Mkuu wa Wilaya, Kasesela awakamata waliotumia jina lake redioni kuadhimisha siku ya wajinga


WAKATI leo kuanzia majira ya saa alfajiri hadi saa 4 ;00 asubuhi ilikuwa ni siku ya wajinga duniani, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Bw Richard Kasesela amewakamata wanahabari wawili wa kituo kimoja cha Radio Fm mkoani Iringa kwa madai ya kuchukizwa na matumizi mabaya ya jina lake katika kudanganya umma.

" Ahsante sana nimewakamata waandishi hao wawili kwa kosa moja kubwa ...mwandishi mmoja aliingia studio na kujitangaza kuwa yeye ni mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela na kuanza kutoa ahadi za kupeleka msaada wa mahindi Kipera na ahadi nyingine nyingi na hata kunidhalilisha hata mimi hii ni sikukuu ya wajinga ya kutaniana zaidi na ni kosa kutumia chombo cha habari kutania na ukitumia chombo cha habari kutania basi ukimaliza tu kutania bila hata kupumzika unapaswa unapaswa kueleza wasikilizaji kuwa hakuna ukweli wa jambo hilo na ilikuwa ni siku ya wajinga.....wao wametangaza kiutania kudanganya watu hata mimi nimewakamata kiutani hivyo hivyo"

Akizungumza na mtandao huu wa matukiodaima ofisini kwake leo kuhusiana na hatua yake ya kuwakamata wanahabari hao wawili alisema kuwa hazuii chombo cha habari ama mwanahabari au mtu yeyote kusherekea siku ya wajinga japo alisema alichochukizwa na hatua ya chombo hicho cha Radio Fm (jina tunalo) kumchukua mtangazaji mwenzao kujifanya ni mkuu wa wilaya ya kuanza kupotosha wasikilizaji kwa kutumia jina na sauti yake na mbaya zaidi walikuwa wakidanganya mambo ambayo ni ya kweli .

'Siku ya wajinga ipo miaka yote ila kujiita wewe ni fulani ama kiongozi na kutumia jina hilo kudanganya watu huo ni sawa na utapeli na upotoshaji .......kwani hata baadhi ya vitu vya kudanganya ni vile ambavyo haviwezi kuhatarisha amani ama kuchafua mwingine kwa kisingizio cha siku ya wajinga....mfano ukatangaza kuwa polisi wameua watu 10 wakati ni utani unafikiri nini ambacho kwa utani wako huo unaweza kuligharimu jeshi la polisi ....wananchi wanaweza kuandamana kwenda kuvamia polisi kwa utani wako."

Bw Kasesela alisema kutokana na upotoshaji huo kwa jamii amewaita polisi ili kuandika maelezo yao kwa upotoshaji huo dhidi yake na tayari amewaachia baada ya kutoa maelezo hayo na kuwa mbaya zaidi kituo hicho kilitangaza siku moja kabla kuwa asubuhi ya leo watakua na mkuu wa wilaya wakati kimsingi siku ya wajinga ni April Mosi kila mwaka na sio Machi 31.

Alisema kuwa sikukuu ya wajinga ni saa 4 tu na sio zaidi ya hapo na kuwa kutokana na kutangaza uongo huo amepokea simu kutoka kwa waathirika wa mafuriko ambao walikuwa wakilalamika hatua ya serikali kuwaacha walengwa wa chakula cha msaada na kupeleka sehemu ambayo haina shida ya chakula cha msaada hivyo kuvitaka vyombo vya habari kujenga heshima yake kwa kuendesha vyombo hivyo kitaaluma zaidi badala ya kuvitumia kwa upotoshaji.

Hata hivyo waandishi haoa wawili tayari wameachiwa huru baada ya kuhojiwa na jeshi la polisi sababu ya kufanya hivyo.