Maoni kuhusu kusudio la Rais Magufuli la kima cha juu cha mshahara kuwa mil 15/= tu

Hatua ya Rais John Magufuli kutaka kupunguza mishahara ya watendaji mbalimbali wa taasisi za umma kutoka kiwango cha juu cha Sh. milioni 40 kwa mwezi hadi kufikia Sh. milioni 15 inatajwa kuwa ni pigo jingine kwa baadhi ya vigogo hao ambao hivi sasa wanateseka kwa kuishi maisha wasiyoyazoea ya kubana matumizi kila uchao.

Rais Magufuli mwenyewe alitangaza katikati ya wiki kuwa anapokea Sh. milioni 9.5 kwa mwezi, kiwango ambacho ni chini ya mshahara wa wabunge wa Sh. milioni 11.9 kabla ya makato.

Akiwa mapumzikoni mkoani Geita katikati ya wiki, Rais Magufuli alisema atapunguza mishahara mikubwa wanayolipwa wakuu wa taasisi za umma ili kuendana na dhamira ya serikali yake ya kujielekeza zaidi katika kuinua hali za wananchi na kwa kufanya hivyo, wale waliozoea kuishi kama malaika sasa wajiandae kuishi kama shetani.

Punguzo hilo la mshahara alilokusudia Rais Magufuli, kutoka Sh. milioni 40 hadi Sh. milioni 15, ni sawa na asilimia 62.5. Kwa hesabu za mwaka, ni sawa na kupunguza mshahara wa jumla kutoka Sh. milioni 480 hadi Sh. milioni 180, pungufu ya Sh. milioni 300 ya kiwango cha sasa cha mshahara wa vigogo hao.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa hatua hiyo ya kupunguza mishahara ya wakuu wa taasisi mbalimbali za umma ikitekelezwa, maana yake hali itakuwa ngumu zaidi kwa wahusika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Nipashe, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa nchini walisema hali hiyo itazidi kuonyesha kuwa Rais Magufuli anazidi kuthibitisha kuwa hafurahishwi hata kidogo na namna fedha za umma zinavyotumika kunufaisha watu wachache huku Watanzania wakitaabika kwa kukosa huduma muhimu za umma kama maji, elimu ya uhakika na huduma bora za matibabu hospitalini.

Baadhi yao walidai kuwa hatua hiyo ya kutaka kupunguza mishahara kwa vigogo ili wale waliozoea kuishi kama malaika waonje ladha ya maisha ya kishetani siyo ya kushangaza kwa sababu hadi sasa, tayari Rais Magufuli ameshawapa ‘kibano’ wakuu wengi wa taasisi hizo kwa kuziba mianya mingi iliyokuwa ikitumika kuvuna mamilioni.

“Binafsi sishangazwi na hatua hii ya Rais Magufuli kwa sababu tangu alipoingia madarakani, alishasisitiza kuwa serikali yake itabana matumizi na kuhakikisha kuwa inaongeza mapato na kuelekeza fedha nyingi katika kuboresha huduma zinazowagusa wananchi moja kwa moja,” mmoja wa wachambuzi hao aliiambia Nipashe jana.

Akifafanua, mchambuzi huyo alisema punguzo hilo la mshahara litakuwa ni nyongeza tu ya orodha ya mapigo wanayoendelea kuyapata vigogo kutoka kwa Rais kwa sababu kuna hatua kadhaa zilizochukuliwa kudhibiti mnatumizi ya ovyo ambazo hivi sasa zimewalazimu baadhi ya wakubwa kubadili mwenendo wa maisha yao, ikiwa ni pamoja na kuachana na maisha ya kifahari na anasa ghali.

“Ni kweli kuna baadhi ya wakuu wamekuwa na maisha ghali kutokana na fedha nyingi walizokuwa wakijilipa kwa visingizio mbalimbali,” mchambuzi mwingne alisema kabla ya kuongeza:

"Hivi sasa mianya hiyo imezibwa na hivyo baadhi yao wameanza kutaabika kwa kulazimika kuwa na maisha yenye kuzingatia nidhamu ya fedha.

“Mishahara ikipunguzwa kwa kiwango alichotaja Rais Magufuli, maana yake wengi kati ya wakuu hawa wataumia zaidi. Mshahara ndiyo pato lao la ukakika kwa sasa baada ya kubanwa kila kona.

Aidha, katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa ni kweli, ikiwa hatua ya kupunguza mishahara itachukuliwa sasa, itakuwa ni sawa na kuongeza pigo jingine kubwa la tano kwa vigogo ambao hivi sasa, wengi wao wanataabika kutokana na kutokuwa na rundo la mianya ya kuchota fedha bila jasho kwenye taasisi zao.

Imebaibika kuwa maamuzi mengine aliyochukua Rais Magufuli na ambayo hadi sasa yangali yakiathiri mwenendo wa maisha wa vigogo wengi wa taasisi za umma ni kufutwa kwa safari holela za nje; kuondolewa kwa posho holela za vikao; kufutwa kwa matumizi holela ya fedha kwa ajili ya hafla, semina, kongamano na maadhimisho mbalimbali na pia kufutwa kwa ulaji wa fedha za umma kupitia matengenezo ghali ya vitu kama kalenda, t-shirts na matangazo.

POSHO SAFARI ZA NJE, NDANI

Wakati akiwahutubia wabunge katika uzinduzi rasmi wa Bunge la 11 uliofanyika Novemba 20 mjini Dodoma, Rais Magufuli alisema serikali yake imeamua kudhibiti safari za nje kwa sababu zimekuwa zikiligharimu taifa mabilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumiwa katika maeneo mengine ya maendeleo.

Kwa mfano, Rais Magufuli alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2013/2014 na nusu ya kwanza ya 2014/2015 pekee, taifa lilitumia zaidi ya Sh. bilioni 356.7 kugharimia safari za nje ya nchi, kiasi ambacho kingeweza kujenga barabara za lami za urefu wa km 400.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa uamuzi wa kufutwa safari holela umewaathiri kwa kiasi kikubwa baadhi ya wakuu wa taasisi za umma kutokana na ukweli kuwa walikuwa wakisafiri mara kwa mara na kulipwa mamilioni ya fedha.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliwahi kukaririwa akikiri kuwa ni kweli, wakati wa utawala wa awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete vigogo walikuwa wakisafiri sana na “kupishana angani kama nyumbani kunawaka moto”.

Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa kwa wastani, wapo wakuu wa taasisi za umma waliokuwa hawakosi kusafiri nje ya nchi walau mara moja kwa mwezi na wakiwa huko, walikaa wastani wa siku tano kwa kila safari. Kwa sababu hiyo, jumla ya siku zote za kuwa nje ya nchi kwa mwaka zilikuwa 60.

Januari 15, 2015, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, alikaririwa akisema kuwa wakuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA) walikuwa wakijilipa dola 800 kwa siku kila wanapokuwa nje ya nchi na Sh. 500,000 wanapokuwa katika safari za ndani. Hivyo, kwa wastani, kigogo mmoja wa TPA alikuwa akivuna dola za Marekani 48,000 kwa mwaka kwa safari za nje, ambazo kwa mujibu wa kikokotozi cha kubadili fedha cha mtandao wa Oanda jana, kiasi hicho ni sawa na Sh. milioni 102.83.

Aidha, ikiwa mkuu wa taasisi kama ya Bandari angesafiri ndani ya nchi walau mara moja kwa mwezi na kukaa siku tano kwa kila safari, angetumia pia siku 60 akiwa safarini na hivyo jumla ya malipo yake kwa mwaka kuwa Sh. milioni 30.

Kwa sababu hiyo, wastani wa jumla ya posho za safari kwa mwaka kwa mkuu wa taasisi iliyolipa wakuu wake mishahara kama ya Bandari wakati huo, ni Sh. milioni 132.83.

Kiasi hocho ni nje ya posho nyingine zinazoambatana na safari katika baadhi ya taasisi kama ‘entertainment allowance’ inayofikia hadi Sh. 700,000 kwa siku na ‘communication allowance’ ambayo viwango hutofautiana na baadhi hulipwa hadi Sh. 600,000.

Akizungumzia safari za vigogo wa TPA, Zitto alisema zilitumika Sh. bilioni 10 kwa ajili ya kugharimia safari hizo katika kipindi cha miaka mitatu tu, tena bila hata ya kupata kibali kutoka kwa Msajili wa hazina.

Hata hivyo, tangu Magufuli aingie madarakani, uchotaji fedha holela kupitia safari umedhibitiwa na hivyo kuwakosesha ulaji wakuu wa taasisi za umma za namna kama ya TPA.

POSHO ZA VIKAO

Eneo jingine ambalo Magufuli anaendelea kuwatesa vigogo waliokuwa wakiishi maisha ya kifahari enzi za Rais Kikwete ni uvunaji wa mamilioni ya fedha kupitia vikao, hasa vya ndani.

Chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kuwa katika baadhi ya taasisi, idadi ya vikao hufikia hadi 20 kwa wiki na katika kila kikao, vigogo walikuwa wakilipana posho nono kulingana na nafasi zao.

Kwa mfano, uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa katika taasisi moja maarufu, kiwango cha posho kwa kila kikao kwa mkuu wake ni Sh. 120,000.

“Kutokana na kuwapo kwa posho, karibu kila siku tulikuwa na vikao zaidi ya viwili. Kwa wakuu ndiyo vikao vilizidi kwa sababu hata wakija wageni, akimaliza kuzungumza nao anastahili kulipwa kwa sababu huhesabiwa kuwa kila mazungumzo na wageni pia ni kikao,” chanzo hicho kiliiambia Nipashe kwa sharti la kutoandikwa gazetini.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa vikao hivyo vya kazi vilikuwa vikizidi idadi ya 15 kwa wiki katika taasisi nyingi za umma, lengo kubwa likiwa ni kuhalalisha malipo ya posho kwa kila mmoja.

Hivyo, ikiwa itakadiriwa kuwa kila mkuu wa taasisi alikuwa akihudhuria wastani wa vikao 15 kwa wiki, maana yake makadirio ya wastani wa vikao hivyo kwa mwaka ni 780. Kwa sababu hiyo, wakuu wa taasisi hizi walikuwa wakilipwa walau Sh. milioni 93.6 kwa mwaka kutokana na posho za vikao hivyo.

Agizo la Magufuli la kufuta malipo ya vikao holela kwa serikali yake limefuta ulaji huo kwa wakuu wengi wa taasisi za umma na hivyo kujikuta wakiwa katika wakati mgumu kifedha kulingana na mazoea.

“Kwakweli hali sasa ni mbaya. Fedha zitokanazo na posho za vikao hazipo tena na hivyo kila mtu anaishi kwa kujibana hasa kulinganisha na hali ilivyokuwa kabla ya ujio wa Magufuli,” mmoja wa maafisa waandamizi wa taasisi moja aliiambia Nipashe.

Kabla ya Magufuli kufuta matumizi ya aina hiyo, kamati ya PAC chini ya Zitto iliwahi kuanika matumizi holela ya fedha za umma kupitia vikao na mikutano baada ya kupitia hesabu za TPA za mwaka wa fedha 2012/2013 na kubaini kuwa zimetumika Sh. bilioni 9.6 kwa ajili ya kugharimia vikao na mikutano yao ya ndani.

HAFLA, SEMINA, MAKONGAMANO 

Kukosekana kwa posho zitokanazo na shughuli kama za hafla, semina, makongamano maadhimisho ya siku mbalimbali duniani ni eneo jingine ambalo linalowaza njaa vigogo mbalimbali wa taasisi na mashirika ya umma. Kwa mujibu wa Rais Magufuli, ni marufuku kutumiwa fedha kiholela kwa shughuli za aina hiyo ambazo hapo kabla zilitumika kuwaingizia ulaji wakubwa kutokana na posho na pia kuongeza gharama za maandalizi ya shughuli hizo ambazo zilikuwa zikiligharimu taifa mabilioni ya fedha.

Mfano mmojawapo wa fedha nyingi zilizokuwa zikitumika kwa shughuli kama hizo na baadhi ya vigogo kunufaika nazo ni maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyokuwa yafanyike kitaifa mkoani Singida na kutarajiwa kutumia zaidi ya Sh. milioni 200.

Rais Magufuli alipiga marufuku matumizi ya fedha hizo kwa ajili ya maadhimisho hayo na kuamuru zipelekwe kusaidia huduma kwa waathirika wa ugonjwa huo.

Aidha, Rais Magufuli aliamuru Sh. milioni 235 zilizochangwa kwa ajili ya hafla ya uzinduzi wa Bunge la 11 mwishoni mwa mwaka jana mjini Dodoma kwenda kununulia vitanda kwa wagonjwa waliokuwa wakilala sakafuni kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili. Sh. milioni 15 tu ndiyo zilinunua vinywaji na chakula kwenye sherehe hiyo.

Chanzo kimeiambia Nipashe kuwa baadhi ya wakuu wa taasisi wamepata pigo kubwa kiuchumi kwa sababu walikuwa wakinufaika kwa njia mbalimbali zikiwamo za posho na kuongeza ‘cha juu’ kupitia gharama za maandalizi ya shughuli hizo.

VIBANO VINGINE

Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amepiga marufuku pia matumizi holela ya fedha za umma kwa shughuli zisizokuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi ikiwamo maandalizi holela ya machapisho kama ya kalenda, vitabu vya kumbukumbu za kila siku maarufu kama ‘diary’, t-shirts na pia kadi za salamu za sikukuu.

Inadaiwa kuwa vitu hivyo vilikuwa vikiwapa ‘ulaji’ mnono wakuu wa taasisi nyingi za umma lakini tangu aingie Magufuli, yote hayo yamebaki kuwa historia.

“Mambo yanazidi kuwa magumu. Mianya mingi iliyokuwa ikiwaingizia watu fedha za burebure serikalini inaendelea kuzibwa na matokeo yake watu wanalazimika kuacha ufahari na kuishi kutokana na vipato vyao halali,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe.

“Kwa mfano, hivi sasa hakuna tena kusafiri kwenda kwenye vikao vya kazi Bagamoyo, Ngurdoto kule Arusha au kokote kule ikiwa washiriki ni kutoka mikoa isiyozidi nane.

"Ni kwa sababu maelekezo yanasema vikao aina hiyo vinapaswa kuendeshwa kupitia teknolijia ya video (video conference)… hakuna pia malipo ya ziada kwa ajili ya kukodisha kumbi za mikutano kwa sababu maelekezo yanataka mikutano yote ifanyike kwenye kumbi za taasisi husika.

"Nakwambia hali ni mbaya na mabosi wanahangaikia zaidi kwa sababu hawakuzoea kuishi kwa namna wanavyoishi sasa,” chanzo kilioongeza.