Loading...
Friday

Natumbua jipu! Sehemu ya IV: Wimbi la PhD za Heshima Tanzania – Utoposhwaji uliofumbiwa macho

Sehemu ya Nne
Makala hii imekua ngumu sana kwangu kuandika kati ya makumi ya makala ambazo nimewahi kuandika kwa sababu inagusa baadhi ya watu nilio karibu nao kwa namna moja ua nyingine. Hata hivyo nalazimika kuandika maana jambo hili linahusu jamii nzima ya kitanzania na madhara yake ni makubwa na sio swala langu pekee au la mtu fulani. Hivyo katika kuoenesha kwa vielelezo ukubwa wa tatizo, nitaomba nisamehewe na wale ambao nitagusa utambulisho wao kwa namna moja au nyingine na niwashauri waitazame mada hii kwa upana na mbele ya kile wanachokiona kinawahusu wao. Kama vile ambavyo viongozi wetu wa dini hukemea dhambi wanaposimama bila “kutazama mtu usoni, cheo chake, au uhusiano wake na wao”, naomba nami angalau kwa makala hii tu nifuate utaratibu huo ili kuweka kumbukumbu sawa na tupone.

Katika sehemu ya kwanza ya makala hii nilitaja kwa makusudi kabisa kwamba, miongoni mwa waathirika wakuu wa biashara ya shahda za heshima uchwara ni waumini wa madhehebu ya Kikristo ambayo kwayo nami ni muumini. Ila leo niingie ndani zaidi kusema kwamba kundi ambalo limeamau kuitakatisha na kukumbatia biashara ya shahada za heshima uchwara ni wakristo wa madhehebu Kipentekoste au maarufu kama ‘walokole’. Utanielewa baadaye kadiri unavyoendelea kusoma sehemu hii ya mwisho kwenye mfululizo wa mada hii. Sijajua sababu nini hasa kwa kundi hili kuparamia heshima badala ya elimu na watu tofauti wana maelezo tofuati.
C:\Users\User\Dropbox\155 Uandishi\gwajima.jpg
C:\Users\User\Dropbox\155 Uandishi\Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera akivishwa kofia ya udaktari wa Heshima ..JPG
C:\Users\User\Downloads\12819254_1256740811009200_7250989661072100148_o.jpg
https://3.bp.blogspot.com/-uqxwOl8ohiQ/VrgU4qaWWiI/AAAAAAAAVMg/a34o5bfHIo8/s1600/1.JPG
https://3.bp.blogspot.com/-kmJ0Bzl0hN8/VrgNgsGT_PI/AAAAAAAAVLY/i685qwemkcs/s1600/IMG_7069.JPG
https://4.bp.blogspot.com/-CK5f3ETM3E4/VrgU5qzjl2I/AAAAAAAAVMw/2wkO3qs4dks/s1600/IMG_7263.JPG
https://4.bp.blogspot.com/-N0f7BkE3Hc8/VrgNhYdpV3I/AAAAAAAAVLs/_IY2EeMdUhI/s1600/IMG_7091.JPG
http://3.bp.blogspot.com/-jq0ur7RtCvk/TYTZPSXv2qI/AAAAAAABfBY/OyBO8Gs3gHQ/s1600/IMG_0019.JPG
C:\Users\User\Downloads\IMG-20160320-WA0002.jpg
Baadhi ya watu maarufu walionunua stashahada, shahada, na PhD za heshima toka vyuo uchwara
Mtu mmoja alisema huenda hii inatokana na ukweli kwamba madhehebu kongwe kama Katoliki, Anglikana, Lutherani na mengine kama hayo, yamejaa wasomi waliobebea elimu ya dini (theology, philosophy of religions, divinity, etc) kwa ngazi za shahada ya kwanza hadi PhD na madhehebu haya hueshimu eleimu kama msingi mkuu wa utumishi katika kanisa. Kwa uapnde mwingine, kwa muda mrefu madhehebu ya kipentekoste yamekua hayaweki mkazo sana katika elimu kama kitu cha muhim na lazima kwa watumishi wao na badala yake wanatukuza “upako na wito” bila kujali maandalizi ya matumizi yake. Hata hivyo huenda madhehebu haya yamefika mahali yamejikuta yanakosa nguvu, mvuto na ushawishi katika jamii kwa kuwa na viongozi wengi ambao uwezo wao wa kitumishi unatiliwa mashaka kwa kukosa elimu itakayosaidia wito wao kutumika vizuri. Matokeo yake wameamua kutafuta njia ya mkato “kutafuta usawa” kupitia utukufu wa heshima za kununua.
