Loading...
Tuesday

HAPA KAZI TU: Hospitali zilisaidie taifa kuokoa muda wa kufanya kazi

Leo nimeamka asubuhi nikiwa na ratiba ya kumuona daktari wa meno (dentist) kabla ya kwenda kazini ili anisaidie kuziba matundu kwenye meno yanayoninyima raha na utamu wa kula nyama ya mbuzi. Kupata huduma hii pia kutanipunguzia matumizi makubwa ya vijiti (toothpicks) tunavyoagiza toka Uchina kwani kwa muda mrefu sasa hata nikinywa uji nalazimika kuchokonoa meno. Niliingia mtandaoni na kutafuta mawasiliano ya moja ya hospital maarufu hapa Dar es Salaam na bila ajizi nilipiga simu kuomba miadi (appointment) ya kumuona dentist. Aliyepokea simu aliniambia sina haja ya kuweka miadi bali niende tu hospital na nitamuona daktari moja kwa moja. Nimefika hospital saa tatu kama na dakika 20 hivi na nikaambiwa kwa kawaida daktari hufika saa tatu hivyo atakua njiani na kwa kuwa nilikua ni mtu wa saba kwenye orodha ya wanaomsubiri, nalazimika kusubiri. Nimengoja masaa zaidi ya matatu sasa na sina hakika ya muda nitakaomuona daktari kwani ndio kwanza anahudumia walionitangulia nami nikaamua niandike makala niliyowaza kuiandika tangu wiki jana.
Wiki iliyopita nilihitaji kumwona daktari ambaye amekua akiwahudumia watoto wangu na nikajulishwa huwa anapatikana kwa masaa kadhaa katika moja ya hospital kubwa hapa Dar es Salaam. Nilitaka uchunguzi wa afya ya ya mtoto hivyo nilipopata simu ya hospital hiyo nikapiga ili kuomba miadi. Nilipiga ile namba (ya TTCL) kwa siku mbili bila kupokelewa na kesho yake nikaamua kwenda hospital baada ya kupata uhakika wa muda ambao daktari huyo anapatikana. Nilifika hospital kabla ya saa kumi na nusu kwani niliambiwa hutoa huduma kuanzia saa 11 jioni na nikapewa namba 11 kwenye orodha ya waliokua wanamsubiri. Pamoja na kuwahi kote huko nilisubiri hadi saa tatu usiku na ndipo nilipomuana daktari. Kwa kuwa sikua na tatizo la dharura haikumchukua daktari zaidi ya dakika 10 kunipa huduma niliyohitaji. Hivyo nilitumia zaidi ya masaa manne kusubiri huduma ya dakika kumi.
http://gdb.voanews.com/C5780C1E-88E8-4FD0-8B0E-650979C1A539_cx0_cy11_cw0_mw1024_s_n_r1.jpg
http://www.health-e.org.za/wp-content/uploads/2014/01/clinic.jpg


