Loading...
Monday

Yatokanayo: Katibu Mkuu CHADEMA, Dk Vincent Mashinji

Picha za awali za utambulisho wa Katibu mkuu wa CHADEMA, Dk Vincent Mashinji uliofanyika leo Machi 14, 2016 jijini Mwanza mara baada. (picha: GSengo blog)

GAZETI LA NIPASHE LIMEANDIKA

KATIBU MKUU MPYA CHADEMA ALIKUWA 'KICHWA' UKAWA


Licha ya Katibu Mkuu mpya wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, kutokuwa na jina kubwa katika ulingo wa siasa na wengi kumwona mgeni, ndiye aliyekuwa 'kichwa' (think tank) wa Ukawa, imefahamika.

Juzi, Chadema ilimteua Dk. Mashinji kuwa Katibu Mkuu mpya kushika nafasi ya Dk. Willibrod Slaa, aliyejiuzulu nafasi hiyo Julai 30, mwaka jana, kwa kile akichokieleza kuwa ni utaratibu kutofuatwa wa kumkaribisha Edward Lowassa, aliyehamia katika chama hicho kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, uteuzi wake umepokelewa kwa mtazamo tofauti kutokana na kutokuwa na jina kubwa katika ulingo wa siasa, lakini imefahamika kuwa ni mmoja wa watu waliofanikisha mipango mikakati ya Ukawa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kupata mafanikio makubwa, baada ya kuwa na wabunge 113 bungeni ikiwa ni wale wakuchaguliwa na viti maalumu.

Idadi hiyo ni kubwa zaidi kupatikana tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa kwanza unaojumuisha vyama vingi mwaka 1995.

Katika mafanikio hayo, Dk. Mashinji alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Sera na Wanataaluma wa Ukawa na ndio walioandaa Ilani ya Chadema katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Akielezea uwezo wake na anavyomfahamu, Mwenyekiti wa Kamati ya Sera na Wanataaluma wa Ukawa, Dk. Rodrick Kabangira, ambaye amefanya kazi kwa karibu na Dk. Mashinji, alisema ni mtendaji mwenye malengo ya kimkakati na kufuatilia kwa karibu anayoyatenda.

"Nilifahamiana naye mwaka 2011 tulipokuwa tunaandika majarida mbalimbali ambayo tuliyawasilisha Chadema kama la namna ya kuboresha sekta ya afya na baadaye kuandika ilani, lakini katika Kamati ya Ufundi ya Ukawa, tumefanya kazi pamoja. Namfahamu vizuri ni mtu sahihi kwa Chadema katika kuelekea mwaka 2020," alisema.

Alisema wakati wa kampeni za uchaguzi, alikuwa mzungumzaji wa namna Sera na Ilani ya Chadema inavyoweza kutekelezwa kwa kuwa anaijua kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho na kwamba kwa mwonekano ni mpole na anayezungumza taratibu, lakini anatoa neno zito.

AMWAGA SERA FURAHISHA

Akihutubia mamia ya wananchi wa Mwanza katika viwanja vya Furahisha jana, Dk. Mashinji alisema ataongoza kimkakati zaidi kwa kuwa na mabadiliko ya kimfumo ndani na nje ya chama kwa kujenga matawi ya chama katika kila eneo.

"Naagiza kila kata kuwe na kamati za ufuatiliaji palipo na diwani na ambako hakuna ili kuhakikisha masuala ya wananchi yanafuatiliwa kwa karibu katika sekta mbalimbali kama elimu, maji na mengine. Madiwani wafanye kazi, hatukuwapeleka kuuza sura bali kusimamia kwa karibu maslahi ya wananchi," alisema

Aidha, aliagiza wabunge wote wa Ukawa kugeuza suala la Katiba Mpya ni agenda ya kudumu kwa kila dakika wanazopata ndani ya Bunge na kwamba kikosi cha kimkakati ndani ya chama kitaimarishwa katika utekelezaji wa shughuli zinazolenga kutetea maslahi ya wananchi.

Dk. Mashinji alisema ni lazima maeneo yanayoongozwa na Ukawa, ustawi wa wananchi uonekane na kwamba mambo yatakayosimamiwa ni mabadiliko ya wananchi ili washike hatamu ya chama na viongozi washirikiane nao.

Lingine ni kujiandaa kwenda kwa kasi kwani kwenda pole pole jua litazama na giza kuingia na kushindwa kusonga mbele kufikia malengo ya kuchukua dola m,waka 2020.

ATAJA VIPAUMBELE VYAKE

Dk. Mashinji ameweka wazi vipaumbele vitano ambavyo ataanza navyo baada ya kuingia ofisini katika kuhakikisha Chadema inafanikiwa kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, ikiwamo kukipeleka chama hadi kwa wananchi wa kawaida.

Akizungumza jana na Nipashe, aliwashukuru wajumbe wa Baraza Kuu waliompigia kura za ndiyo kwa asilimia 100 huku alitaja vipaumbele hivyo kuwa ni utekelezaji wa ilani ya Chadema katika halmashauri wanazoongoza, kupinga rushwa na makundi yanayotaka kumea, Katiba Mpya na kusimamia mabadiliko ndani na nje ya chama.

Alisema wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu kaulimbiu kubwa ya chama hicho ilikuwa mabadiliko ambayo hayajahitimishwa kwa kushindwa uchaguzi bali yametajwa katika ilani na yatatekelezwa kwa vitendo.

"Baraza Kuu na wengine bado tuna jukumu la kuwasimamia na kuwatetea Watanzania. Tusiogope licha ya watu kunakili mambo yetu na kutaka kuyatekeleza, hawawezi kutufikia sisi ambao ndio tunajua utekelezaji wake, twendeni katika kiini cha tatizo," alisema.

Dk. Mashinji ambaye aliambiwa uteuzi wake na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, wakiwa hotelini, alitaja kingine ni kukisogeza chama kwa wananchi zaidi kwani kufanya operesheni mbalimbali na mikakati ya kichama kwa kuwa mtaji mkubwa wa chama ni watu.

"Msingi wa chama uko chini, mtaji wa chama ni watu na siyo vipeperushi, magari. Hezekiah Wenje akishinda kesi si yeye ni Wananyamagana wameshinda, hivyo ni lazima tuwafikie wannachi huko waliko ili 2020 tuweze kushinda uchaguzi,"alisisitiza.

Alisema kazi iliyoko mbele yake si nyepesi, lakini watafikaje Ikulu itajulikana baada ya kufika mtoni, na kuwataka wanachama na viongozi kutoogopa polisi na vyombo vingine vya dola vinavyotumika kuwanyanyasa.

Kipaumbele kingine ni kusimamia mabadiliko ya Katiba Mpya ambayo yalianza kwa kuhakikisha mifumo iliyopo inabadilika kwa kuwa imekuwa chanzo kikubwa cha kuwanyima haki za msingi na ukuaji wa uchumi wa Watanzania.

"Hatuwezi kupiga hatua kubwa kimaendeleo kwa katiba tuliyonayo au iliyopendekezwa na Bunge Maalumu. Tuna matatizo nyeti ya kitaifa ambayo chanzo chake kikubwa ni mfumo. Ukiangalia suala la rushwa utabaini shida ni mfumo uliopo na ambao tunahitaji kuubadili kwa kutumia Katiba Mpya, hivyo nikiiingia ofisini litakuwa kipaumbele," alisema.

Aliongeza kuwa: "Lengo letu ni nguvu ya umma, tuiwezeshe kutambua haki zao mfano mgogoro mkubwa baina ya wenyeviti na mameya wa halmashauri ni wakuu wa wilaya na mkoa kuingilia utendaji wa halmashauri kwa kuwa kuna mifumo ya kikoloni kwa Katiba Mpya tutaiondoa."

