Mbunge wa Kilombero asimulia mateso, manyanyaso na misukosuko anayopata atakapo kutimiza wajibu wake

Mbunge wa jimbo la Kilombero Peter Lijualikali akitolewa kinguvu na askari wa jeshi la polisi kufuatia amri ya Mwenyekiti wa kikao cha halmashauri ya wilaya ya Kilombero kumtaka kuondokana kutokana na kutokuwa mjumbe halali wa kikao cha baraza la madiwani halmashauri hiyo kilichofanyika ukumbi wa mikutano wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.Picha na Juma Mtanda
Juma Mtanda, Morogoro

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndio chama pekee cha upinzani kilichoibuka kidedea na kung’ara katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015 katika mkoa wa Morogoro baada ya kushinda majimbo mawili ya ubunge ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa vyama vingi vya upinzani nchini.

Majimbo ya Mlimba na Kilombero kwa sasa ndio majimbo yanayongozwa na upinzani kupitia CHADEMA huku idadi kubwa ya kata zikinyakuliwa na madiwani wa upinzani katika kuwakilisha vikao vya halmashauri ya wilaya ya Kilombero.

Katika jimbo la Mlimba linaongozwa na mbunge, Suzan Kiwanga wakati jimbo la Kilombero linaongozwa na mbunge machachali, Peter Ambrosi Lijualikali (31).

Kati ya majimbo hayo mawili, jimbo la Kilombero ndilo jimbo linaloonekana kukumbwa na utata na figisufigisu kati ya ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Kilombero na mbunge wa jimbo hilo, Peter Lijualikali katika kuhudhuria vikao vya baraza la madiwani katika halmashauri hiyo.

Mwananchi imefanya mahojiano maalumu na mbunge wa jimbo la Kilombero, Peter Lijualikali katika mji wa Ifakara ikitaka kujua namna alivyojiingiza katika siasa, historia ya maisha yake na nini kiini cha figisufigisu zinazodaiwa kuelekezwa kwake kwa kuzuiliwa kudhuria vikao halali vya halmashauri ya wilaya ya Kilombero ilihali yeye ni mbunge wa jimbo la Kilombero?.

Lijualikali anaanza kueleza kuwa chanzo cha yeye kupata misukosuko na askari wa jeshi la polisi kukamatwa mara kwa mara na kuswekwa rumande katika kituo kikuu cha polisi Ifaraka na kukaa katika gereza la Idete siku saba kunatokana na msimamo wake wa kusimamia haki katika jamii inayomzunguka na ndani ya chama chake cha CHADEMA.

“Ukiangalia kwa undani nakamatwa mara nyingi na askari na kulala rumande chanzo cha yote ni msimamo wangu wa kusimamia haki ndani ya jamii ninayoongoza na katika chama changu kwa sabau sipendi haki ipindishwe”.anasema Lijualikali.

Lijualikali anaeleza kuwa kabla ya yeye kushinda ubunge wa jimbo la Kilombero katika uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka 2015 pia ameshinda kiti cha udiwani kata ya Ifakara na imedhihirisha kuwa ni kiongozi anayependwa kutokana na kutetea maslahi ya walio wengi wakati akiwa diwani.

Mwaka 2013 aligombea udiwani kata ya Ifakara katika uchaguzi mdogo na kushinda kiti hicho kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wa kata hiyo na Mwenyekiti wa baraza la halmashauri ya wilaya ya Kilombero marehemu, Ramadhan Kiombile.

Lijualikali anasema kuwa baada ya kuanza ya kuwatumia wananchi katika nafasi ya udiwani alianza kuzuia wananchi wasichangia michango isiyokuwa na tija hasa baada ya kudai kubaini fedha za ujenzi wa shule ya kata zilikuwa zikiliwa na baadhi ya vigogo wa halmashauri ya wilaya Kilombero.

“Kitendo cha kuwazuia wananchi wasichangia michanga ya maendeleo ya ujenzi wa shule ya kata, ushuri wa gunia la mkaa sh3,000 badala ya sh720 na mambo mengine kilikuwa chanzo kikubwa cha kuchukiwa na Mkurugenzi wa halmashauri na watawala wengine na kumjengea uhasama mkubwa”.alisema Lijualikali.

Nina ukaribu na wananchi kwa kutetea maslahi yao na wao wameona mimi ni aina ya kiongozi ninayekuwa kuwaongoza na nimekuwa nikitumia usafiri wa baiskeli kwenda kanisani au matembezi ya kawaida hasa pale pasipolazimu kutumia gari imesaidia kuelezwa changamoto nyingi na wananchi.alisema Lijualikali.

Historia ya maisha yake

Lijualikali anasema kuwa yeye amezaliwa Juni 25 mwaka 1985 katika mji wa Kigoma na kusoma shule ya msingi Kulasini Dar es Salaam kuanzia darasa la kwanza mwaka 1994 na mwaka 2000 alihitimu elimu hiyo.

Mwaka 2001 hadi 2004 alisoma kidato cha kwanza hadi cha nne shule ya sekondari ya Airwing huku kidato cha tano na sita akisoma Tegeta High School mwaka 2005 hadi 2006 jijini Dar es Salaam.

Alijiunga na chuo kikuu cha Tumaini tawi la Dar es Salaam mwaka 2008 hadi mwaka 2011 katika kozi ya Library and Information feience huku akiwa Katibu wa jimbo la Temeke (CHADEMA), Katibu Kata ya Mtoni kwa Aziz Ally Dar Es Salaam.

Kutokana na vyeo hivyo alikuwa anaingia katika vikao vya ushauri wilaya ya Temeke (DCC) na amejifunza mambo mengi ya kiungozi na utawala kupitia.

Baada ya kuhitimu elimu ya chuo kikuu aliajiliwa katika chuo kikuu cha St Francis kama Mkutubi wa maktaba kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2015.

Paciens Ambrose Lijualikali ni baba wa Peter Lijualikali miaka ya 1980 aliajiliwa na jeshi la polisi upande wa uhasibu akiwa raia mjini Kigoma na mwaka 1990 aliajiliwa rasmi kuwa askari wa jeshi la polisi Tanzania baada ya kumaliza kozi.

Mwaka 1992 alihamishwa kutoka Kigoma na kwenda kuwa mwasibu kituo cha polisi uwanja wa ndege Terminal One jijini Dar es Salaam.

“Baba yangu ni mpogolo wa kijiji cha Itete Njiwa wilaya ya Malinyi mkoa wa Morogoro na mama ni muha mkazi wa kijiji cha Kagongo kilichopo Kigoma”.alisema Lijualikali.

Lijualikali anaeleza kuwa ana ndugu wa damu akiwemo Peter, Ambrose, Moses, Deborah na Baraka huku akiwa na mchumba.

Jimbo la Kilombero

Jimbo la Kilombero lina kata 19 kati ya kata hizo tisa zinawajibika katika halmashauri ya Mji Ifaraka huku kata 10 zikiingia halmashauri ya wilaya ya Kilombero na kuungana na kata zinazounda jimbo la Mlimba.

Katika uchaguzu wa serikali ya mitaa mwaka 2014, CHADEMA ilinyakua mitaa 29 huku CCM ikiambulia mitaa minne kati ya mitaa 33 inayounda halmashauri ya Mji wa Ifakara.

Mbunge huyo machachali amehoji kuwa yeye amepigiwa kura ya ubunge katika uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka jana kupitia jimbo la Kilombero lakini leo anazuiliwa kuhudhuria vikao vya baraza la madiwani kutumia nguvu ya dola je ni nani sasa mbunge wa jimbo la Kilombero?

Amesema kuwa hoja inayotolewa ya yeye kulazimishwa kuingia kwenye vikao vya baraza la madiwani la halmashauri wa Mji wa Ifakara eti kwa sababu ni diwani wa kata ya Ifakara haina nguvu na ina mapungufu makubwa.

“Hoja zao wananilazimisha niingie katika baraza la madiwani la halmashauri ya Mji Ifakara kwa sababu nimechaguliwa kuwa diwani kata ya Ifakara lakini bado hawaangalii ukubwa wa watu waliopo katika jimbo la Kilombero lenye kata 19 hapa kuna haja ya Tamisemi kuvirudia vifungu vyao kuangalia wapi wamejikua.”alisema Lijualikali.

Kwa maana hiyo jimbo la Kilombero halina mbunge ?, je halmashauri ya Mji wa Ifakara imetangazwa lini kuwa jimbo mpaka mbunge wa jimbo la Kilombero ahamishiwe huko ?..lakini Tamisemi na Tume ya Taifa ya uchaguzi ikae pamoja na kutoa jibu la kuniruhusu nidhurie vikao vyote.alisema Lijualikali.

Aliongeza kwa kusema kuwa makosa tayari yamefanywa na ili yeye afanye kazi vizuri za katika jimbo la Kilombero bila migongano afanye kazi na halmashauri zote mbili za Mji Ifakara na Kilombero.

“Hebu fikiria hesabu zao wanataka nifanye kazi za ubunge katika halmashauri ya Mji Ifakara wakati Mji Ifakara bado haujatangazwa kuwa jimbo, nisubirie Mji Ifakara itakapo tangazwa kuwa jimbo.

Kukamatwa, kuswekwa rumande na gerezani

Peter Lijualikali anaeleza namna anavyojisikia pindi sakala la kukamatwa na askari wakati akitekeleza majukumu ya kutetea haki iwe ndani ya chama ama wananchi wake kwa jambo analoliona limepindishwa na hapo ndipo panapokuwa chanzo cha yeye kukamatwa kwake.

“Nimekamatwa na askari sio chini ya mara sita na amewahi kukaa gereza la Idete siku saba na kukaa mahabusu katika kutuhumiwa kesi mbalimbali na nimewahi kutumia kifungu cha miezi sita nje nashukuru kifungo hicho nimemaliza na yote sababu ya kutaka kujua ukweli tu”.alisema Lijualikali.

Katika kupata misukosuko ya kukaa rumande na gerezani imemsaidia kama kiongozi kujua mambo mengi.

Suluhisho

Tume ya taifa ya uchaguzi ifanye kazi kwa mujibu wa sheria na kudai vurugu zinazotokea zimetokana na tume kukataa Mji Ifakara kuwa jimbo na vigezo vya majimbo halmashauri mpya ikianzishwa inalazimu tume itangaze jimbo la uchaguzi.

Kutokana na tume kucheelewa kutangaza jimbo, halmashauri ya Kilombero imejikuta ina halmashauri mbili katika jimbo lakini tume inaweza kutangaza jimbo la Ifakara kabla ya mwaka 2020 ili kuepusha vurugu zinazoendelea kujitokeza.

Rais Magufuli aingilie kati

Mbunge huyo amemuomba rais John Pombe Magufuli aingilie kati kutokana na madai anayodai kuonewa na askari wa jeshi la polisi la kumkamata pasipo kufuata sheria za bunge na kumnyanyasa.

Kwa upande wa jeshi la polisi, amemuomba IGP Ernest Mangu, askari wa chini yake ngazi ya mkoa na wilaya kufanya kazi ya uaredi kwani wilaya ya Kilombero amedai hufanya kazi chini ya chama tawala jambo linaloishushia hadhi jeshi hilo lenye heshima kubwa Tanzania.

“Rais Magufuli awaagize waziri wa Tamisemi amalize huu mgogoro na IGP pia wasaidizi wake wanafanya kazi kwa maagizo ya kisiasa na jambo hili linanifanya ninyanyasike kwa Mkurugenzi kwani suala hilo halitaisha kwa yeye atalazimika kuingia katika vikao vya halmashauri ya baraza la madiwani Kilombero bila kujali kitatokea nini.”alisema Lijualikali.

Vikao vya baraza la madiwani ndilo linalopanga kila bajeti za halmashauri kutokana na mapato yake inakuwa kiongozi mkuu asiwepo katika matukio hayo?.

Ashitushwa na matokeo ya uenyekiti, aangua kilio polisi

Mbunge huyo amestushwa na kusikitishwa na matokeo ya nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri baada ya CCM kuchakua kiti hicho.

“CCM ilikuwa na wajumbe 18 na UKAWA wajumbe 19 lakini kutokana na hujuma zilizofanywa na wapinzani wetu wamefanikiwa kumlubuni na kupata ushindi huo baada ya kuadiwa kuingizwa katika moja ya kamati vyeti za kamati ndani ya halmashauri”.alisema Lijualikali.

Lijualikali anaeleza kuwa aliangua kilio kituo cha polisi baada ya kupokea taarifa za CCM kutwaa Uwenyekiti wa halmashauri lakini kumbe siye yeye aliyeangua kilio bali na mbunge wa jimbo la Mlimba Suzan Kiwango huku mbunge wa viti maalumu CHADEMA mkoa wa Morogoro Devotha Minja akishikwa na huzuni kwa tukio hilo.

Kutokana na matokeo hayo, mbunge huyo anaeleza na kudai kuwa ndiyo sababu ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Kilombero, Azimina Mbilinyi ya kuwazuia wabunge, Peter Lijualikali, Devotha Minja, viongozi waandamizi UKAWA na waandishi wa habari kuingia ukumbini.
"Vikao vya baraza la madiwani ni vikao vya wazi, mkurugenzi anawajibika kuwatangazia wananchi siku saba kabla ya kikao cha kuwaalika kusikiliza vikao pamoja na kufunga vipaza sauti ndani na nje imekuwa kuwe na ubaguzi kuna nini?" alisema Lijualikali.

Vyombo vilivyoruhusiwa kuingia katika kikao hicho pamoja na TBC, StarTV na HabariLeo ambavyo vilikuwa katika msafara wa aliyekuwa mkuu wa mkoa Morogoro, Dkt Rajabu Rutengwe. Waandishi wa gazeti la Uhuru na Mzalendo, redio Pambazuko na mwandishi wa ITV aliyeingia kwa mkono wa kushoto.  Vyombo vilivyozuiliwa ni Mwananchi, Nipashe na JamboLeo.