Loading...
Thursday

Mwalimu Mndeme: Milioni 50 kwa kila Kijiji - Sehemu ya Kwanza

Mtaji wa Milioni 50 kwa kila kijiji zitumike kujenga Tanzania ya Viwanda: Sehemu ya Kwanza

http://i1.wp.com/millardayo.com/wp-content/uploads/2015/12/REUTERS1083589_Articolo.jpg?resize=640%2C400
Katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia mgombea wake ambaye kwa sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dr. John Magufuli, kilituahidi sisi watanzania kwamba serikali yake itagawa kiasi cha shilingi 50,000,000 kwa kila kijiji kama mtaji wa kuwawezesha kiuchumi. Ahadi hii haikuwepo tu kwenye hotuba za kampeni bali imeoainishwa vema kwenye sura ya tano ya Ilani cha Uchaguzi ya CCM ihusuyo uwezeshaji wananchi kiuchumi. Kipengele (d) cha ibara ya 57 katika ukurasa wa 105 inasema hivi:  

Kwa kutambua kwamba kuwawezesha wananchi kiuchumi ni hatua ya msingi katika kujenga Taifa lililoimarika kiuchumi na lenye lengo la kujitegemea, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, CCM kitaielekeza Serikali kutekeleza yafuatayo: (d) Kutenga kiasi cha Shilingi milioni 50 kwa kila kijiji kama Mfuko wa Mzunguko (Revolving Fund) kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia Ushirika wa Kuweka na Kukopa (SACCOS) katika vijiji husika.

Pamoja na ahadi hii, nimesikia msititizo mkubwa wa serikali hasa kupitia Makamu wa Rais Mh. Bi Samia Suluhu Hassan akizikumbusha halmashauri za wilaya kwamba zinawajibika kisera kutenga sehemu ya mapato yao ya kila mwaka na kuyatumia kama mtaji wa kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi.

Msukumo huu wa serikali ya awamu ya tano wa kuwawezesha wananchi kiuchumi ni jambo jema na la kuungwa mkono na kila anayeipenda nchi yetu na mwenye moyo wa uzalendo na kujali hali za maisha za wananchi walio wengi. Hata hivyo yapo mambo ya kujiuliza katika hili:
  1. Wananchi hawa wameandaliwa kwa kiasi gani katika kuzitumia fedha hizi kwa malengo kusudiwa na kuwasaidia kuboresha maisha yao?
  2. Wananchi hawa watazitumia fedha hizi kwa kazi au biashara gani tofauti na zile ambazo wamekua wakifanya kila siku au kuona kwa wengine?
  3. Serikali imejipanga kwa kiasi gani na kwa utafiti upi kuhakikisha makosa yaliyofanywa huko nyuma kwa mipango ya uwezeshaji kama huu hayarudiwi tena?
Nauliza maswali haya kwa sababu kumekuwepo na jitihada nyingi za serikali, sekta binafsi, taasisi zisizo za kiserikali, taasisi za fedha na watu binafsi katika kuwawezesha wananchi wa hali ya chini kujitafutia kipato kupitia mitaji. Mitaji mingi yenye riba kubwa, riba ndogo, na hata isiyo na riba kabisa, imetolewa kwa wananchi wengi kwa miaka kadhaa sasa kupitia Savings and Credit Cooperative Societies (SACCOS), Village Community Bank (VICOBA) na njia zingine. Swali la kujiuliza ni je, mitaji hii iliwasaida walengwa kwa kiasi gani? Imebadili maisha yao kwa kiasi gani? Na je, mafanikio yaliyopatikana yana uzito kiasi gani hata kuwa msukumo wa kuendelea na utaratibu huohuo kupitia pendekezo jipya la kugawa Shilingi 50M kwa kila kijiji?
Kuna kila sababu ya kuwa na taarifa sahihi kabla ya ugawaji wa mitaji hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha itafanya kilichokusudiwa. Nakumbuka Rais aliyemaliza muda wake “alijipatia umaarufu” mkubwa kwa mabilioni yaliyoitwa kwa jina lake lakini hadi anamaliza urais, hatujawahi kupata mrejesho wa mabilioni yale kwa maana ya kujua yako wapi, yalitumiwa au kugawanywa kwa kina nani, yalimsaidia nani, iwapo zilirudishwa serikali, na iwapo zilipotelea kwa ambao walibahatika kuwa “malaika wa zama zake”.
Tanzania ina vijiji takribani 19,000. Kama kila kijiji kikipewa shilingi 50,000,000 serikali itakua imegawa takribani Billion 900 kutekeleza ahadi hii kwa wananchi. Fedha hizi sio kidogo kwani zinakaribia kulingana na makusanyo yetu ya mapato kwa mwezi mmoja. Ni lazima tufikirie vizuri iwapo namna tunavyotaka zitumike italeta tija na kusaidia kuongeza vipato, kuondoa umaskini, na kusaidia walengwa wenye uhitaji. Nchi yetu ina wilaya takribani 150 na hivyo kila wilaya ina wastani wa vijiji 126. Kama fedha hizi zikigawanywa kwa wilaya badala ya vijiji kila wilaya inaweza kupata mgao wa shilingi billion 6.25 za kitanzania. Kwa hali ya nchi yetu, hizi sio fedha kidogo na zikitumika vizuri kimkakati zinaweza kuleta mabadiliko makubwa sana. Kuna changamoto kadhaa zitakazokabiliana na mkakati wa Milion 50 na ambazo zinaweza kukwamisha kabisa kufanikisha kilichokusudiwa au kikachukua muda mefu sana bila kuonesha mafanikio.
  1. Lazima tutegemee kwamba ugawaji wa fedha hizi katika kuwafikia wananchi utakabiliana na siasa nyingi na hata rushwa  hasa katika ngazi za chini. Zoezi hili lazima liandamwe na figusufigidu kubwa sana iwapo litakua mikononi mwa halmashauri kutokana na dhana ya “uungu watu” wa watumishi walioko ngazi za chini karibu na wananchi vijijini.
  2. Wananchi walio wengi hawajaandaliwa namna ya kutumia fedha hizi kwa uzalishaji wenye tija na wengi wana matumaini makubwa yasiyoendana na uhalisia. Watu wengi huwaza namna ya kupata mitaji lakini hawajajiandaa na mchakato wa kuzalisha baada ya mtaji.
  3. Kwa wingi wa wananchi wahitaji kule vijijini, fedha hizi ni ndogo sana unapolinganisha na wingi wa wahitaji wanaohitaji mitaji. Udogo wa mtaji ni kizuizi kikubwa sana katika kufanikisha mradi wa uwekezaji unaotegemewa uzalishe kwa faida.
  4. Serikali inaweza kujikuta inatumia muda mwingi na gharama kubwa sana kujighulisha na uratibu wa zoezi hili
Kwa chamoto hizi na zingine nyingi, nashawishika kwamba kuna haja ya kufiria upya/vizuri zaidi juu ya mkakati huu na utekelezaji wake. Napata shida kuona iwapo fedha hizi zitasaidia wananchi kuboresha maisha yao kiuchumi na iwapo matokeo haya yatakidhi mahitaji ya wakati.
Katika sehemu ya pili ya makala hii, nitapendekeza jinsi mtaji huu wa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji unavyoweza kutumika katika kujenga msingi wa utekelezaji wa mango wa kuijenga Tanzania ya Magufuli yenye uchumi uliojikita katika viwanda.

Imeandikwa na Mwalimu MM


0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP