Loading...
Monday

Hatua zilizoshukuliwa na serikali hadi sasa kuhusu Mbunge aliyepewa mgodi hifadhini

SERIKALI imeingilia kati mpango wa Mbunge wa Meatu, Salum Khamis ‘Mbuzi’ (CCM) wa kutaka kuchimba madini ndani ya pori la hifadhi na Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori katika eneo la Makao (JUHIWAPOMA) wilayani Meatu.

Eneo la Makao linaendeshwa kisheria na Kampuni ya Mwiba Holdings Limited.

Mbunge huyo pamoja na washirika wake, Enock Yakobo na Abdillahi Lessani, walipewa leseni Novemba 18,2014 iliyosainiwa na Ofisa Madini Kanda ya Ziwa, Juma Semanta. Leseni hiyo itadumu kwa miaka saba.

Hata hivyo, Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, imeunda kikosi kazi kuchunguza uhalali wa leseni hiyo ambayo inadaiwa imetolewa kwa ‘mlango wa nyuma’.

Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA kuwa baada ya kukamilika ripoti hiyo ya uchunguzi ikiwamo kubaini watumishi waliohusika kutoa leseni hiyo, suala hilo litakabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kesho mjini Dodoma.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Makao wilayani Meatu juzi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, alitangaza kusimamishwa mpango wa uchumbaji madini katika eneo hilo kuepusha mgogoro wa masilahi katika eneo hilo.

“Tunasimamisha huu mpango wa kuchimba madini. Kinachowagombanisha hapa ni uamuzi ambao ninyi mliufanya huko nyuma. Leo (juzi), mnasema hamna eneo la kuchunga mifugo. Kwa hiyo habari ya madini hapana,” alisema Mtaka.

RC pia alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meatu, Godfrey Machumu, kuhakikisha Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Makao, Isack Magaka, anakamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa Polisi kwa kukwepa kuhudhuria mkutano huo wa kujadili mgogoro uliopo.

Mtaka alitoa agizo hilo baada ya kutaka Magaka ajitokeze kuwaeleza wanakijiji taarifa ya mapato na matumizi ya fedha zinazotolewa na kampuni ya Mwiba, ndipo ilipobainika kwamba hakuwapo mkutanoni hapo.

“Lazima tuhoji matumizi ya fedha za wananchi,” alisema Mtaka.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Makao, Anthony Philip, alikiri mbele ya mkutano huo kuwa kijiji hicho kimekuwa kikipokea Sh milioni 115 , zikiwamo Sh milioni 80 za kodi ya pango kila mwaka kutoka kampuni ya Mwiba yenye mkataba wa kuendesha shughuli za uwindaji wa utalii na upigaji picha katika pori hilo.

Mbali ya fedha hizo, Meneja Uhusiano wa Mwiba Holdings Limited, Clarence Msafiri, alisema kampuni hiyo pia imekuwa ikikipatia kijiji hicho Sh milioni mbili kila mwaka kwa ajili ya kodi ya uwanja wa ndege na fedha nyingine nje ya makubaliano kwa ajili ya kuchangia utekelezaji wa miradi ya jamii kijijini hapo.

“Tunalipa Sh milioni mbili kila mwaka kwa ajili ya uwanja wa ndege na tunatoa fedha nyingine zisizo kwenye makubaliano yetu (Mwiba) na kijiji cha Makao kuchangia maendeleo.

“Mfano hivi sasa tumejipanga kuchangia ununuzi wa madawati kwa ajili ya wanafunzi shuleni kuitikia wito wa Rais John Magufuli,” alisema Msafiri.

Kuhusu mgogoro unaoendelea kati ya Kijiji cha Makao na kampuni ya Mwiba, Mtaka alimtaka mwenyekiti wa kijiji kwa niaba ya wanakijiji kutangaza kusudio la mgogoro na kampuni hiyo ili liwekwe kwenye maandishi na hatimaye Serikali ilitafutie usuluhishi wa sheria.

“Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, tumesikiliza tuhuma dhidi ya Mwiba. Kwa kuwa jambo hili ni la sheria, sheria inamtaka mwenyekiti wa kijiji atangaze kusudio la mgogoro na kampuni ya Mwiba ili liwekwe kwenye maandishi kwa ajili ya kutafutiwa usuluhishi kukiepushia kijiji hiki matatizo,” alisema Mtaka.

Mwenyekiti wa Kijiji, Philip, alipewa nafasi mkutanoni na kusema, “Mimi naomba tu ndugu zangu wananchi kwamba ninatangaza kusudio la mgogoro na kampuni ya Mwiba.”

Mgogoro baina ya pande hizo mbili unadaiwa kuikwamisha kampuni ya Mwiba kukabidhi Sh milioni 356 ilizotenga mwaka huu kwa ajili ya kuchangia gharama za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika vijiji vya Makao, Iramba Ndogo, Mwangudo, Sapa, Mbushi, Jinamo na Mwabagimu vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) katika eneo hilo.

Profesa Maghembe

Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, aliomba Watanzania wawe na subira katika suala hilo kwa vile Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anton Mtaka, analishughulikia kwa uzito na taarifa yake ataiwasilisha serikalini kesho.

“Sheria ya Hifadhi ya Wanyamapori inaeleza wazi kuwa hakuna umiliki katika eneo la juu ya ardhi ambayo ni hifadhi.

“Hata waliotoa leseni ya uchimbaji wa madini kuna shaka ndani yake ila naamini taarifa ya Mkoa wa Simiyu itaeleza kwa kina.

“Hivi sasa tunajua kuna watu kazi yao ni kutaka kukwamisha juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ambaye amedhamiria kuijenga Tanzania ya viwanda.

“Wao wamekuwa na kazi ya kueneza kila aina ya uchafu na uongo kwa wawekezaji ambao wana nia njema, hawa tutawashughulikia tu,” alisema Profesa Maghembe.

MTANZANIA ilipomtafuta Mbunge wa Meatu, Salum Khamis kupata ufafanuzi wa madai hayo dhidi yake, simu yake haikupatikana hadi tunakwenda mtamboni.

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP