Loading...
Sunday

Ripoti inasema Tanzania ni nchi ya 1 Afrika na 3 duniani kwa kuzalisha ufuta

Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Kilimo ya Naliendele imetoa ripoti na kueleza kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika na ya tatu duniani kwa uzalishaji wa ufuta.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania imekuwa kinara baada ya ugunduzi wa mbegu aina ya Lindi 2002 inayozalisha ufuta wenye uzito mkubwa na kustahimili magonjwa ukiwa shambani.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk Omar Mponda amesema uzalishaji wa ufuta umeongezeka maradufu kutoka tani 30,000 mwaka 1990 hadi kufikia tani 460,OOO mwaka huu, hivyo kuifanya Tanzania kuwa ya tatu ulimwenguni ikiongozwa na nchi za Myanmar na India. “Mtu anaweza kusema hawa watafiti wanafanya kazi gani, kazi yetu inachukua muda mrefu kupata teknolojia kwa sababu kupata mbegu bora siyo chini ya miaka 10, hivyo unatakiwa uwekeze kwa kipindi hicho kabla ili uje kupata mbegu.

“Lakini napata faraja kama mtafiti kwa kupata mbegu kwani sasa hivi tunaweza kujivunia kwenye ufuta na tuna karibu aina nane,” amesema Dk Mponda.

Hata hivyo, baadhi ya wakulima wanasema maisha yamebadilika kutokana na kilimo cha ufuta baada ya kutumia mbegu ya Lindi 2002 iliyofanyiwa utafiti na taasisi hiyo.

Mmoja wa wakulima hao, Abdallah Salum alisema amepata mafanikio kwa kilimo cha ufuta.

“Sasa nina nyumba mbili za bati na ninasomesha watoto sekondari kutokana na mavuno ya mbegu hii ya Lindi 2002 na hata uzito wake ni tofauti na mbegu zetu za kienyeji tulizokuwa tukizitumia hapo awali,” amesema Salum.

Zainab Mkwiru alisema kilimo cha ufuta kinamuwezesha kujikimu kimaisha.

“Zamani nilikuwa nalima, lakini sikuwa napata faida kwani nilikuwa nalima kwa ajili ya matumizi yangu...baada ya kuonana na washauri wa utafiti na kilimo sasa nafanya kilimo cha biashara na kumudu gharama za maisha,” amesema Mkwiru.

Ufuta unalimwa kwa kipindi cha miezi mitatu na tayari wakulima wameendelea kunufaika kwa kipindi kifupi kutokana na uwapo wa soko.

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP