Loading...
Wednesday

Marais Magufuli, Kagame wazindua rasmi daraja la Rusumo na OSBP

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa RwandaMhe. Paul Kagame wakitembea kwa pamoja mara baada ya kuzindua rasmi daraja la kimataifa la Rusumo na Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Rusumo.
Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, ameingia nchini Rwanda kwa usafiri wa magari akitokea nyumbani kwake Lubambangwe, katika kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita ambako alikuwa mapumziko tangu tarehe 29 Machi, 2016.

Katika eneo la Rusumo, Rais Magufuli na Rais Kagame kwanza wamefungua majengo ya Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani kilichopo upande wa Tanzania,kisha wakafungua daraja la mto Rusumo, na baadaye wakafungua Majengo ya Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani kilichopo upande wa Rwanda.

Mradi huu wa ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha utoaji wa Huduma za Mpakani cha Rusumo, umehusisha ujenzi wa majengo ya mamlaka ya Mapato katika pande zote mbili na daraja lenye urefu wa mita 80 na upana wa mita 9.5, na umegharimu shilingi Bilioni 61.4 zilizotolewa kwa ufadhili wa serikali ya Japan kupitia shirika lake la JICA.

Akizungumza katika sherehe ya ufunguzi wa mradi huo Rais Magufuli ameishukuru Japan kwa kutoa fedha za kuwezesha utekelezaji wa mradi huo na ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Rwanda kupitisha mizigo yao Tanzania kupitia mpaka huo, pamoja na kuitumia bandari ya Dar es salaam.

Dkt. Magufuli amewasihi wananchi wa Rwanda na wanajumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla, kushirikiana kibiashara kwa kutumia fursa zilizopo huku akibainisha kuwa Tanzania imeanza juhudi za kuimarisha miundombinu yake ya barabara na kujenga reli ya kati, ambayo tayari washirika 13 wameonesha nia ya kufanikisha ujenzi huo.

Aidha, Rais Magufuli amewaonya maafisa forodha na vituo vya ukaguzi kuacha mara moja tabia ya ucheleweshaji wa upitishaji wa mizigo, na amesema serikali imeshaamua kuwa barabara ya Rusumo hadi Dar es salaam itakuwa na vituo vitatu ambavyo ni Rusahunga, Singida na Vigwaza ili magari yatumie muda wa siku 3 badala ya kutumia siku zaidi ya 10.

Kwa upande wake Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye ameongozana na mkewe Mama Janeth Kagame, pamoja na kuishukuru Japan kwa kufadhili mradi huo amesema Tanzania na Rwanda zina kila sababu ya kushirikiana kiuchumi na ameongeza kuwa ni matumaini yake kujengwa kituo hicho kutaongeza biashara na idadi ya watu wanaovuka daraja kutoka 2,000 wa sasa hadi watu zaidi ya 15,000 kwa siku.

Akiwa Rwanda Rais, Magufuli amefanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Paul Kagame na hapo Kesho, Rais Magufuli atashiriki maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 22 ya mauaji wa Kimbari yaliyotokea mwaka 1994 ambapo watu takribani milioni 1,000,000 waliuawa.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano,
IKULU
Kigali

06 April, 2016.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa RwandaMhe. Paul Kagame wakikata utepe kwa pamoja kuashiria uzinduzi rasmi wa daraja la kimataifa la Rusumo, mchana huu.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi leo tarehe 06 April, 2016 kwa kutembelea nchi jirani ya Rwanda, ambapo yeye na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame wamefungua Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani (One Stop Border Post) na Daraja la Kimataifa la Mto Rusumo katika Mpaka wa Tanzania na Rwanda.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wakifurahia mara baada ya kuzindua rasmi daraja hilo la kimataifa la Rusumo na OSBP Rusumo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame kwa pamoja leo Aprili 6, 2016 wamezindua daraja la kimataifa la Rusumo na Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Rusumo.

Zoezi hili la uzinduzi pia limehudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu serkalini kutoka Nchi zote mbili, Mabalozi, na Viongozi wa Taasisi mbambali za Kitaifa na Kimataifa.

Daraja la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha huduma kwa Pamoja Mpakani ni kiungo muhimu katika Ukanda wa Kati(Central Corridor), mtandao huu wa barabara unaunganisha barabara kuu ya Dar es Salaam - Chalinze – Morogoro – Dodoma – Singida – Nzega – Tinde – Isaka – Lusahanga na Rusumo kupitia Kibingo Nakayonza hadi Kigali Nchini Rwanda. Mtandao huu utakuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi kati ya Nchi hizi mbili za Tanzania na Rwanda.

Akizungumza katika sherehe za uzinduzi wa mradi huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Magufuli aliwahimiza Wananchi wa Nchi zote mbili kutumia fursa ya uwepo wa Daraja la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha huduma kwa Pamoja Mpakani Rusumo kujiletea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Jumuiya yetu Afrika Mashariki kwa ujumla.

Aidha Mhe. Rais amewaasa Wananchi kulinda miundombinu kwani kuna baadhi ya wananchi wanadiriki kuiba alama za barabarani, vyuma vya madaraja na kuharibu taa za barabarani kwa baadhi ya miji, ameagiza vyombo vya usalama kuhakikisha wanalinda miundombinu hiyo na kuwachukulia hatua za kisheria kwa wale watakaodiriki kufanya uharibifu huo.

Aidha licha ya mradi huo kurahisha usafairishaji wa bidhaa na watu Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa alieleza faida kadhaa za mradi huo zikiwemo; kuwa ni kiungo muhimu cha kuiunganisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya nyingine za Kikanda kama vile SADC na COMESA, kurahisisha mawasiliano ya kijamii baina ya watu wa Tanzania na Rwanda, pamoja na kuimarisha uhusiano na kukuza biashara kati ya Nchi hizi mbili za Tanzania na Rwanda na Nchi nyingine za Maziwa Makuu.

Ujenzi wa Daraja la Kimataifa la Rusumo na Kituo cha huduma Pamoja Mpakani Rusumo ni moja ya miradi inayotekelezwa kwa msaada kutoka Serikali ya Japan kwa Nchi za Tanzania na Rwanda kupitia shirika lake la maendeleo la JICA.

Mradi huu kwa upande wa Tanzania umegharimu takribani kiasi cha TShs. 33,206,508,072.07 hadi kukamilika.

Miradi mingine inayotekelezwa kwa kushirikiana na Serikali ya Japan kupitia JICA ni pamoja na ujenzi wa Barabara ya Arusha – Namanga, Iringa – Dodoma, Namtumbo – Kilimasera – Matemanga – Tunduru pamoja na barabara ya Masasi - Mangaka.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wakikata utepe kwa pamoja kuashiria uzinduzi rasmi wa daraja la kimataifa la Rusumo na Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Rusumo. Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu serkalini kutoka Nchi zote mbili, Mabalozi, na Viongozi wa Taasisi mbambali za Kitaifa na Kimataifa.


Muonekano wa sehemu ya Daraja hilo la Rusumo

Jiwe la msingi lililowekwa baada ya uzinduzi wa daraja hilo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wakipita kwenye Daraja hilo la Rusumo mara baada ya uzinduzi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame wakikata utepe kwa pamoja kuashiria uzinduzi Kituo cha Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Rusumo. Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu serkalini kutoka Nchi zote mbili, Mabalozi, na Viongozi wa Taasisi mbambali za Kitaifa na Kimataifa.

Picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi wa huo

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP