa usaliti wa Savimbi. Hata hivyo, wengi wape, Angola ikapata uhuru wake. Nini matokeo ya kibaraka huyu? Mabeberu kama kawaida yao wakamchoka na kufanya mbinu ili auwawe. Wamemsahau. 

Kibaraka karagosi mwingine wa Afrika ni Mabutu wa Congo. Ni yeye alitumwa kumua Lumumba, mwanampinduzi na mzalendo kwa manufaa ya mabeberu. Mabutu akawa dikteta, ameua, ametesa na amenyonya uchumi wa Congo. Mabeberu kama kawaida yao, baada ya kumtumia Mabutu kwa masilahi yao, mwisho wakamuacha afe kwa saratani bila msaada wowote. 

Viongozi hawa vikaragosi katika Afrika wametumika sana kwa maelekezo ya mataifa ya magharibi. Ni hawa ambao ni makasuku ambao wanasema ambayo wakubwa wanayoyataka. Ni hawa ambao ni mawakala wao hutenda wanachotaka. Ni hawa ndiyo makuwadi wao, wanaowasemea.

Zanzibar imefanya uchaguzi mwaka wa jana uchaguzi uligubikwa na ghiliba za kuiba kura, vitisho na hujuma kadha. Nilidhani wakubwa huko nje ambao ndiyo miamba ya demokrasia, wao wangekuwa wa kwanza kuunga mkono marejeo hayo kinyume chake wamekuwa vikwazo. Sasa Wametafuta Savimbi na Mabutu wao huko Zanizbar ili wafanye kazi ya ukaragosi. Wamemfunga uzi na kuanza kumchezesha. Wakamua wao acheke, huvuta uzi wa uso, ili ukunjuke, naye acheke. Wakiamua atembea, huvuta uzi wa miguu, ili atembee. Wakipenda azungumze, atazungumza lakini anayoyasema yanapitia tu kinywani mwaka lakini maagizo ya wenye karagosi. 

Huitwa Dubai, London, New York ili kupewa maelekezo na maagizo nini la kufanya. Huko huwekwa kitako na kupewa mikakati namna ya kuikwamisha nchi katika maendeleo yake. Wakati huo hao, mabeberu kwa kutumia vyombo walivyoviunda wao wenyewe hutoa sauti ya kutishia ya kutoshiriki uchaguzi wa marejeo wakiwa waangalizi wao. Baadaye, watasusa kutoa misaada na mikopo kwa nchi. Tabia ya undumakuwili kwa wakubwa hao imezoeleka sana. Zanzibar uchaguzi kurejewa hawataki. Karagosi wao hutumika kupaza sauti. 

Zipo nchi kadhaa ambazo hata hakuna vyama siasi na hakuna chaguzi lakini wameufyata. Kisa? Wanabembeleza mafuta na rasmali zao. Saudia, Omani au EAU wana vyama siasa? Kuna uchaguzi wa Rais? Tunamsubiri akirudi atwambiye aliyoambiwa huko alipokwenda kufundwa. Utakuwa ukaragosi na ubarakala tu!
  • Imeandikwa na Dkt. Muhammed Seif Khatib
  • Imenukuliwa kutoka kwenye blogu ya CCM
 
Toggle Footer
TOP