Loading...
Tuesday

CCM kubadili namna ya kuwapata Wajumbe wa Halmashauri Kuu

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinakusudia kubadilisha muundo na mfumo wa kuchagua wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho kwa kuondoa nafasi za wajumbe wa wilaya na kurejesha mfumo wa zamani wa wajumbe wa mikoa.

Pamoja na kubadili mfumo, chama hicho pia kimesisitiza kutekeleza nia ya kuwatimua viongozi na wanachama wake wote wanaodaiwa kukisaliti kwa kuunga mkono wagombea wa vyama vingine wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Hayo yalisemwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliopokuwa akizungumza na viongozi, wanachama na wafuasi wa chama hicho mkoani Mara.

“Hatutawafumbia macho wote waliokisaliti chama katika uchaguzi mkuu uliopita; tutawatimua wote waende kwenye vyama walivyoviunga mkono,” alisema Nape.

Alisema kutokana na usaliti wa wanachama na viongozi hao, uchaguzi mkuu uliopita ulikuwa mgumu kwa chama hicho tawala, licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na wanachama waaminifu kukipatia ushindi dhidi ya wagombea wa vyama vya upinzani.

“Hatutakurupuka katika kuwashughulikia wasaliti wote; tutawashughulikia kwa umakini ili tubaki na viongozi wachache lakini waaminifu kwa chama,” alisema Nape.

Kuhusu wajumbe wa NEC, Nape ambaye pia ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo mpango huo utatekelezwa kabla uongozi wa chama haujakabidhiwa kwa Rais John Magufuli.
 
Toggle Footer
TOP