Watumishi walio likizo, masomoni watakiwa kuripoti vituo vya kazi kwa uhakiki

Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke walioko masomoni na likizo wametakiwa kurudi mara moja katika vituo vyao vya kazi ili kuhakikiwa.

Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na uongozi wa Halmashauri hiyo ikiwa ni katika kutekeleza agizo la Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli la kuhakiki watumishi wote wa umma waliopo kwenye orodha ya malipo ya watumishi wa umma ndani ya siku 15 ili kubaini watumishi hewa wanaoendelea kulipwa mishahara.

Akizungumza kwa njia ya simu msemaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke Bi Joyce Nsumba amesema zoezi hilo ni muhimu sana kwa watumishi hivyo basi watumishi wote wa Halmasahuri hiyo waliopo likizo na masomoni wanatakiwa kurudi katika vituo vyao vya kazi ili kuhakikiwa.

“Taarifa imeshatoka kwa watumishi wote kuwa wanatakiwa kuhakikiwa na kwa wale waliopo likizo na kwenye masomo wanatakiwa kurudi ili wahakikiwe na kuendelea na likizo na masomo yao kwani mara baada ya uhakiki huu kukamilika, majina ambayo yatakuwa hayajahakikiwa yatafutwa kwenye orodha ya watumishi,” Alisema Bi Joyce.

Bi Joyce Nsumba ameongeza kuwa mpaka sasa uhakiki unaendelea kwa makundi mbalimbali wakiwemo watumishi kutoka Idara ya Afya, Elimu, Fedha na Biashara, Kilimo,Mifugo,Ujenzi,na Maendeleo ya Jamii na mpaka sasa wameshahakiki zaidi ya watumishi 8,000.

Zoezi la uhakiki wa watumishi wa umma nchini limekuja mara baada ya uchunguzi uliofanywa katika mikoa ya Singida na Dodoma katika Halmashauri 14 na kugundulika kwa watumishi hewa 202 wanaolipwa mishahara na hivyo Mhe. Rais Magufuli kutoa agizo la kuhakiki watumishi wote katika Wizara, Mikoa, Wilaya, Idara, Taasisi na Wakala za Serikali ndani ya siku 15.
  • Taarifa ya Raymond Mushumbusi - MAELEZO