Dk. Mashinji alisema lingine ni kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chadema 2015, ambayo alishiriki kuiandaa tangu mwanzo na anajua inavyoweza kutekelezwa kivitendo katika halmashauri zinazoongozwa na Chadema katika kuleta maendeleo endelevu ya wananchi.
Katibu huyo ambaye ni Daktari wa Binadamu, alisema pia ni lazima kuwa pamoja katika ujenzi wa chama na kushika hatamu, huku akitumia mfano wa maji ambayo huenda pamoja na yanapofika kwenye maporomoko hushuka pamoja.

Jambo lingine ni kupinga rushwa na makundi ambayo yameanza kumea ndani ya chama, ili kuendelea kukitofautisha chama hicho na kingine na kudhihirishia umma kuwa wamejipanga kushuka dola ifikapo 2020.

WABUNGE CHADEMA WAMZUNGUMZIA
Mbunge wa Moshi Mjini, Jaffary Michael, alisema chama kimepata mtu sahihi kwa wakati sahihi kwa kuwa moja kwa moja inakwenda kuvunja propaganda zilizopandikizwa kuwa ni chama cha Kaskazini.

Alisema ataleta mawazo mapya ndani ya chama kuliko kuendelea na watu wale wale wenye mawazo yale yale na akipewa ushirikiano ataweza kuvaa viatu vya Dk. Slaa, kwa kusimamia maono yake ambayo alitumia muda wake mwingi katika ujenzi wa chama imara.
Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro, alisema uwezo wa mwenyekiti wa taifa kuficha siri ni ushahidi tosha kuwa chama kinasiri na intelejensia ya hali ya juu na kina sifa za kushika dola kwa mwaka 2020.

Alisema Dk. Mashinji si mgeni katika utendaji serikalini na harakati mbalimbali ikiwamo kutetea maslahi ya madaktari na sekta ya afya ambayo inakabiliwa na matatizo mengi hadi sasa, hivyo kwa kumtumia wataweza kunyonya ujuzi na kuupeleka katika halmashauri zinazoongzwa na Chadema.

Naye Mwalimu alisema siku zote duniani hakuna mbadala wa mtu kwa kuwa kila mmoja ana uwezo, uimara na udhaifu wake, kinachotakiwa ni kutekeleza majukumu kwa viwango vinavyotakiwa.

"Nimeshika nafasi ya kaimu katibu, haikuwa kazi rahisi kwa kuwa nafadi hii ni nyeti sana, kila mtu anakuangalia wewe, lakini naamini bosi mpya tuliyempata ni mtu imara, anaijua Chadema siyo kwa kuisoma, bali kushiriki ikiwamo kuandika ilani na machapisho mbalimbali," alibainisha.

Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Kiwelu, alisema kwa kiongozi huyo anaiona Chadema mpya kwa kuwa ni mtu mwenye uwezo na anafahamu anachokitenda.

Awali, akizungumza wakati wa kumuombea kura kwa Baraza Kuu, Mbowe, alisema ameona Dk. Mashinji anastahili kuendeleza guruduma la chama hicho kwa kuwa ni mtu makini, mwenye maono na anayejua atendalo.

Mjumbe wa Kamati Kuu, Lowassa, alisema Mbowe amedhihirishia umma kuwa uamuzi wake ulikuwa makini sana kwa kuwa ameleta mtu kijana na shupavu hasa katika nyakati za mabadiliko.

"Tumekupa imani kubwa, chama kinachofuata kuongoza nchi ni Chadema, lengo letu ni kukamata dola na rafiki yetu wa kweli ni kutuwezesha kufika Ikulu 2020," alisema.

WADAU WAPONGEZA

Uteuzi wa Dk. Mashinji kuwa Katibu Mkuu wa Chadema umepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wanasiasa na wasomi nchini.

Baadhi ya makundi hayo, wameeleza kuwa Chadema imemteua mtu ambaye alikuwa hafahamiki kwa wananchi, hivyo imekuwa ‘surprise’ kwa wanachama wao, kwa kuwa walikuwa wanatarajia kusikia jina kubwa.

Mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya siasa, Abdulhakim Atiki, alisema pamoja na kuwa Mashinji hafahamiki kwa wananchi, lakini alikuwa ni mmojawapo wa wanachama walioshiriki katika kutengeneza Ilani ya Ukawa wakati wa uchaguzi mkuu.

Alisema ni kijana mwenye uwezo wa kuongoza Chadema kama makatibu wakuu wengine waliotangulia.

Alisema tangu kuondoka kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Aman Kabourou, aliyetokea Kanda ya Ziwa, hakukuwa na katibu mkuu mwingine aliyetokea upande huo, hadi alipoteuliwa Mashinji.

“Nadhani Chadema wamezingatia ukanda zaidi, tena ukizingatia wakati wa uchaguzi mkuu maeneo ya Kanda ya Ziwa hawakufanya vizuri, hivyo wamemteua Mashinji ili kujiimarisha zaidi,” alisema.

Naye mwanazuoni kutoka Chuo cha Diplomasia, Israel Sosthenes, alisema hamfahamu Dk. Mashinji vizuri, lakini Chadema hadi kumteua kushika nafasi hiyo ya juu watakuwa wako sahihi na uhakikia na mtu huyo.

Alisema katibu mkuu ndiye mtendaji mkuu katika usimamizi wa chama, na kwamba ni mapema kumzungumzia kama ataweza au la.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Anna Mghwira, alisema hakuwa anamfahamu Dk. Mashinji, na kwamba amemfahamu mara baada ya kuteuliwa.

Alisema Chadema ni chama kikubwa nchini, hivyo hakiwezi kumtemteua mtu kushika nafasi hiyo kubwa ndani ya chama kama uwezo wake ni mdogo.

Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Siasa ya Sayansi, Dk. Bashiru Ally, alisema hamfahamu Dk. Mashinji utendaji wake kiundani, kwa kuwa ni mara ya kwanza kumsikia.

Alisema anawafahamu viongozi wakuu wote wa Chadema, alisema Dk. Mashinji hakuwahi kumwona kumwona wala kumsikia akishiriki katika masuala ya chama, alisema kama aliwahi kushiriki itakuwa ngazi za chini.

Alisema uteuzi wake unaweza kuwa na faida ndani ya Chadema, kwa kuwa ni mtu ambaye hana mambo mengi kama walivyo viongozi wengine wakubwa ndani ya chama hicho.

Aliongeza kuwa, Dk. Mashinji ni jina jipya pia, ni kijana ambaye anaweza kumudu kazi ya ukatibu mkuu wa chama.

GAZETI LA MWANANCHI LIMEANDIKA


MASHINJI - NINA DHAMIRA KUSHIKA DOLA 2020


Katibu Mkuu mpya wa Chadema, Dk Vincent Mashinji ametamba kuwa licha ya umri mdogo alionao na kipindi kifupi cha uanachama ndani ya chama hicho, ana uwezo, nia, dhamira na lengo la kukiandaa kushika dola mwaka 2020.

“Nilikuwa mwanachama wa Chadema asiye na kadi ya uanachama kwa kipindi kirefu, baadaye bila malipo, kushawishiwa wala kutumwa, mimi na wasomi wenzangu tuliandaa na kutekeleza mikakati ya kukijenga chama nje ya mfumo rasmi wa chama,” ni kauli ya Dk Mashinji wakati akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Chadema juzi usiku.

Daktari huyo wa binadamu aliyetambulishwa jana kwenye mkutano wa hadhara jijini Mwanza, alisema baada ya kukutana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, yeye na wenzake walikutanishwa na aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa.

“Baada ya kutusikiliza na kuelewa mikakati yetu, Dk Slaa alituhoji iwapo sisi ni wanachama hai wenye kadi za Chadema. Swali lililotushtua kwa sababu miongoni mwetu hakuna aliyekuwa na kadi,” alisema na kuendelea.

“Tulimjibu Dk Slaa kuwa uanachama wetu uko mioyoni; hoja aliyoikubali, lakini akatuelekeza kujiunga na kuchukua kadi rasmi kwa sababu yapo majukumu ambayo hatuwezi kuyatekeleza bila kuwa wanachama hai,” alisema na kuongeza:

“Nilichukua rasmi kadi ya Chadema Machi Mosi, 2013 kutekeleza ushauri wa Dk Slaa,” alisema Dk Mashinji, mwenye umri wa miaka 43.

Ilani ya chama

Aliongeza: “Kwa sababu nilishiriki kuandaa ilani ya uchaguzi na sasa nimekabidhiwa jukumu la kuwa Katibu Mkuu wa chama, nitasimamia utekelezaji wa ilani hiyo katika halmashauri zote za wilaya zinazoongozwa na Chadema.”

Aliwataka mameya na wenyeviti wa halmashauri zilizo chini ya chama hicho kuisoma, kuilewa na kuitekeleza ilani hiyo aliyosema sehemu kubwa imeigwa na CCM ili kuwaonyesha wananchi tofauti ya vyama hivyo kivitendo linapokuja suala la maendeleo na maslahi ya umma.

Mshikamano kuelekea 2020

Akizungumzia mkakati wake kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, Dk Mashinji alisema dhamira yake kuu ni kuwaunganisha wanachama, viongozi, wapenzi na wafuasi wa Chadema kwa kutoa fursa kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake kufikia lengo la kushika dola miaka mitano ijayo.

“Kila mwana Chadema aweke lengo la kukijenga chama tayari kwa ushindi 2020. Tuige tabia ya maji mtoni ambayo kila tone dogo hujiunganisha na tone lingine na kufanya mafuriko makubwa yanayotembea,” alisema.

Mashinji ni nani?

Akisimulia historia yake fupi, Dk Mashinji alisema alizaliwa mjini Musoma mkoani Mara, makuzi yake ni jiji la Mwanza na kusomea Uganda namna ya kuishi katika mazingira magumu, zikiwamo vurugu.

“Ninachomaanisha ni kutuma salaam kwa watani zetu kuwa mimi siyo mtu legelege hata kidogo,” alisema na kuibua shangwe ukumbini.

Alisema kwa kuzaliwa mkoani Mara, amefanikiwa kubeba tabia ya ujasiri, uthubutu na kutohofia lolote wanalosifika kuwa nalo watu wa mkoa huo na papo hapo amerithi tabia ya upole, lakini wenye msimamo wa jamii ya mkoa wa Mwanza na kuahidi kuzichanganya pamoja katika uongozi wake.

Maoni ya wachambuzi

Wakitoa maoni yao wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema chama hicho kinahitaji mtu atakayekijenga ili kiendelee kuwa chama chenye nguvu nchini.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema chama hicho kinahitaji mtu mwenye msimamo na uwezo wa kukabiliana na mbinu kali za chama tawala CCM.

Alisema katibu mkuu ndiye mtendaji wa chama, kwa hiyo nafasi hiyo inahitaji mtu mwenye uwezo wa kuwaleta watu pamoja na kukifanya chama kuwa kimoja.

“Siwezi kumzungumzia huyu aliyeteuliwa jana (Mashinji) kwa sababu simfahamu. Bila shaka Baraza Kuu limeona anafaa ndiyo maana amepitishwa. Wengi tulitarajia watu wenye majina makubwa kushika nafasi hiyo,” alisema Profesa Mpangala.

Hata hivyo, alisema hajashtushwa na uamuzi huo kwa sababu waliompitisha wanamfahamu vizuri na wanaamini atatekeleza majukumu yake vizuri.

Katibu Mkuu wa NCCR – Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema nafasi ya katibu mkuu wa chama inahitaji mtu mkali ambaye atawasimamia watendaji wengine wa chini yake, maadili na katiba ya chama chake.

“Siwezi kumzungumzia huyo (Mashinji) moja kwa moja kwa sababu simfahamu. Lakini ana kazi kubwa ya kukijenga chama chake na kuhakikisha kwamba katiba ya chama inafuatwa,” alisema.
Nyambabe aliongeza kuwa ana imani Mashinji atafanya kazi vizuri kwa sababu viongozi wa juu wa Chadema wameridhia uteuzi wake.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Emily Jonathan alisema hana uhakika kama Mashinji anaweza kuvaa viatu vya Dk Slaa kwa sababu katibu huyo mkuu wa zamani wa Chadema alikuwa na nguvu na ushawishi wa kipekee katika uongozi.

Alisema pengo la Dk Slaa limeonekana wakati wote tangu alipoondoka Chadema. Alisema mtu wa kuziba pengo hilo anatakiwa kuwa na haiba yake au kuwa na mtindo mwingine wa uongozi ambao utamfanya kuwa na ushawishi kwa wanachama na viongozi wenzake.
  • Imeandikwa na Peter Saramba na Peter Elias


GAZETI LA MTANZANIA LIMEANDIKA

Mbowe atoboa siri uteuzi Dk. Mashinji


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ametoboa siri ya kumteua Dk. Vincet Mashinji kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Mbowe alisema amemteua Dk. Mashinji kutokana na kiwango chaka cha elimu pamoja na ushujaa wake wa kupambania maslahi ya madaktari kwa kuitisha migomo.

Akihutubia maelefu ya wakazi wa Jiji la Mwanza jana katika viwanja vya Furahisha wakati wa kumtambulisha kiongozi huyo, Mbowe alisema Chadema imemteua Dk. Mashinji kutokana na sifa, uwezo na si kwa sababu ya ukabila.

Alisema kwa uteuzi huo, ametoa somo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuteua mtu ambaye baba yake si kigogo wa chama, tofauti na wao ambao wamekuwa wakitoa nafasi kwa watoto wa vigogo au kwa misingi ya rushwa.

Alisema Dk. Mashinji ana kiwango cha juu cha elimu na si mwoga jambo ambalo anaamini litamsaidia kuendesha chama.

“Baada ya kupekuwa historia yake tulibaini ni mmoja wa wale walioanzisha mgomo wa madaktari nchi nzima, kisha akafukuzwa akiwa na wenzake kina Dk. Steven Ulimboka.

“Tulipogundua aliongoza mgomo tulijua si mwoga, kama alikomaa kutetea maslahi ya madaktari na wenzake, basi tuliona anafaa kukomaa kutetea Watanzania… si mtoto wa Mbowe wala mtoto wa Lowassa (Edward).

“Tumeamua kumteua mtu mwenye sifa na uwezo pamoja na karama za uongozi, tumemwibua kutoka chini, angekuwa CCM angelazimika kuhonga mpaka ndugu zake ili ashinde nafasi hii,” alisema.

Alisema uteuzi huo, unaonyesha dhamira ya Chadema ya kugawana madaraka na kubainisha ndani ya Kamati Kuu wapo watu ambao wana sifa za kuwa makatibu wakuu, lakini wana majukumu mengine.

Alisema wamekubaliana walioko bungeni waendele kupambana huko ili mambo mengine yafanywe na katibu.

Dk. Mashinji

Kwa upande wake, Dk. Mashinji akizungumza baada ya kutambulishwa, alisema jukumu la kwanza ambalo linamkabili ni kujenga chama hicho kimkakati.

Alisema atafanya kazi zake kisasa kwa lengo la kuongeza ufanisi.

Alisema tayari ametoa maelekezo kwa madiwani wa Chadema katika halmshauri zote kuanza kuunda kamati za ufuatiliaji za wananchi ambazo zitakua na jukumu la kufuatilia utendaji na utekelezaji na maendeleo kwa kata husika.

“Huu ndiyo mkakati wangu wa kwanza naanza kuutoa hapa, umebeba lengo la la kuisukuma Chadema mbele na kufanikisha kushinda na kushika dola mwaka 2020.

Lowassa

Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa aliwashukuru wananchi wa Mwanza kwa kumpigia kura wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka jana.

Alisema kura nyingi alizopata ni kielelezo cha kukubalika kwa wananchi hao, japokuwa waliotangaza walisema hazikutosha.

Alisema imani yake ni kujipanga zaidi ili mwaka 2020 washike dola na kwamba wamepata katibu mkuu mpya kijana ambaye atasimamia chama vilivyo na anaamini watafanya vizuri zaidi.

Wenje

Akizungumzia uchaguzi, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Ezekiel Wenje alisema kulingana na matokeo yalivyo, japo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), haikumtangaza anatambua yeye ndiye mshindi na ndiyo maana amekwenda mahakamani kufungua kesi.

Aliomba wafuasi wa chama hicho kumwombea, wakati huu ambao kesi yake inaendelea kusikilizwa mahakamani.

“Ukitaka kujua nani kashinda tupite mtaani mimi na huyo Mbunge wa CCM (Stanslaus Mabula), utaona yeye anatembea na polisi, mimi napita nakatiza mitaa, hii maana yake aliyetangazwa anatembea na hofu ya Mungu,” alisema.

Mwalimu


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar ) Salum Mwalimu alisema uteuzi wa Dk. Mashinji umeonyesha ukomavu ndani ya chama na namna ambavyo inaweza kuibua watu wenye karama za uongozi.

“Niseme CCM imezoea kununua watu wa upinzani, kila ikinunua sisi tutaibua wapya kama tulivyofanya kwa Dk. Mashinji,” alisema.

Chadema wapongezwa uteuzi wa Dk. Mashinji


BAADHI ya wanasiasa na wananchi wa kada mbalimbali wamepongeza hatua ya Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa kupitisha uteuzi wa Dk. Vicent Mashinji, kuwa katibu mkuu wa chama hicho.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro, alisema uteuzi wa Dk. Mashinji umekuwa wa siri na umekiletea chama hicho heshima ya kipekee.

Alisema hatua ya uteuzi wa Dk. Mashinji, ambaye ameteuliwa kushika nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Dk. Willbrod Slaa, umekiletea heshima kuingia katika historia kwa chama hicho.

Dk. Slaa, alitangaza kujiengua katika nafasi hiyo na kujiweka kanda na siasa na kwa sasa anaishi ughaibuni nchini Canada.

“Vyama vya upinzani katika hili la Dk. Mashinji tumejifunza kuwa wapinzani wana uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi muhimu kwa siri kuliko chama tawala cha CCM na serikali yake,” alisema Mtatiro.

Alisema watu mbalimbali walikuwa wanashinda kwenye mitandao wakitabiri jina la Katibu Mkuu huku wakipambanua weledi na uwezo wa katibu wanayemtaka lakini cha ajabu wote walikosea.

“Kila mmoja aliyetabiri alikosea na huenda wote waliokosea kama wangewekeana ahadi huenda wangemlipa fedha nyingi na angeweza kuwa bilionea Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwakuwa wameliwa,”alisema Mtatiro.

Mtatiro alisema kwa wanaomfahamu Dk. Mashinji ni mtu makini ana uwezo wa kukisaidia chama hicho kwa kuwa anafahamu siasa za kisasa na ataipeleka Chadema katika hatua za juu zaidi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Sanaa na Uhamasishaji Ofisi ya Katibu Mkuu (Chadema), Fullgency Mapunda, alisema amefarijika na uteuzi na Baraza Kuu la Taifa kumchagua kiongozi makini na anaamini atafanya mabadiliko makubwa yatakayosaidia kukivusha chama hicho.

“Kuchaguliwa kwa Dk. Mashinji kamati Kuu kwa kushirikiana na mwenyekiti wa chama hawakufanya makosa kwani wana amini mipango iliyokuwa imekwama inakwenda kutekelezwa,”alisema Mapunda.

Naye, Ommy Herman alisema yeye kama mwanaharakati hawezi kuacha kusifia uteuzi huo kwa kuwa imefuta tetesi za watu waliodai aliyekuwa Waziri Mkuu, Fredrick Sumaye ndiye angekuwa Katibu Mkuu.

Kwa upande wake Chriss Zephania, alisema hana shaka na uteuzi wa Dk. Mashinji, kwa kuwa anaamini kamati tendaji haikukurupuka.

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP