Loading...
Saturday

Akamatwa na malighafi magendo kutoka nje na kuiweka kwenye mifuko ya kampuni za Tanzania

Hii ni sukari iliyomwangwa chini kabla ya kuwekwa kwenye viroba
Siku ya tarehe 6/4/2016 maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kikosi cha (FAST) wakiwa na maofisa wa Polisi walifanya upekuzi kwa lengo la kutafuta magendo kwenye nyumba ya mfanyabiashara Yusuf Barkat Saleh.

Upekuzi huo ulifanyika baada ya kupata taarifa za kiintelijensia zilizofanyiwa kazi muda mrefu.

Bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi zilikamatwa kama ifuatavyo:
 1. Sukari ya India kilo 50, jumla mifuko 762
 2. Sukari ya nje iliyokamatwa kwenye mifuko ya viwanda vya hapa nchini kilo 25, jumla mifuko 135 Mafuta ya kula lita ishirini (20) aina mbalimbali kutoka nje, jumla madumu 49
 3. Betri aina ya Tigger katoni 223 
 4. Hamira katoni 135 
 5. Sabuni za kufulia katoni 48 
Vitu vingine mbalimbali vilivyokamatwa kama ushahidi wa biashara haramu ya magendo ya sukari.
 1. Mashine mbili (2) za kushonea kwenye mifuko ya iliyowekwa sukari inatoka nje ya nchi na kuwekwa kwenye mifuko ya viwanda vya nchini nya sukari vya Kilombero, TPC na Mtibwa Sugar.
 2. Mifuko mitupu mipya ya sukari kilo 25 kutoka India 2000
 3. Mifuko iliyotumika ya kilo 50 mitupu ya sukari 36,000
 4. Mifuko ya sukari iliyotumika ya viwanda vya Tanzania ya kilo 25 kiasi cha 1,150.
 5. Madumu mafuta ya nje mchanganyiko ya kula lita 20 kiasi cha 609 
 6. Madumu matupu ya lita 10 ya nje kiasi cha 310
Madumu yaliyokuwa na mafuta ya kula na ndoo zinazotarajiwa kuwekwa mafuta
Ifuatayo ni habari kwa kina iliyochapishwa kwenye gazeti la MWANANCHI

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imemtia mbaroni mfanyabiashara aliyepiga chenga agizo la Rais John Magufuli la kuzuia uingizaji sukari kutoka nje, badala yake akaamua kuingiza shehena ya bidhaa hiyo kwa njia ya magendo.

Mfanyabiashara huyo, Yusuph Barakati Saleh alikamatwa na TRA akidaiwa kumiliki mifuko 896 ya sukari iliyoingizwa nchini kupitia bandari bubu katika Kijiji cha Njianne, Kilwa mkoani Lindi.

Hatua hiyo imekuja takriban miezi miwili baada ya Rais Magufuli kutangaza kwamba hakuna vibali vitakavyotolewa kuruhusu uingizaji wa sukari, ili kuvilinda viwanda vya ndani.

Sukari hiyo iliyoingizwa nchini kutoka India na Brazil, ilikamatwa na timu ya doria ya TRA (Fast) usiku wa kuamkia Jumatano.

Timu ya Fast na Polisi ilibaini shehena hiyo ikiwa imehifadhiwa katika ghala, sehemu ikiwa imebadilishwa vifungashio na kutumia mifuko yenye nembo za viwanda vya Kilombero, TPC na Mtibwa ili ionekane imezalishwa nchini na kuingizwa sokoni.

Pia ilikuwapo sukari ambayo haikuwa imefungwa kwenye mifuko, bali ilikuwa imerundikwa kwenye turubai ikionekana kulowa maji.

Mwandishi alishuhudia sehemu ya sukari hiyo ikitiririka maji ya rangi ya kahawia, na ilidaiwa kuwa maji hayo yamekuwa yakikusanywa na kuingizwa sokoni kama asali.

Pia katika eneo hilo zilikamatwa bidhaa nyingine ambazo ni katoni 223 za betri za redio aina ya Tiger, katoni 135 za hamira na katoni 48 za sabuni.

Katika ghala jingine ambalo inasadikiwa ndimo shughuli ya kubadilisha vifungashio hufanyika, vilibainika vifaa mbalimbali kama mashine ya kusaga, jenereta, mzani, malighafi za kutengenezea mifuko na mashine za kushonea mifuko hiyo.

Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema bidhaa hizo zilikamatwa na kikosi hicho cha Fast, ambacho hufanya doria maeneo mbalimbali na kukamata bidhaa za magendo kwa kushirikiana na polisi.

“Kazi hii imetokana na juhudi za wananchi wema ambao wametupa taarifa na kikosi chetu cha Fast kwa kushirikiana na polisi wamebaini kwamba vitu hivi viko hapa,” alisema Kayombo. Alisema ghala hilo liko chini ya ulinzi na mzigo wote ambao umekamatwa utataifishwa na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika.

Kayombo alisema pia ilikamatwa mifuko mitupu 2,000 yenye uwezo wa kujaza kilo 25 kila mmoja na mingine 36, 000 ya kilo 50 kila mmoja.

Alisema pia kuna mifuko 1,150 ya viwanda vya Tanzania iliyotumika ya kilo 25 kila mmoja, madumu matupu ya mafuta ya kula 609 ya lita 20 kila moja na mengine 310 ya ujazo wa lita 10 kila moja.

Akizungumzia athari za bidhaa hizo, Kayombo alisema kuwa ni pamoja na madhara ya kiafya kwa watumiajai na kwa uchumi kwa kuwa Serikali inapoteza mapato.

“Hatuwezi kuwa na uhakika wa ubora wa sukari hii maana itakuwa haijapita Shirika la Viwango (TBS), wala Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA),” alisema Kayombo.

Kayombo alisema TRA inakabiliwa na changamoto kubwa ya kupambana na bidhaa za magendo ambazo huingia kupitia bandari 11 bubu zilizomo wilayani humo.

Bandari hizo ni Kilutu, Kiheli, Sueli, Shuka, Mayungiyungi, Milamba, Mapimbi, Limayao, Kisongo, Kimwera na Nchinga.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho alisema kuwa amemfahamu mfanyabiashara huyo na shughuli hizo tangu mwaka 2008 na amekuwa akishusha mizigo hiyo wakati wowote, huku vijana wakijipatia ajira za muda.

“Huyu jamaa alikuwa hachagui muda wa kuleta mizigo, alikuwa akileta muda wowote, usiku na mchana kwa sababu hapakuwa na mtu wa kumghasi,” alisema mkazi huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Alisema mfanyabiashara hiyo amekuwa anawauzia bidhaa hizo wenye maduka na hata wanakijiji wamekuwa wakinunua sukari hiyo.

Mkazi mwingine alisema licha ya kumuona mfanyabaishara huyo akishusha mizigo yake mara kwa mara, alikuwa hajui kama bidhaa hizo ni za magendo.

----------- MWISHO ------------


Nyumba hii ndiyo Ofisi ya Bosi ambayo utumika kuweka bidhaa kabla ya kusambazwa sokoni iliyopo Somanga njia nne eneo la Kikanda Wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi.

sehemu ya kuweka sukari na kupima.

Nyumba inayotumika kuweka sukari

Mkurugenzi wa Elimu kwa walipa kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Richard Kayomboakionesha ndoo zinazotarajiwa kuwekwa mafuta.

Sukari na viroba vya kuweka kwa matayarisho ya kuingizwa sokoni.

Askari wakisimamia zoezi la kuvunja mlango
Mkurugenzi wa Elimu kwa walipa kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, Richard Kayombo akizungumza na waandishi.

Mkurugenzi wa Elimu kwa walipa kodi Richard Kayombo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA akionesha sukari.

Mkurugenzi wa Elimu kwa walipa kodi Richard Kayombo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA
Aina ya mafuta kutoka nje ya nchi tayari kuwekwa kwenye ndoo kwa kupeleka Sokoni

Polisi akilinda viroba vyenye sukari kutoka nje ya nchi.

Nyumba ya mtuhumiwa Yusuf Sareh iliyopo Somanga Njia nne Kikanda.

 
Toggle Footer
TOP