Baada ya kushuhudia wanasiasa wakijitwalia “PhD za online” toka kwenye vyuo visivyojulikana pamoja na za heshima na kuanza kujitambulisha kama madokta, “walokole” wengi tumejikuta “tumelelemewa na upako” wa shahada na heshima za mkato huku tukiongozwa na viongozi wetu. Huenda kiu hii inatokana na ile hali ya kutaka imani zetu ziendane na mamlaka na heshima ambazo hata hazima maana wala utukufu kwa yule tunyemwamini na kumtumikia. Tunalazimisha kuonekana bora, wa maana, tumesoma, tuna akili sana, tuna upako, na sasa tuna PhD za heshima. Nimefuatilia watunukiwa wa shahada hizi kwa miaka kama nane  sasa na niseme tu kwamba ni jambo ambalo limenisumbua sana hasa baada ya kuona jinsi ambavyo uongo na udanganyifu vinabadilishwa na kuonekana kama ukweli.
Nakumbuka siku moja ya Jumapili miaka kama mitano hivi nikiwa kwenye nasikiliza ibada ya kanisa moja iliyokua inarushwa moja kwa moja na kituo cha radio cha Kikristo nilisikia kitu kilichonichefua kuhusu hizi shahada za heshima. Aliyekua anaongoza ibada alitangaza kwamba “Baba Mchungaji” wao katunukiwa PhD na chuo chenye jina la “XXX Global University” na hivyo kwa sasa ni “Baba Mchungaji Dokta YYY”. Ili kuonesha kwamba baba mchungaji huyu sio wa kawaida tena, akasema kwa sasa ana heshima sawa na ya Rais XXX maana naye ni Mh Rais Dokta ZZZ. Kama viel haitoshi akasema watu wengine wamepewa degree na vyuo vya kawaida tu vya Tanzania lakini Baba Mchungaji wao kapewa na chuo cha Global ikimaanisha chuo cha dunia nzima na hivyo PhD yake ni ya juu zaidi kuliko zilizotolewa nan a vyuo vya ndani. Kusema ukweli nilisikia aibu na hasira ndani yangu na nilijipa kibarua cha kumjua kwa undani aliyekua anaongoza ibada na kutamka maneno hayo. NIlisikitika sana nilipogundua aliyekua anaongea maneno yale ni msoni wa ngazi ya shahada. Kilichonisumbua zaidi ni pale nilipoona kuanzia siku ile mchungaji yule hatambulishwi bila kuanza na cheo cha udokta. Nilijiuliza maswali matatu yafuatayo:
 • Huyu mchungaji na kondoo zake wanajua maana ya shahada ya heshima? Kwa nini wanaongea jambo la aibu namna hii kwenye radio inayosikilizwa na maelfu ya watu?
 • Hivi mchungaji huyu na washarika wake wanaomshangilia (hasa huyu aliyekua anamsifu) wamefanya utafiti wa kukijua hicho chuo “kilichomgawia PhD” ni cha aina gani na iwapo alichopewa ni heshima ya ukweli au aibu?
 • Kwa nini watu wanaomjua Mungu wakubali kufunikwa na upofu kwa jambo ambalo wanaweza kulitambua kwa utashi walionao?
Siku moja nilimuuliza mtu aliye karibu na Mchungaji mmoja ambaye naye alivishwa udokta uchwara, “Ni kwa nini mchungaji wako ambaye anaonekana ni mwelewa sana kakubaliana na jambo hili?’ Akanijibu kwamba Mchungaji wake aliona ni heshima maana watu hao walimfuata na kumletea fomu ajaze na kuilipia hivyo akaona ‘bwana kafanya muujiza kumtambua mchango wake’ na hana budi kuukumbatia mmujiza wa ukodta. Swali la kujiuliza hapa ni je,hivi kama nikiletewa fedha za wizi ofisini kwangu huku nikijua nitangepokea ili mradi mimi mwenyewe sikuziiba na aliyenileta kaleta kwa kupenda mwinyewe?

Nini Kinafanyika katika utoaji wa shahada uchwara za heshima?
Ndani ya miezi michache iliyopita tuliona kundi kubwa la watu waliopewa au kumwagiwa shahahada za heshima hapa Dar es Salaam na kule Mwanza. Wingi huu ullinisukuma kutafuta kuelewa mchakato unaotumika kuwapata watu hawa na kuwatunuku wanachotukunikiwa. Niliyokutana nayo nalazimika kuyasimulia maana kwangu niliyaona ni kama mchezo wa kuigiza tena usioigiza ukweli.
Katika uchunguzi wangu niligundua kwamba kuna vyuo kadhaa ambavyo vyote havina kampasi wala ofisi Tanzania ambavyo vinafanya biashara ya shahada za heshima (kwa lugha ya kingereza vinaitwa Diploma Mills) Vyuo hivi uchwara vinatumia watu wanaoitwa wawakilishi wao hapa Tanzania ambao nao ni wafaidika wa shahada hizo hivyo wanaitwa madokta au maprofesa na wengi wao ni wachungaji/maaskofu wa madhehebu ya kipentekoste au wakristo wenye majina na vyeo. Wawakilishi hawa hupendekeza watu wanaoona wanawafaa ambao huwatumia kama sehemu ya kamati/timu yenye jukumu la kupendekeza nani wapewe heshima hizo (PhD, shahada ya uzamili, shahada ya kwanza, stashahada, na cheti). Kamati hii ya ufundi ikishakaa na kupendekeza majina, huwapekelea wahusika barua zenye taarifa hiyo ya kutunukiwa shahada au stashahada au cheti. Pamoja na barua hiyo, wateule hawa hupewa fomu ambayo wanatakiwa kuijaza kulingana na aina ya heshima anayopewa. Katika orodha ya moja ya vikao vya kupitisha majina ya watu wanaotakiwa kupewa tuzo ambayo nimebahatika kukutana nayo, kuna majina zaidi ya 100 yaliyopendekezwa.
 • Sehemu kubwa ya majina haya ni ya maaskofu, wachungaji, watangazaji wa radio na runinga, waimbaji wa nyimbo za injili na wakristo wengine wenye majina au nafasi kubwa za kiungozi na biashara. Sikubahatika kuona mtu aliyetamulishwa kwa dini tofuati na ukristo. Kwenye kundi la waimbaji wa injili nilishangaa kuona majina karibu ya waimbaji wote ninawajua hapa Tanzania kuanzia wale ambao hawajamaliza darasa la saba hadi wale wenye degree. Halikadhalika, nilishangaa nilipoona baadhi ya shahada zimetolewa kwa mafungu hasa pale zinapopewa kundi zima la kwanya ya kanisa. Huu ni muujiza ambao nadhani unapatika kwenye sayari ya Jupiter pekee kwa shahada au stashahada kupewa  kundi.
 • Majina yako kimakundi: Kundi la waliopewa PhD ni la watu ambao angalau wana shahada moja au elimu inayofanana na hiyo na uzoefu wa miaka kama kumi. Kundi la pili ni la wanaopewa shahada za uzamili na hawa nao ni wale ambao angalau wana diploma. Kundi la tatu ni la wanaopewa diploma/stashahada ambao hao ni wale ambao angalau wana cheti. Kundi la mwisho ni wanaopewa cheti ambao hawa ni kuanzia ambaye hajamaliza darasa la saba hadi cheti ili mradi ana jina na utumishi
 • Moja na vituko nilichokiona wakati nachambua majina haya, ni kuona wale ambao wanachambua majina na kupitisha wahusika wa kupewa heshima hizo (yaani wajumbe wa kamati ndogo ya ufundi), nao wako kwenye orodha ya wanaopendekezwa kupewa shahada za heshima. Kwa kifupi walikua wanajipendekeza na kujitathmini kupewa shahada za heshima
 • Miongoni mwa wajumbe wa kamati ya ufundi, hakuna mwenye elimu ya ngazi ya PhD na baadhi yao hawana elimu hata ya shahada ya kwanza. Hivyo watu ambao hawana shahada na ambao hawajui PhD inapatikanaje, ndio wanapendekeza na kuweka vigezo vya nani apewe PhD ya heshima pamoja na tuzo zingine
 • Muujiza mgumu kabisa katika mchakato huu, ni kuona kwenye minutes/dondoo za kikao cha kamati ya ufundi wajumbe huanza na kufunga vikao vyao kwa maombi ikimaanisha wana kibali cha Mungu wao katika kile wanachokifanya.
 • Kama vile haitoshi vikao vya kujadili tuzo hizi za heshima zinafanyikia ama mitaani /vijiweni kwenye migahawa au nyumbani kwa mmoja wa wajumbe.
Nini kinatokea kwa wanaotunukiwa?
Wale “wanaobahatika” kupewa heshima hizi za ajabu, hutakiwa kupitia yafuatayo:
 • Baada ya kupokea barua za kuwataarifu heshima wanazopewa, wahusika hutakiwa kujaza fomu ambayo pamoja na mambo mengine hutakiwa kuorodhesha mambo kadhaa ambayo wamefanya yenye kuthibitisha ustahili wao wa heshima husika. Kwa anayepewa PhD anatakiwa ataje angala mambo aliyofanya na anayodhani ni mchango wake kwa muda usiopungua miaka 15. Hivyo mimi kama mchungaji mteule naweza kutaja kwamba huwa nahubiri, nasadia watoto yatima, nafanya ushauri nasaha, nasuluhisha ndoa, nimechangia watoto waliokosa ada za shule, nk. Haya yanatosha kabisa kunipa PhD ya heshima. Fomu hii hutakiwa kurudishwa wiki mbili baada tangu alipopewa barua.
 • Mteule huyu hutakiwa kurejesha fomu iliyojazwa akiambatanisha wasifu wake (CV) na vielelezo vyovyote alivyonavyo juu ya utumishi wake kwa jamii na kisha kurudisha akiwa ameambatanisha na ada alizoelekezwa kulipa. Kwa wanaopewa PhD, hutakiwa kulipia dola za kimarekani 1,500 kama ada ya kutunukiwa heshima hiyo pamoja na shilingi laki tatu (300,000) za kitanzania ambazo ni gharama ya mhafali na joho atakalovaa. Kwa wale wanapewa shahada za chini hadi vyeti, ada hupungua kulingana na heshima anayoinunua na wale wa mwisho kabisa (cheti) hutakiwa kulipia heshima ya cheti chao kwa shilingi laki tano (500,000) za kitanzani pamoja na ile laki tatu ya joh. Bezi hizi ni kwa watahiniwa wa karibuni kabisa (current) na wale wa miaka kama tano hivi iliyopita ada zao zilikua pungufu lakini walilipa na ilikua ni kwa dola pia.
 • Wakisharudisha fomu zao na ada iliyoelekezwa kwa wale wawakilishi wa vyuo hivi, basi moja kwa moja mhusika hupitishwa kama mtunukiwa na hakuna namna yoyote ya kuhakiki iwapo yale aliyojaza kama mchango wake kwenye jamii yana ukweli na ni kwa kiasi gani
Kama wewe ni mmoja wa ambao wameshuhudia mahafali ambayo yamefanyika siku za karibuni na kuwatunuku makumi ya watu heshima, na picha zao zimesambaa kwenye mitandao, basi ujue kwamba huu ndio mchakao wanaliopitia. Kama mchungaji na askofu wako kapewa PhD na vyuo hivi uchwara, ujue amelipia heshima hiyo ambayo ni “fedha uliyombariki nayo naye kaenda kujibariki kwa PhD ya heshima”. Hii ni aibu, ujinga na dharau kubwa sana sio tu kwa taaluma na elimu, bali kwa mantiki nzima ya shahada za heshima. Kwa kifupi huku ni kuidanganya  na kuipotosha jamii kwa kiwango cha juu sana.  
Ukirejea sehemu ya pili na ya tatu ya makala hii, nilioanisha mchakato na vigezo vya utoaji heshima unaotumiwa na vyuo makini duniani na mantiki ya heshima hizo. Jaribu kulinganisha utaratibu huo na mchakato huu  wa wafanya biashara ya shahada za heshima kisha uniambie iwapo tuna ujasiri wa kuutazama huu mchezo wa uchuuzi  kwamba ni jambo la kuheshimiwa. Iwapo jambo hili lingetazamwa kwa hili uzito stahiki, tungeona kwamba hata ile heshima ndogo wanayostahili iliwapasa kunyang’anywa kwa kujiingiza kwenye utapeli huu usio wa kimaamdili ya kiimani wala kijamii. Mchakato unaotumiwa na vyuo vikuu makini duniani kuwapa watu shahada za heshima ni mchakato unaogharamiwa na vyuo vyenyewe maana wao ndio wanaonzisha mchakato huo na kumzawadia muhusika heshima hiyo. Hali kadhalika, wao ndio hufanya utafiti wa mchango wa mtu husika na sio mtu mwenyewe “kujifagilia” kwa wasifu wake kustahili heshima hiyo.
Kuna maswali kadhaa ya kujiuliza?
 • Hivi vyuo vinavyokuja kufanya biashara ya kugawa heshima hapa Tanzania vinapitia mlango gani? Vina ruhusa ya taasisi gani ya umma inayoratibu mambo yahusianayo na vyuo vikuu?
 • Je, hizi fedha wanazokusanya baada ya kuuza tuzo za heshima zinakwenda wapi? Zinasafirishwa nje ya nchi au zinabaki hapa nyumbani?
 • Je, wachuuzi hawa wanalipa kodi za nchi kwa kufanya biashara ya shahada za heshima? Na kama hawalipi ni kwa nini?
 • Ni kwa nini watu wanaotukiwa heshima na vyuo hivi uchwara wanasisitiza sana kutambulika kwa kuitwa madokta kitu ambacho ni kinyume na utaratibu wa shahada za heshima?
Mfano vyuo uchwara vinaavyouza shahada za heshima kwa wingi Tanzania
Katika sehemu za awali za makala hii, nilionesha umuhimu wa shahada za heshima kwa wanaozipokea kua ni lazima uendane na uhalali, heshima, umakini na uhalali wa chuo husika (integrity and credibility). Kwa ulimwengu wa sasa hakuna chuo Kikuu makini ambacho kitafanya kazi zake na kuhifadhi taarifa zake ndani ya mafaili na kuweka kabatini. Vyuo makini vyote duniani vimeweka taarifa zao nyingi kwenye website ili kujitangaza na kuonesha kile wanachofanya. Nimejaribu kutafiti vyuo hivi kuona vinaelezewaje na vina kitu gani kwenye websites zao. Vingi ya vyuo hivi havina taarifa zinazoeleweka kwenye mitandao na vingine vina websites uchwara za kuwadanganya wale wateja wao wa heshima uchwara. Kwa mfano:
 1. Omega Global University (Maarufu kama OGU): Chuo hiki kinachotambulishwa kwamba kiko nchini Afrika Kusini na ni maarufu kwa “kuuza shahada kwa wingi hapa kama pipi” hasa watumishi. OGU kina website ya ajabu na yenye kudanganya (hii hapa: http://ogu.org.za/ ). Webiste hii imejaa picha nzuri za kuvutia lakini bila maelezo yoyote ya kitaaluma. Kinaonesha kina schools (Ndaki) nyingi lakini unapobofya kusoma habari za schools (ndaki) hizo, unakutana na picha au ukurasa zisizo na taarifa yoyote.
  • Kama vile haitoshi, nimejaribu kutumia teknolojia ya google maps kupata anuani kamili (mahali kilipo na kampasi ya chuo hiki nchini Afrika Kusini lakini anuani waliyoitoa kwenye website yao haitambuliki kitu ambacho sio cha kawaida na ni aibu.
  • Pia nimejaribu kutuma barua pepe (email) kwa anuani ambayo imewekwa kwenye website yao ambayo ni [email protected] na kukuta anuani hii ni uchwara/ ya uongo/ fake na haipo. Hakuna domain name yenye jina la http://omegaglobaluniversity.org.za . Ukituma ujumbe kwenye anuani hii iliyoko kwenye tovuti yao unapata jibu hili:

Delivery to the following recipient failed permanently:     [email protected]
Technical details of permanent failure:  DNS Error: 90269123 DNS type 'mx' lookup of omegaglobaluniversity.org.za responded with code NXDOMAIN. Domain name not found: omegaglobaluniversity.org.za


  • Katika utafiti wangu, nimegundua kwamba chuo hiki ndicho kimetunuku tuzo za kumwaga za PhD kwa wachungaji wengi maarufu hapa mjini na hasa walioko Dar es Salaam. Sehemu kubwa (sio wote) ya wachungaji wa makanisa ya kipentekoste yaliyoko Dar es Salaam wanaojitambulisha kama madokta. Hawa ni pamoja na wa makanisa ya TAG, Agape, Ufufuo, na mengine mengi. Wengine ni pamoja waimbaji mashuhuri wa nyimbo za injili, viongozi wa waiambaji wa musiki wa injili.
 • African Graduate University (maarufu kama AGU):  AGU kinajitambulisha kwamba kiko nchini Siera Leone ni chuo kingine ambacho hivi karibuni kimeuza vyeti, stashahada, shahada, na PhD za heshima kwa wingi kwa wakristo (wengi wao wakiwa ni watumishi na washarika wa madhehubu ya kilokole).  Website ya chuo hiki nayo ni ya ajabu, ya ovyo na isiyo na taarifa muhim za chuokikuu kama ilivyo chuo cha OGU kwa kile nilichokileza mwanzoni (tazama hapa: http://agusierraleone.org/ ). Chuo hiki hakina taarifa za mawasiliano wala chochote ambacho ungetegemea kukiona kwenye website ya chuo kikuu. Ni cha kizushi na usanii mtupu. Wewe jiulize, tangu lini Siera Lione moja ya nchi mbovu kabisa Afrika kwa mambo mengi iwe na chuo cha kuja kutunuku watu shahada Tanzania?
Vyuo hivi vya OGU na AGU, vina mfumo wa ajabu kabisa wa kugawiana “utukufu huu wa PhD za heshima”, kwnai wale waliopewa PhD za heshima awali kwa sasa ndio “wamekua magwiji” wa kuwagawia wengine na ndio huongoza mahafali. Baadhi yao ambao tayari “wamekubuhu katika zoezi hili” wameshapewa vyeo vya uprofesa wa heshima.
Hii ndio status/hadhi ya vyuo vinavyowatunuku heshima za PhD na hawa ndio “wapakwa mafuta wetu” walioamua kujipandisha hadhi yao ya kitumishi kwenye jamii kwa kununua udokta. Jambo la kujiuliza ni iwapo watu wanaopewa heshima hii wanajiridhisha ya heshima hizi kama nilivyoshauri kwenye makala iliyotangulia au iwapo wanaona kila kitu ni “muujiza na utendaji wa bwana” hata pale wanapoingia mfukoni kununua heshima hizi. Makanisani mwa watumishi hawa kumejaa wasomi wa ngazi mbalimbali ambao wangeweza kuwasaidia viongozi wao kuchukua taadhari na kujiepusha na dharau hii. Kwa nini nao wanakubaliana na jambo hili?
Kote duniani tangu ukristo ulipoanza, utoaji wa elimu (ya kidunia na ya kidini) imekua ni moja ya mikakati ya muhim sana katika kujenga jamii ya waamini ambao ana uelewa mpana wa kile wanachokiamini na ulimwengu/mazingira yanayowazunguka. Kama sehemu ya kuhubiri ukristo na kuifikia jamii yenye uhitaji, wakristo amejenga shule na vyuo na kufungua milango ya watu kusoma kadiri ya uwezo wao. Hata kanisa la sasa bado limeendeleza jukumu hili na ndio mana katika nchi yetu kuna shule na vyuo vingi vinavyomilikiwa na makanisa. Ni jambo la aibu na ajabu sana kuona leo kundi la wakristo wanaoijua kweli, kujivika upofu na kuuvaa upotoshaji kwa kuacha kutafuta elimu ya dini na dunia kupitia mifumo ya kielimu inayoeleweka na badala yake kutafuta heshima za kitaaluma kwa njia za mkato na za udanganyifu. Huu sio Ukirsto wala misingi ya mafundisho ya Imani ya Kikristo yanayosisitiza uadilifu, ukweli, uaminifu, bidi, kujisomea, kufuata taratibu, na kuepuka maovu. Hakuna mtumishi wa kanisa asiyejua ile Mithali isemayo “mtafute sana elimu, wala usimuache aende zake” na Mithali hii imekua ikitumiwa sana kuwashawishi na kuwashauri watu kuheshimu elimu. Uchuuzi wa shahada za heshima kwa mgongo wa kanisa na utumishi, ni kuharibu kabisa dhana ya ukristo kuwa kioo na mwanga wa jamii katika kujenga jamii inayochukia na kukataa maovu.

Hitimisho:
Nashawishika kuhitimisha makala hii maana nimeandika kwa kirefu. Natamani jamii yetu ya kitanzania na vyombo vinavyohusika na uratibu wa elimu na taasisi za dini, walitazame jambo hili katika uhalisia wa hatari na hathari zake kwa nchi yetu.
 • Niwashauri wale wote wanaopenda elimu wakaitafute darasani na kwenye vitabu maana inapatika na waachane na kujivika heshima uchawara zisizo na msaada kwao
 • Sio kila heshima unayopewa ni heshima na wakongwe wetu walisema heshima hainunuliwi barabarani. Ukijiheshimu utaheshishimika na watu watakuja kutafuta heshima kwako
 • Serikali au vyombo vinavyohusika na uratibu wa utoaji elimu, vitazame hili tatizo la biashara ya shahada za heshima ambao wajanja wanaozifanya wameamua kupitia mgongo wa kanisa au Imani ya kikristo, kupata wateja kirahisi na kuepuka kujulikana udanganyifu wao kwenye jamii. Watu hawa watizamwe na kuchukuliwa hatua stahiki ili kulinda heshima ya nchi yetu na kuiheshimu elimu
 • Viongozi wa dini watambue kwamba heshima waliyonayo ni kubwa sana. Kubwa kuliko udokta, uprofesa, urais na kingine chochote kile kwani utumishi wao uko wa Mungu aliyeumba mbingu nan chi na ambaye kwake vyote vilitoka na vyote vitarudi. Hawana haja ya kujichafua katika jitihada za kutafuta heshima
 • Viongozi wa dini na kanisa kwa ujumla wake wawe mfano kama ambavyo kanisa limekua mfano kwa Karne nyingi katika kuheshimu elimu na taratibu zake. Sio hivyo tu, bali katika kusoma na kusisitiza jamii kujisomea ili kupata mwanga na maarifa ya kuboresha maisha yetu na jamii tunamoishi. Wawashawishi wale wanaowangoza kupenda elimu na kwenda shule kuitafuta kwa bidiii yote
 • Serikali ifuatilie mapato yatokayo na biashara ya hii kwani ni fedha nyingi zinakusanywa kwa mgongo wa kikanisa huku ikiwa zinapatikana kibiashara kama ilivyo kuuza nyanya. Pia ikataze vyuo vyote kutoka nje kufanya biashara ya aina hii ndnai ya mipaka yetu
 • Nivishauri vyuo vikuu vya ndnaiya nchi yetu, kuachana na biashara ya kugawa PhD za heshima kwa kila wanayejisikia. Heshima hii itolewe pale tu inapodhiirika kuna mtu anastahili na sababu za kutunuku ni wazi kwenye jamii. Sio lazima kuzitoa kwenye kila mahafali na zisitolewe kwa hofu za kidini wala kisiasa.
 • Mwisho, niwshauri wale wote wanaopenda kujiheshimu na wamegundua kwamba wamejipotezea heshima zao kwa kujinunulia shahada za heshima, kwanza watubu, wawaombe radhi wale waliowadanganya kwa matumizi ya udokta katika kutukuza heshima uchawara, wazikane shahada hizo ikiwa ni pamoja na kuwazuia watu wasiwatambulishe na udokta. Hakuna njia mbadala wa dhambi zaidi ya kuitubu, kuikataa, na kuiacha.
Nakushukuru kwa kusoma makala hii.
Imeandikwa na Mwalimu MM

Waweza mwandikia kupitia mmmwalimu(at)gmail.com

 
Toggle Footer
TOP