Waua mke na mume kwa ujira wa sh 600,000/= za mke mdogoMtu na mkewe, Nyanda Masele na Kwilabya Masasila, wakazi wa kitongoji cha Mawasiliano kijiji cha Mpeta wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma, wameuawa kwa kukatwa mapanga.

Inadaiwa mauaji hayo yalitekelezwa baada ya mke mdogo, Salome Igede, kukodi majambazi kwa Sh.600,000 kuwaua Masele na Masasila.

Akizungumza na Nipashe juzi, mtoto wa marehemu hao, Ngolo Yanda, alisema tukio hilo lilitokea Machi 9, saa 6:00 usiku, katika kitongoji hicho, baada ya watu kadhaa kuvamia chumba cha wazazi wake waliokuwa wamelala na kuwashambulia kwa mapanga hadi kuwaua.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma, Ferdnand Mtui, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema watu watano wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za mauaji, akiwamo mke mdogo wa marehemu na mtoto mwingine wa marehemu.

“Nilisikia mlango unagongwa kwa nguvu na nikasikia kelele na sauti ya mama inaita, Ngolo, Ngolo njoo unisaidie, halafu nikasikia sauti nyingine ikisema tulia wewe na tukawa tunaona tochi zinamulika ndani,” alisema Yanda.

Alisema baada ya muda kimya kikatanda na ndipo akatoka chumbani kwake kwenda chumba cha wazazi ambako alikuta wote wakiwa chini huku damu zimetapakaa kwenye miili yao.

Ndipo alipopiga kelele na kumuita kaka yake Juma Nyanda aliyekuwa amelala nyumba nyingine, alisema.

Naye mtoto wa kiume wa marehemu hao, Nyanda, alisema wakati anaamka baada ya kugongewa mlango na dada yake, alikuta majambazi hao wameshaondoka na akaomba msaada kwa majirani.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpeta, Raphael John, alisema chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina.

Alisema walibaini ni ushirikina baada ya majambazi hao kukamatwa na polisi wa kituo cha Nguruka kisha kukiri kufanya mauaji hayo kwa kukodiwa na mke mdogo wa marehemu kwa Sh.600,000.

“Walijieleza walikuwa wamekubaliana malipo hayo na mke mdogo wa marehemu ambaye alimtuhumu mke mwenzie alikuwa anamloga kwa muda mrefu," alisema John na kuongeza, "Pia walidai aliwahi kuhangaika kubeba mimba ya miaka kumi bila kuzaa.”