Nikiwa pale hospitali niliumizwa sana na jinsi watoto walivyokua wanahangaika, kulia na kusumbuliwa na kiu na njaa (pamoja na wa kwangu). Kwa bahati mbaya, maeneo yetu ya utoaji wa huduma za jamii kama hospital, hayafikiriwi kabisa mahali pa watoto kucheza wakati wanasubiri wazazi wao au wao wenyewe kusubiri huduma. Matokeo yake, walikua wanacheza kila mahali pale hospital jambo ambali sio salama na ni hatari kwa afya zako kwani wanaweza kubeba magonjwa ambayo hawakuja nayo.
Watoto wengi waliletwa na wazazi wote wawili hivyo idadi ya watu wazima waliomsumbiri walikua wengi. Kwa mtazamo wa harakaharaka, wengi wa wazazi hawa ni wafanyakazi au wafanya biashara wa kiwango cha kati. Wengi walionekana wamepitia pale hospital wakitokea makazini kwani walikua na mabegi ya kazini na wengine wamevalia kiofisi. Nilipowatazama wakihangaika pale bila kujua muda wa kupata huduma, ilinisumbua sana. Kama ilivyokua kwa wazazi wengine nilicheza na mtoto wangu hadi akachoka nami nikaishiwa na ujuzi huku sote tukisumbuliwa na njaa. Nilijiuliza iwapo kupitia huduma ya daktari mmoja watu wengi hivi wanapoteza masaa mengi ya kazi, je ni kwa kiasi gani nchi inapoteza nguvu kazi bila sababu kwa kuwa huu ndio utaratibu karibu kwenye kila hospital nchini?.
Nchi yetu iko chini ya uongozi wa serikali ambayo sio tu inathamini dhana ya kufanya kazi kama uti wa mgongo wa maendeleo ya mtu binafsi na taifa, bali inasisitiza  umuhim wa kila mtu kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kwa moyo wa uzalendo na utumishi. Watu waliozoea kufanya kazi kwa bidi wanajua umuhim wa muda katika kufanya kazi yenye tija na kufikia malengo. Ndio mana kwenye nchi zilizoendelea, malipo ya kazi/ajira huthaminishwa kwa masaa/muda ambao mtu amefanya kazi na sio kumlipa tu kwa mwezi kwa vile kaajiriwa.
Inasikitisha sana kwamba huduma za afya katika nchi yetu bado zinaendeshwa kienyeji sana na watoa huduma hawajali kabisa muda wa wagonjwa au watu wanaokuja kutafuta huduma katika vituo vya afya. Dhana ya kuthamini muda wa mteja/mgonjwa kama moja ya vigezo vya ubora wa huduma bado haijapewa kipaumbele na matokeo yake taifa linapoteza nguvu kazi kubwa sana kila siku kwa muda ambao watu wanapoteza wanapofuatilia huduma za afya. Sio kila mtu anayekwenda hospital au kituo cha afya ni mgonjwa asiye na uwezo wa kufanya kazi. Wako wanaokwenda kupima tu afya zao au kutafuta kinga ya magonjwa; wako wanakwenda kusindikiza ndugu na jamaa wanaoumwa; wako wanaokwenda kufuatilia hali ya matibabu; na wako wanaokwenda tu kutafuta mazingira mazuri ya meno kutafuna nyama kama ilivyo kwangu leo. Makundi yote niliyoyataja hapa ni watu wanaotakiwa kufanya kazi na hawana sababu ya kupoteza masaa kadhaa au siku nzima wakisubiri huduma mahospitalini. Sio kila huduma ya afya au kila mteja anayetembelea vituo hivi ni mhitaji wa huduma ya dharura na hivyo kulazimka kupata huduma kadiri inavyopatikana.
Vituo vingi vya afya na hospital, hasa za umma/ serikali, bado hazina mifumo ya kieletoniki/kompyuta ya kusaidia menejimenti ya wateja wao (wagonjwa) ikiwa ni pamoja na uwezo wa kuweka na kufuatilia kumbukumbu za miadi (appointments) kwa wanaotaka huduma zisizo za dharura, kufutailia matibabu, au utaalamu wa madktari bingwa. Hata hospital za binafsi zenye mifumo hii wamejikita katika kuboresha rekodi / kumbukumbu za wateja wao, kuboresha mawasiliano na upelekaji wa taarifa kwenye vitengo ndani ya hospital, na kudhibiti upotevu wa mapato. Kwa utafiti wangu usio wa kitaalamu, bado hakuna hospital iliyowekeza mifumo ya kuhakikisha wanaokoa muda wa wateja wao wanapohitaji huduma.
Kulingana na taarifa za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi mwisho wa mwezi wa tatu mwaka huu, Tanzania ina watumiaji wa simu za mikononi takribani milioni 40 (namba/ line za simu zilizosajiliwa na zinazotumika). Tuchukulie kila Mtanzania annamiliki line mbili maana wako wengine wana hadi line tatu na zaidi. Hii inamaanisha watu milioni 20 wanatumia simu za mikononi. Wingi huu wa simu za mikononi, unaonesha kuna uwezekano asilimia kubwa ya wanaotafuta huduma za afya wanaweza kupata mawasiliano ya simu na hivyo uwezo wa kupiga kituo cha afya/hospital na kuweka miadi ya kuonana na daktari au kupata huduma wanaoyoihitaji. Hata kama haitawezekana kwa watanzania wote, basi kwa sehemu kubwa wale walioko mijini wanaweza kupata huduma hii.
Kwa kutumia utaratibu wa kuweka miadi kw anjia ya kupiga simu tunaweza kuokoa sana muda wa wateja/wagonjwa. Pili, itasaidia kuwapa wateja uhuru (flexibility) ya muda ambao ni muafaka zaidi kwao kupata huduma kulingana na majukumu waliyonayo. Tatu itakua msaada hata kwa watoa huduma kwani mara nyingine wanapoteza muda wao wakikaa kusubiri watu wa kuwahudumia wasio na hakika nao wakati muda huo wangeweza kuutumia kwa majukumu mengine. Hivyo basi, nashauri yafuatayo:
  1. Huduma zote zisozo za dharura kwenye hospital ziwekewe utaratibu wa kutolewa kwa miadi. Kila hospital iwe na mtu maalum ambaye atakua mapokezi na kazi yake kubwa ni kupokea simu na kuweka miadi ya watu wanaohitaji huduma. Kila daktari mzoefu anajua kabisa wastani wa muda anaotumia kwa kila aina ya mgonjwa anayemuona. Kwa mfano, dentist anahitaji nusu saa hadi lisaa kumuhudumia mtu asiye na complications (tatizo gumu). Hivyo hospital itawapa wateja miadi ya kumuona kila baada ya dakika 30 au 45 na hivyo kukadiria muda ambao mgonjwa atatakiwa awe amefika hospital. Huenda daktari wa watoto au kina mama akahitaji dakika 20 na hivyo kama ataona wagonjwa 10 kwa siku na kazi anaanza saa tatu asubuhi, yule mgonjwa wa kumi kupiga simu ataambiwa aje saa sita na dakika 20 mchana. Ila kwa utaratibu wa sasa, anayehudumiwa wa kwanza na wa kumi au 20 wote wanakuja saa tatu asubuhi. Wale wasioweza au kutaka kutafuta huduma kwa miadi waende tu kama watakavyo lakini wajue kabisa wale wenye miadi watatibiwa kwanza iwapo walipofika kuna ambao walishapiga simu na kupewa muda. Watapewa kipaumbele tu pale ambapo wana matatizo ya dharura au kuna mtu kachelewa miongoni mwa walioweka miadi


  1. Wizara ya afya, itoe maagizo kwamba, kwa kuanzia, kila hospital iwe na huduma maalumu itakayowawezesha wagonjwa kupiga simu kuulizia upatikanaji wa huduma na muda wa kuipata. Mara nyingine watu wamekua wakifunga safari ndefu na kuacha majukumu nyeti ya kazi kwenda kutafuta huduma. Ila wanapofika kwenye hospital husika wanaambiwa daktari hayuko, huduma haipatikani, kifaa (x-ray, ultrasound, nk) haifanyi kazi, au huduma inatolewa kwa siku maalumu. Taarifa hizi mtu anaweza kuzipata kwa kupiga simu na kuepuka kupoteza muda na fedha kwenda kupewa majibu ya iana hii wanapofika hospitalini.  Niliwahi kukutana na kijana mmoja pale Muhimbili aliyekua anahitaji upasuaji wa uvimbe mkubwa kwenye mdomo wake na akanijulisha kwamba amekua akifuatilia miadi ya kufanyiwa upasuaji kwa mwaka mmoja na kila anapokuja anapigwa kalenda na kuambiwa nafasi haijapatikana. Hakuwa mkazi wa Dar es Salaam hivyo waweza kuelewa jinsi hali hii ilikua mateso kwake.


  1. Watoa huduma za afya waachane na hali ya kuwa miungu watu kwa mantiki kwamba wao ndio wanaamua sio tu hali ya afya za watu wengine, bali ndio wanawapangia na kumua ni kwa mtindo gani watautumia muda wao na kutekeleza majukumu yao. Waone huruma na waumie wanapoona mtu anapoteza masaa na siku nzima kufuatilia huduma au maelezo ya huduma ambayo wangeweza kumrahisishia iwapo wangebadili na kuboresha utaratibu.


Dhana ya “HAPA NI KAZI TU” itakua na nguvu ya utekelezaji na kuleta tija zaidi iwapo pamoja na mambo mengine tutaepuka kupoteza muda wetu wa kufanya kazi na kuwasaidia wengine kutumia muda wao vizuri. Ninashawishika kwamba, kwenye utoaji wa huduma za afya, ndilo eneo linalopoteza muda wa watanzania huenda kuliko maeneo mengine yote. Tuna nafasi ya kupunguza tatizo hilo bila gharama ya ziada kwa kutumia nyenzo tulizonazo tukianzia na matumizi ya simu za mikononi.
Kutokana na maendeleo ya teknolojia ya simu za mikononi hapa nchini, twaweza kufanya mambo mengi kwa simu zetu na tukaokoa sana muda wa kazi. Tunalipa bili mbalimbali, tunareset ving’amuzi vyetu majumbani, tunatizama salio na kuhamisha fedha kwenye account zetu za bank, na mengine mengi. Kwa teknolojia hiihii twaweza kutazama iwapo hospital inatoa huduma Fulani, iwapo daktari anapatikana, kuweka miadi ya kupata huduma na mengine mengi.


Imeandikwa na Mwalimu MM

Waweza kumwandikia kupitia mmmwalimu(at)gmail.com

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP