Loading...
Saturday

FikraPevu: Mawaziri wamekula rushwa katika ardhi?

INAELEZWA kwamba kuna kila dalili za mawaziri wenye dhamana ya kusimamia Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na watendaji wengine kupewa rushwa ili wasitekeleze agizo la kurudisha serikalini mashamba na viwanda vya bidhaa na kilimo vilivyotelekezwa, FikraPevu inaripoti.

Mbali ya mashamba hayo, lakini pia viwanja vilivyopimwa kwa gharama ya mabilioni ya fedha za umma jijini Dar es Salaam na maeneo mengine nchini navyo vimetelekezwa na waliovinunua kwa zaidi ya miaka 10 sasa licha ya serikai mara kadhaa kuahidi kuwanyang’anya wahusika.

Viwanja 20,000 vilipimwa jijini Dar es Salaam katika kipindi cha mwaka 2002/2003 kwa gharama zilizotajwa kufikia Shs. 8.9 bilioni, ambapo serikali ilitarajia kukusanya Shs. 26 bilioni kwa mauzo ya viwanja hivyo.

Kutoendelezwa kwa mashamba na viwanja hivyo kumesababisha migogoro mikubwa kati ya wawekezaji na wananchi ambao wamekuwa wakivamia kwa nia ya kupata maeneo ya kilimo na makazi, hali ambayo katika maeneo mengine imesababisha hata umwagaji wa damu.

Kwa upande mwingine, kutelekezwa kwa viwanda vya bidhaa na kilimo pia kumechangia ongezeko la ukosefu wa ajira kuliko hata viwanda hivyo vilipokuwa mikononi mwa serikali.

Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu umebaini kwamba, kwa miaka mitano sasa mawaziri walioongoza wizara hiyo pamoja na watendaji wao wameshindwa kutekeleza mapendekezo ya Bunge kupitia kamati zake, hususan iliyokuwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), kwamba mashamba na viwanda vilivyouzwa kwa wawekezaji na kutelekezwa virejeshwe mikononi mwa umma.

Kumbukumbu zilizopo zinaonyesha kwamba, mapendekezo hayo ya POAC yalitokana na taarifa ya ufuatiliaji wa mashamba na viwanda vya bidhaa na kilimo iliyofanyiwa kazi na Shirika Hodhi (CHC) katika kuwabaini wahusika waliotelekeza kama walivyokuwa wameagizwa na kamati hiyo.

FikraPevu inatambua kwamba, wakati akihitimisha Bajeti ya Ardhi yam waka 2011/2012, Waziri wa Ardhi wa wakati huo Profesa Anna Tibaijuka, aliliahidi Bunge kwamba, baada ya kikao hicho wizara yake ingekwenda kufanya ukaguzi huru wa nani aliyetelekeza mashamba hayo huku akisisitiza kuwa ‘siku za fungate’ zilikuwa zimekwisha (the honeymoon was over).

Aidha, Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Ardhi, Halima Mdee, katika hotuba yake ya bajaeti kivuli kuhusu wizara hiyo kwa mwaka 2012/2013, alihoji ni kwa nini serikali haikuwa imetoa idadi ya mashamba yaliyokaguliwa na wizara na mahali yalipo na ni hatua gani ambazo zilikuwa zimechukuliwa na serikali dhidi ya wawekezaji husika.

“Mheshimiwa Spika, wakati Kambi ya Upinzani ikisubiri taarifa kutoka kwa Waziri wa Ardhi juu ya ukaguzi huru iliyofanywa na wizara kuweza kuwabaini waliotelekeza mashamba, Kambi ya Upinzani inataka Serikali itoe msimamo juu ya taarifa ya ufuatiliaji wa mashamba na viwanda vya bidhaa na kilimo iliyofanyiwa kazi na CHC, kutokana na maelekezo waliyopewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC),” alisema Mdee.

Aidha, kati ya mashamba 27 makubwa ya mkonge yaliyobinafsishwa, ni mashamba 13 tu yenye jumla ya hekta 71,184 ambayo yalikuwa yameendelezwa kwa kiasi, wakati mashamba 14 yenye ukubwa wa hekta 44,764 yalikuwa hayajaendeleza kabisa ama yalitekelezwa.

Taarifa za uchunguzi zinaeleza kwamba, pamoja na ahadi nyingi walizozitoa wawekezaji hao wakati wananunua mashamba kwamba wangeyaendeleza na kuboresha mara mbili uzalishaji, wengi walitumia hati za mashamba kuchukulia mkopo mikubwa kwenye taasisi za fedha na kwenda kuwekeza katika maeneo mengine huku wakiyatelekeza mashamba hayo.

Wakati wa hotuba yake, Mdee aliishukia familia ya Chavda kwamba ni miongoni mwa wawekezaji waliochukua mashamba makubwa ya umma, lakini wakatumia hati kuchukua mabilioni ya fedha na kutokomea mpaka sasa.

“Ikumbukwe kwamba ni familia hii hii ya Chavda (V.G Chavda na kaka yake P.G. Chavda), waliojitwalia mkopo wa Dola 3.5 milioni mwaka 1993 chini ya DCP (Debt Conversion Program) wakiahidi kufufua mashamba ya mkonge Tanga ndani ya miaka 10, na kupata Dola 42 milioni. Walipopata hayo mapesa, hawakufanya lolote, na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao. Kwa utaratibu huu, lazima tuwachukulie wawekezaji wa aina hii kama ni ‘waporaji’ na hawana tofauti na majambazi yanayoiba benki kwa kutumia nguvu!” alisema.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, familia hiyo ya Chavda kupitia kampuni ya Chavda Group, ilinunua mashamba saba ya mkonge mkoani Tanga mwaka 1998 yenye ukubwa wa jumla ya hekta 25,000 ambayo yote waliyachukulia mkopo na baada ya kupata fedha wakayatekeleza na kuondoka nchini.

Mashamba hayo na ukubwa wake kwenye mabano ni Kikulu Sisal Sstate (hekta 5,900), Kwamgwe Sisal Estate (hekta 3,700), Kwafungo Sisal Estate (hekta 2,310), Bombuera Sisal Estate (hekta 2,370 lipo Korogwe) ambalo kutokana na deni benki ya CRDB ililiuza shamba hilo kwa kampuni ya AMC Arusha Ltd mwaka 2002, na shamba jingine ni Hale Mwakiyumbi Sisal Estate, lenye ukubwa wa hekta 4,309 ambalo, kama lile la Kwafungo, bado linashikiliwa na CRDB.

Wakati shamba la Manza Bay Sisal Estate nalo lilikuwa linashikiliwa na CRDB kabla ya kuliuza kwa kampuni ya Mbegu Technologies mwaka 2001 (ambaye naye amelikodisha kwa Omari Mduduma lakini halijaendelezwa mpaka sasa), shamba la Kwashemshi Sisal Estate (hetka 1,498.5) lilikuwa linashikiliwa na benki ya NBC hadi mwaka 2003 benki hiyo ilipoliuza kwa Mathew Upanga Mnkande ambaye ameliendeleza kwa 35% tu.

Katika awamu ya nne, serikali iliyafutia hatimiliki mashamba matatu ya wawekezaji, ambayo ni Ufyomi Galapo Estate, Utumaini lenye ukubwa wa ekari 4,040 ambalo liko wilayani Mafia na lile la Malonje lililoko wilayani Sumbawanga, ambalo limekuwa na mgogoro mkubwa baina ya wananchi na mwekezaji.

FikraPevu inatambua kwamba, shamba la Kikwetu, mkoani Lindi nalo limefutiwa umiliki baada ya mmiliki wake kampuni ya Amboni Estates Ltd, kushindwa kuliendeleza. Uamuzi huo umechukuliwa Desemba 2016 chini ya serikali ya Rais John Magufuli, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni mwaka 2015.

Mashamba mengine 11 yenye ukubwa wa ekari 7,700 ambayo yalifutiwa umiliki yapo katika vijiji vya Kasharazi na Rwakalemera wilayani Ngara mkoani Kagera, ambayo hayana hati na yametelekezwa.

Mashamba ambayo yalikuwa yameendelezwa kwa sehemu tu, kwa mujibu wa taarifa ya CHC ni Ndungu Sisal Estate (hekta 1,230. 9) lililouzwa kwa kampuni ya L.M Investiment ya Tanga mwaka 1997 kwa Shs. 278 milioni, Mkumbara Sisal Estate (hekta 1,734) lililouzwa mwaka 1997 kwa M/S D.D Ruhinda & Company LTD kwa Shs. 100 milioni, Magunga Sisal Estate lililopo Korogwe (hekta 6,520) ambalo linamilikiwa kwa ubia na kuendeshwa kwa kilimo cha mkataba kati ya wakulima wadogo wa mkonge na Katani Limited, Ngombezi Sisal Estate lipo Korogwe (hekta 6,480) ambapo hekta 3881 zimegawiwa kwa wakulima, lakini ni hekta 1301.6 tu ndizo zilizopandwa mkonge.

Shamba la Toronto Sisal Estate lenye ukubwa wa hekta 6,023 lilibinafsishwa kwa kampuni ya Highland Estate Limited kwa bei ya Shs. 265.4 milioni mwaka 1998, lakini mpaka Septemba 2011 lilikuwa limeendelezwa kwa asilimia 50 huku mwekezaji akiwa ameweka amana hatimiliki ya shamba na kushindwa kupata mkopo mwingine kutokana na kudaiwa riba, hivyo kushindwa kuliendeleza.

Mengine ni Hale Mruazi Sisal Estate (hekta 4,180) lakini hekta 1,136 tu ndizo zilizopandwa mkonge, Ubena Sisal Estate (hekta 4,227) lipo Pwani ambalo liliuzwa kwa Highlands Estates Ltd mwaka 2007 kwa Shs. 278 milioni sasa limeendelezwa kwa 12% tu, Kingolwira/Pangawe Sisal Estate, Morogoro (hekta 3,703) aliuziwa Highland Estates Limited kwa Shs. 210.2 milioni kupitia PSRC mwaka 2007 limeendelezwa kwa 22%, Msowero Sisal Estate, Kilosa (hekta 5,200) ambalo liliuzwa na Mamlaka ya Mkonge Tanzania kwa Kampuni ya Noble Azania Agricultural Enterprises mwaka 1993, limepandwa mkonge katika hekta 900 tu sawa na asilimia 17, wakati hekta 200 kwa miaka kadhaa zilikuwa zikipandwa alizeti na mtama.

Mashamba mengine ni Rudewa Sisal Estate, Kilosa (hekta 6,351) lililouzwa kwa kampuni ya Farm Land mwaka 1992 ambayo nayo ikaliuza tena kwa kampuni ya China State Farms Agribusiness (Group) Corporation Tanzania Limited (CSFACOT) kwa Dola za Marekani 1.2 milioni mwaka 2000, na Kimamba Fibre Estate, Kilosa (hekta 5,743) lililouzwa kwa kampuni ya ANCO Ltd mwaka 1998 kabla ya kampuni hiyo kuuza hekta 3,043 kwa kampuni ya Sino na kubakiwa na hekta 2,700.

Aidha, mashamba ambayo hayajaendelezwa kabisa ni Kibaranga Sisal Estate (hekta 6,900) ambalo liliuzwa kwa Kampuni ya Katani Ltd na iliposhindwa kuendeleza serikali ililiweka chini ya PSRC na Bodi ya Mkonge, Allidina Sisal Estate (hekta 2,300) liliuzwa kwa Noble Azania Agriculture Enterprises mwaka 1993 lakini tangu hapo halijawahi kuendelezwa, Msowero (Godes) Farm (hekta 5,000) lilikuwa linasimamiwa na Wizara ya Kilimo chini ya Tanzania Livestock Research Organization (TALIRO) ambapo mwaka 1993 Serikali ilipanga kujenga chuo cha mifugo, lakini mpaka sasa mpango huo haujakamilika, hivyo shamba linadaiwa kutokuwa na usimamizi wowote.

Mashamba mengine ni, Rutindi Sisal Estate (hekta 1,087) linalomilikiwa na Noble Azania Agricultural Enterprises, Magole Sisal Estate (hekta 1,149) bado la serikali na lipo chini ya Mamlaka ya Mkonge Tanzania, lakini lipo katika hali mbaya, Mauze Sisal Estate (hekta 2,842.5) ambalo lilikuwa na deni la Shs. 1.36 milioni kutoka Benki ya NBC ambayo iliamua kuishikilia hatimiliki na kuliweka chini ya ufilisi wa LART kutokana na kuongezeka kwa deni mpaka Shs. 10 milioni, lakini kwa sasa tayari kuna vijiji vya Kilangali na Mabwembele vilivyoanzishwa na vimesajiliwa ndani ya shamba na halmashauri za vijiji hivyo zinakodisha maeneo katika shamba hilo kwa wanavijiji na watu kutoka nje ya vijiji.

Taarifa hiyo ya CHC inaendelea kutaja mashamba mengine kuwa Myombo (hekta 1,843) na Kilosa (hekta 2,024) yaliyobinafsishwa kwa kampuni ya Katani mwaka 1998 ambayo iliyakodisha kwa kampuni ya Agro-Focus Ltd ambayo nayo ilishindwa kuyaendeleza.

Inaelezwa kwamba, mwaka 2005 Baraza la Mawaziri liliagiza mashamba hayo yatafutiwe mwekezaji mwenye uwezo kwani kampuni ya Agro- Focus Ltd ilikuwa imeshindwa kuyaendeleza, lakini kinyume na maagizo hayo, mwaka 2009 Bodi ya Mkonge iliyauza mashamba hayo kwa kampuni hiyo hiyo ya Agro-Focus ambayo mpaka sasa haijawekeza chochote huku eneo kubwa likiwa pori na lililosalia linakodishwa kwa wananchi kwa ajili ya kulima mahindi.

Mashamba ya Madoto Sisal Estate (hekta 3,200) na Kivungu Sisal Estate (hekta 2,200) yalinunuliwa na kampuni ya Sumagro Ltd mwaka 1998, lakini ikayauza kwa East African Breweries mwaka 2009 na haya mpaka sasa.

Kufuatia taarifa hiyo, kambi ya upinzani iliitaka Serikali kuyarejesha bure bila fidia mashamba yote ambayo wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza, na kwamba wale ambao walikuwa wameyaendeleza kidogo, basi warejeshe sehemu ya mashamba waliyoshindwa kuendeleza ili wapewe wananchi wenye uhitaji.

Kuhusu mashamba ambayo tayari yana wakulima wadogo wadogo wanaoendesha shughuli zao za kilimo, wapinzani waliishauri Serikali kupanga utaratibu wa kuwamilikisha wananchi maeneo husika ili kuondokana na dhana ya ‘uvamizi’ au kukodishwa ardhi kwa ajili ya kilimo na kushauri zoezi hilo lifanywe kwa uwazi ili kuepuka udanganyifu uliotokea katika maeneo mengine ya nchi ambako vigogo na watu wenye nafasi zao walijitwalia ardhi wakijifanya na wao ni sehemu ya wanakijiji.

Aidha, katika kuthibitisha mashaka ya wananchi kwamba, huenda mawaziri chini ya wizara hiyo pamoja na watendaji wengine wa serikali wamekuwa wakipewa rushwa ili kutotekeleza maagizo rasmi, kwa miaka takriban 20 sasa bado maelezo ya kina hayajatolewa kuhusiana na mashamba 83 ya mikoa ya Arusha na Manyara ambayo kwa muda mrefu yamekuwa na migororo baina ya wawekezaji na wananchi.

Taarifa zinaonyesha kwamba, mnamo Juni 17, 1997 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha (kabla haujagawanywa na kuzaliwa Manyara), Daniel ole Njoolay, aliitisha kikao cha watendaji kwa ajili ya kuchambua mapendekezo yaliyotolewa kutoka katika wilaya za mkoa huo kuhusiana na mashamba makubwa ambayo yamekuwa na migogoro.

Katika hotuba yake wakati huo, Mhe. Mdee alitaja idadi ya mashamba kwa kila wilaya kuwa ni Arumeru (mashamba 18), Ngorongoro (10), Babati (11), Simanjiro (2), Karatu 96), na Monduli 36, lakini pamoja na mapendekezo yaliyotolewa, hakuna hatua zilizochukuliwa.

Ikaelezwa pia mwaka mwaka 1999, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, kupitia barua yenye kumb. Na. RC/AR/ CL 2/3 Vol IV/19 ilimwandikia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Arumeru ikimtaarifu juu ya mashamba 11 ambayo yalipata kibali cha Rais kufuta miliki, taarifa ambayo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ilipata kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi kwa barua yenye kumbukumbu namba CL/46/VOL III ya tarehe 1 Juni 1999.

Mashamba hayo ni Namba 78 na 79 – NAIC Usa River, Namba 90 na 91- Madiira Coffee Ltd, Namba 98/2/1 – Duluti New – Duluti Lodge, Namba 218/2 – Maua Limited, Oljoro – Salama Estate, Unit 15 Oljoro – Iman Estate, Karangai Sugar Estate (Tanzania Plantation), Shamba Namba 3 – Milimani Pharmacy, Nduruma – Lucy Estate, Nduruma – Umoja Sisal Estate, na Dolly – Dolly Estate – Flycatchers, ambalo liligeuzwa uwanja wa gofu na shamba la wanyama kinyume na maagizo ya Rais.

Upimaji wa viwanja Dar es Salaam

Mkakati wa serikali wa kuendeleza maeneo yaliyomo pembezoni mwa Jiji la Dar es Salaam ambao ulileta malalamiko makubwa kwa wananchi wa maeneo hayo kwa kuwapunja fidia umeonekana kukwama licha ya kuacha msiba kwa wananchi huku maofisa wachache wa ardhi wakijinufaisha na miradi ya upimaji wa viwanja.

Fidia iliyolipwa kwa wananchi ilikuwa kidogo kuliko hata bei ambayo serikali iliweka katika uuzaji wa viwanja hivyo, mfano dhahidi ukiwa eneo la Luguruni wilayani Kinondoni (sasa Wilaya ya Ubungo) ambapo fidia iliyolipwa kwa meta moja ya mraba ilikuwa ni Shs. 1,977, lakini ardhi hiyo hiyo iliuzwa kwa Shs. 30,000 kwa meta moja ya mraba bila maendelezo yoyote, hivyo kuzalisha faida ya asilimia 1,500 kitendo ambacho kilitajwa kuwa ni wizi na unyonyaji mkubwa.

Serikali katika mwaka wa fedha 2002/2003 ilibuni mradi wa upimaji wa viwanja 20,000 jijini Dar es Salaam uliotakiwa kutekelezwa na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na halmashauri zake, ambapo gharama za upimaji zinlifikia Shs. 8.9 bilioni zikiwa ni sehemu ya Shs. 27 bilioni zilizotengwa kwa ajii ya kuendeleza mradi huo nchini.

Inaelezwa kwamba viwanja vilivyopimwa kati ya mwaka 1999 hadi 2006 vilikuwa jumla 45,000.

Taarifa kutoka Wizara ya Ardhi inasema kwamba, mwaka 2005 vilipimwa viwanja 2,740 na kwamba hadi kufikia Desemba 2013 kulikuwa na viwanja 36,289 katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Lengo la mradi huo lilikuwa kukusanya shilingi bilioni 26, fedha ambazo zilikuwa zipatikane kutokana na mauzo ya viwanja vilivyopimwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo katika wilaya ya Kinondoni viko katika maeneo ya Mivumoni, Mbweni kuelekea Mto Mpiji, Mbweni JKT, Bunju, Kibamba, Luguruni, Kwembe Kati na Mabwepande ambako ulionekana kukwama awali, wakati Wilaya ya Ilala ni katika maeneo ya Buyuni, na Mwanagati.

Viwanja vya wilaya ya Temeke vimepimwa katika maeneo ya Kigamboni, Tuangoma, Kibada, Kisota, Mtoni Kijichi, Mwongozo na Gezaulole ambavyo pamoja na vya wilaya nyingine baadhi vimemilikishwa kwa wananchi ambao wameanza kuviendeleza.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya wizara hiyo vinasema, hadi mwaka 2014 katika mradi huo bado kuna viwanja 7,552 ambavyo havijagawiwa kwa watu, kati yake 6,183 viko wilayani Ilala, Kinondoni (685) na Temeke (684).

Inaelezwa pia kwamba, vigogo wengi wa serikali na idara zake walitumia mradi huo kujimilikisha viwanja, ambapo wilayani Ilala ilielezwa kwamba kigogo mmoja alijimilikisha viwanja zaidi ya 10 huku akitumia majina ya vigogo wa serikali, ambavyo baadaye alivilangua kwa bei ya kati ya Shs. 3.5 milioni hadi Shs. 6.5 milioni.

Inaelezwa kwamba vingi kati ya viwanja vilivyonunuliwa vimetelekezwa na wenyewe jijini humo, vikiwemo katika maeneo yaliyo na makazi ya kisasa, hususan Mbezi, Mbweni JKT, Mbweni Mpiji pamoja na Bunju.

Taarifa zinasema kwamba, licha ya maagizo mbalimbali ya serikali kuwataka wamiliki waviendeleze viwanja hivyo vinginevyo watawanyang’anya, lakini wamekaidi na kuvitelekeza viwanja hivyo, hali inayoleta mashaka kwamba huenda watendaji wamepokea rushwa ili wasitekeleze maagizo hayo.

Baadhi ya wananchi wanaeleza kwamba, huenda wamiliki hao wameamua kuviacha viwanja hivyo vipande thamani ili waviuze kwa bei kubwa zaidi.

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP