Loading...
Sunday

Waziri aandaa mkataba wa kazi kwa idara; Aonya matumizi ya 'internet kwa matumizi ya hoyo'Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasialino, Profesa Makame Mbarawa, amewaweka roho juu watendaji wa Wizara yake kwa kuwaandalia mkataba wa malengo ya kiutendaji.

Mbarawa amesema Wakuu wa Taasisi na Idara zote za Wizara hiyo wataingia mkataba ikiwa ni hatua ya kuongeza ufanisi wa kazi kwa watumishi wa umma na atakayeshindwa kufikia malengo atafungashiwa virago.

Profesa Mbarawa alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na watumishi na wakuu wa Idara wa Wizara hiyo kutoka taasisi 29 ambapo aliwataka kila mtumishi kutumikia vyema nafasi yake na kuhakikisha anatambua wajibu wake wa kujenga miundominu imara na kufikia lengo la kuwa uchumi wa kati ifikapo 2020/2025.

Alisema kwa kuanza wamekubaliana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kukusanya Sh. trilioni moja badala ya Sh. bilioni 652 walizopanga kukusanya na kwamba Wakuu wa Idara watakaoshindwa kutekeleza malengo hayo watafukuzwa kazi.

Waziri alisema nafasi hizo watapewa watu wengine watakaoonekana kuwa na uwezo wa kumudu majukumu hayo na kufikia malengo hayo.

“Tunataka tuwe na mikataba ya kazi baina ya wenyeviti wa bodi na wakuu wa taasisi mbalimbali, ili idara itakayoshindwa kutimiza lengo tumhoji na kama sababu zake hazina mashiko atupishe na nafasi yake apatiwe mtumishi mwingine,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema sekta ya Mawasilino pekee ndio walipeleka mikataba yao ya kazi na alitumia nafasi hiyo kuzitaka mamlaka nyingine kutekeleza agizo hilo mara moja.

Profesa Mbarawa pia aliahidi kuwafukuza kazi mara moja watumishi watakaotumia nafasi zao kutoa maagizo ya kusaidia wazabuni katika wizara yake pindi atakapopata taarifa.

Alisema kuna baadhi ya watumishi wa sekta ya manunuzi wamekuwa wakifuta zabuni zaidi ya mara 10 na kuendelea kuzirudisha hivyo aliahidi kuwa atakayebainika tena atamfuta kazi.

“Tangu nimekuwa Wizara ya Mawasiliano kwa miaka yangu yote mitano sikuwahi na wala sitakaa niwahi kupitisha kimemo kwa wakuu wa idara kwa ajili ya kupitisha zabuni hivyo na mimi nikipokea taarifa za mtumishi anayepitisha zabuni kwa namna yoyote ile bila ya kuzishindanisha nitashughulika naye na sitakuwa na huruma hata kidogo nitaondoka naye,” alisisitiza.

Pia aliwasisitizia watumishi hao kuwa na uadilifu kazi na kila mtu kutekeleza majukumu yake, kuacha tabia ya kutumia huduma za mtandao kwa ajili ya shughuli zao binafsi.

“Hakikisheni mnakuwa waadilifu na muwe na huruma na mali za umma nimepata taarifa kuwa baadhi ya watumishi wanatumia huduma ya mtandao kwa ajili ya matumizi ya ovyo, hakikisheni mnaacha mara moja,” alisema.

Profesa Mbarawa pia alisema ataanzisha utaratibu wa kufanya mkutano na wafanyakazi wote wa wizara hiyo kila baada ya miezi mitatu kwa kutumia televisheni.

Pia alisema wanaandaa utaratibu wa mfumo wa mtandao kwa wakuu wote wa idara utakaowawezesha kupata taarifa za ripoti na mafaili yaliyoko katika ofisi zao ili kuondokana na uzembe wa watumishi wanaokalia mafaili ya watumishi.
 
Toggle Footer
TOP