Zahanati ya Msoga yapandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya

Naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla (kushoto) akiongozwa na Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Msoga, Dk. Juliet Lema wakati wa ukaguzi huo. Kulia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Dkt. Beatrice Jane Byalugaba.(Picha zote na Andrew Chale, Modewjiblog)

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeipa hadhi ya kuwa Hospitali Wilaya iliyokuwa Zahanati ya Msoga ambayo tayari imekamilisha jengo lake jipya la Hospitali hiyo inayotarajia kuanza kuanzia Mwezi Aprili mwaka huu.

Akitoa maagizo hayo baada ya ukaguzi wa timu ya wataalam kutoka Wizara hiyo ya Afya pamoja na Naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla waliofanya hivi karibuni katika Hospitali hiyo, ameeleza kuwa kuanzia Mwezi Aprili ianze kazi kwa kuanza na huduma za wagonjwa wa nje na baada ya miezi mitatu itaendeshwa na huduma zote muhimu ikiwemo kulaza wagonjwa.

“Naagiza ndani ya mwezi mmoja ianze kazi na huduma za kawaida. Baada ya miezi mitatu itaendelea na huduma muhimu zote katika Hospitali hii mpya ya Wilaya” alieleza Dk. Kigwangalla wakati wa kutoa hitimisho lake kwa wasimamizi wa Zahanati hiyo ya Msoga.

Dk. Kigwangalla na timu yake waliweza kukagua majengo ya Hospitali hiyo mpya ambapo na kuona inakidhi vigezo ya kuwa Hospitali ya Wilaya.

Majengo ya Hospitali hiyo yapo katika Kituo cha afya cha Msoga, kata ya Msoga, Chalinze Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani, Ni miongoni mwa Hospitali itakayokuwa ya kisasa na kubwa.

Aidha, kutokana na matukio mengi ikiwemo ya ajali nyingi zinazotokea mara kwa mara katika barabara ya Chalinze-Segera, Hospitali hiyo ya Wilaya itakuwa msaada na itawezesha kupunguza mzigo wa vituo vya afya vya vya jirani ikiwemo Lugoba, Chalinze na vinginevyo ndani ya Halmashauri hiyo yaa mji mdogo wa Chalinze.


Jengo hilo la Hospitali ya Wilaya inavyoonekana kwa nje


Waziri Dk. Kigwangalla akiwa na timu yake wakikagua eneo hilo la Hospitali ya Wilaya. Jengo linaloonekana nyuma awali lilipangiwa kuwa sehemu ya kuhifadhia maiti (mortuary) hata hivyo wamebadilisha matumizi yake na Mochwari itajengwa mbali kidogo na hapo ilikutoa naafasi kubwa kwa kujengwa mochwari ya kisasa.


Ukaguzi huo ukiendelea.


Dk. Kigwangalla akisaini kitabu cha wageni katika Zahanati ya Msoga mara baada ya kufanya ukaguzi na kuagizia majengo mapya ya Hospitali hiyo kuanzia mwezi ujao wa Aprili yaanze kutumika kama Hospitali ya Wilaya ambapo Madawa na vifaa vinatarajiwa kupelekwa muda wowote kuanzia sasa.