Loading...
Friday

Raia wapiga kombolela! Sukari iliyofichwa tani 24 yakamatwa Singida

Watu waliochoka na tabia za kipuuzi za wafanyabiashara kuficha sukari ili kutengeneza uhaba ambao haustahili na kuuza bidhaa hiyo kwa bei ya juu wamesaidia kukamatwa kwa mifuko 655 ya sukari sawa na tani 24.3. wilayani Singida.

Pamoja na kukamatwa kwa mifuko hiyo, wafanyabiashara wawili pia wametiwa ndani kuhusiana na bidhaa hiyo ambayo ilifichwa stoo.

Waliokamatwa ni Mohamed Alute Ally (44) mfanyabiashara wa eneo la Unyankindi aliyekutwa na mifuko 335 ya kilo 25 kila mmoja na Yusufu Suleiman (39) mfanyabiashara wa eneo la Minga katika Manispaa aliyepatikana na mifuko 320 ya kilo 50.

Taarifa ya kukamatwa kwa sukari hiyo na wafanyabiashara hao ilitolewa na mwenyekiti wa kamati ya usalama ya wilaya ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Singida, Saidi Amanzi .

Amanzi alisema waliendesha msako baada ya kupata taarifa za siri kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao walikuwa wanaficha sukari ili waweze kuiuza kwa bei ya juu.

Taarifa inasema kwamba mfuko mmoja wa sukari ambao huuzwa 92,650/- sasa unauzwa kati ya 115,000/- na 120,000/- huku kilo moja ikiuzwa kati ya 2,400/- na 2,800 kwa kilo kinyume na bei elekezi ya 1,800/-.
 
Toggle Footer
TOP