Loading...
Tuesday

Ziara na maagizo ya WM Majaliwa akiwa Mkoani KageraWAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kagera na kumpa siku tano Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bw. Adam Swai amletee taarifa juu matumizi ya sh. Milioni 80 ambazo ni fedha za UKIMWI.

Pia amemtaka ifikapo Machi 20, nwaka huu awasilishe taarifa nyingine ya matumizi ya sh. Milioni 40 za ukarabati wa jengo la wagonjwa maalum (Grade A)

Ametoa agizo hilo leo asubuhi (Jumanne, Machi 15, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo baada ya kutembelea maeneo kadhaa yakiwemo wodi ya watoto, wodi ya wazazi, chumba cha wagonjwa mahututi (ICU ) na chumba cha kuhifadhia maiti.

"Kulikuwa na frsha za ukimwi sh. Milioni 80 ambapo kila mtumishi alipaswa kupata sh. 200,000/- lakini ninyi mmewapa sh. 80,000 /-. RAS fedha hizi zimeenda wapi? Nataka uniletee taarifa ofisini kwangu Dar es Salaam ifikapo tarehe 20 mwezi huu," alisema huku akishangiliwa.

"Kwa mujibu wa taarifa ya CAG pale grade A kuna mgogoro wa sh. milioni 40. Wewe taarifa unayo lakini hujaifanyia kazi yoyote. Nataka tarehe 20 nayo hii pia niipate na nione umetoa mapendekezo gani."

Kuhusu tatizo la madaktari katika hospitali hiyo, Waziri Mkuu alisema atawasiliana na Waziri wa Afya ili madaktari watano ambao wanasubiri ajira rasmi lakini wameanza kazi kwa mkataba hospitali hapo wapewe ajira rasmi. Pia alisema amebaini upungufu wa madaktari bingwa uliopo katika hospitali hiyo.

Pia aliahidi kufuatilia maombi yao ya gari la wagonjwa hasa ikizingatiwa kuwa anayo maombi kama hayo kutoka hospitali za Mawenzi (Kilimanjaro), na Ligula (Mtwara).

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwapongeza watumishi wa hospitali hiyo kwa huduma zao nzuri wanazotoa kwa wagonjwa. "Nineridhishwa na kauli walizotoa wagonjwa juu yenu. Tofauti na hospitali nyingine nilizopita, wao wamesema hawajatozwa fedha ili wapatiwe dawa. Nimefarijika sana."

"Endeleeni kuwa na huruma kwa wagonjwa. Endeleeni kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa. Hawa wagonjwa hawakuogopa kuelezea hisia zao. Wamesema kwa uwazi kabisa kwamba mnawajali," alisema.

Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Thomas Rutachunzibwa alisema hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa madaktari bingwa pamoja na madaktari wa kawaida.


"Tunao madaktari 10 lakini wanaohitajika ni 30. Tunao madaktari wasaidizi wanane lakini wanaohitajika ni 23 na madaktari bingwa waliopo ni watatu tu lakini wanaohitajika ni 24. Tunaomba tupatiwe watumishi hawa ili tuweze kutoa huduma kulingana na matarajio ya wananchi wetu," alisema.

Akifafanua kuhusu mahitaji ya hospitali hiyo, Dk. Rutachunzibwa alisema wanahitaji sh. bilioni 1.8 kwa mwaka bila ya kuweka mishahara ili waweze kufanya kazi yao kwa umakini. "Tunahitaji sh. milioni 802 kwa ajili ya matumizi ya kawaida lakini tunachopokea hivi sasa ni sh. milioni 299 ambayo ni sawa na asilimia 30 ya mahitaji yetu."

"Bajeti ya dawa tuliyotenga ni sh. milioni 960 lakini tunapokea sh. milioni 143 ambazo kiuhalisia zinatosha kwa matumizi ya miezi miwili tu. Tumelazimika kufanya marekebisho ya bei za dawa kwa ridhaa ya Bodi ya hospitali ili tuweze kumudu kutoa huduma kwa wananchi," alisema.

Alisema ili kubana mianya ya upotevu wa mapato, wanahitaji kuwa na kompyuta 15 lakini hadi sasa wamefanikiwa kununua kompyuta mbili tu ambazo ziko Grade A na idara ya wagonjwa wa nje (OPD) ili kuimarisha utaratibu wa ukusanyaji mapato.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMANNE, MACHI 15, 2016.WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aende Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kufanya upya tathmini na kukagua ugawaji wa viwanja 843 kwenye manispaa hiyo.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa agizo hilo jana (Jumapili, Machi 14, 2016) wakati akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadharauliofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa wa Mayunga mjini Bukoba. Alifikia hatua hiyo baada ya wananchi kubeba bango lenye ujumbe kuelezea kutopewa viwanja hivyo vilivyopimwa na Manispaa ya Bukoba. Viwanja hivyo vilipimwa na kugawiwa kwa wananchi ambao baadhi yao baada ya kulipa fedha, hawajapewa viwanja hivyo ikiwa ni takriban miaka zaidi ya 10.

Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Kagera, Waziri Mkuu alilazimika kumpandisha jukwaani Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Bw. Wallace Karia ili atoe maelezo ya nini kimekwamisha wananchi kupewa viwanja hivyo. Katika maelezo yake, Bw. Karia alisema mwaka 2003, vilitengwa viwanja 843, kati ya hivyo 352 vilikuwa eneo la Kyabitembe, 137 Ihungo na
Rwome na vingine 132.

Bw. Karia ambaye hana muda mrefu tangu ahamishiwe katika manispaa hiyo, alisema kumbukumbu za ofisi zinaonesha kuwa viwanja 182 ndio wahusika hawajapewa, na viwanja vingine 85 vilikuwa havijapimwa eneo la Kilimahewa na Kashai, huku kukiwa na vingine 5,000 vya mradi.

Aliongeza kuwa walitarajiwa kuwalipa wananchi hao katika mwaka wa fedha 2016/17; kauli ambayo ilisababisha kelele kutoka kwa wananchi waliohudhuria mkutano huo wa Waziri Mkuu. Kutokana na hilo, Waziri Mkuu aliingilia kati na kumueleza Mkurugenzi huyo kuwa kelele hizo zinaashiria kuwa watu hao hawajaridhishwa na majibu yake.

Alisema anafahamu kuwa mkurugenzi huyo na meya ni wapya, lakini akawaagiza ndani ya mwezi mmoja, kufanya mapitio ya viwanja hivyo 843, na hasa watu 182 ambao hawajapatiwa viwanja wahakikishe wanawapatia kwa sababu viwanja vipo.

“Rais mstaafu alikuja hapa na kupewa kilio cha kupunjwa fedha. Najua wakati huo mtasema ninyi hamkuwepo. Wewe (MD) na Meya wako mkae na kupitia mikataba na mafaili. Nyie na mkoa mkae pamoja na kujua vile viwanja vilivyochukuliwa na JWTZ. Nitamleta CAG hapa, ndani ya mwezi mmoja afanye mapitio ya viwanja tu,” alieleza Waziri Mkuu na kushangiliwa na maelfu ya wananchi.

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu pia aliwahakikishia wakazi wa Manispaa ya Bukoba kuwa watalipwa fidia zao baada ya kukubali kupisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya sh. bilioni 31. Waziri Mkuu aliendelea na ziara yake ya siku tatu mkoani Kagera kwa
kutembelea wilaya za Misenyi na Karagwe na leo atakuwa wilayani Ngara.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MACHI 15, 2016.


Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akimsalimia Pedelia Erenius na mwanwe Alia James( miezi saba) wakati alipotembelea wodi ya wanawake na watoto katika hospitali ya mkoa wa Kagera mjini Bukoba Machi 15, 2016.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na madaktari na waguzi wa hospitali ya mkoa wa Kagera hospitalini hapo mjini Bukoba Machi 15, 2016.
Baadhi ya Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya mkoa wa Kagera wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakti alipozungumza nao hospitalini hapo mjini Bukoba Machi 15, 2016.

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akiwasalimia wnanchi wa eneo la Benaco wilayani Ngara akiwa katika ziara ya mkoa wa Kagera Machi, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipewa kahawa iliyoyokaangwa maarufukwa jina la akamwani ikiwa ni mapokezi ya kimila ya Wahaya wakati alipokwenda nyumbani kwa Waziri wa Zamani wa Ardhi, Profesa Tibaijuka mjini Muleba kutoa pole kufuatia msiba wa mama yake mzazi, Aulelia Kajumulo Machi 15, 2016.

  • Picha: Ofisi ya Waziri Mkuu
 
Toggle Footer
TOP