Taarifa ya IPTL, PAP kuhusu habari iliyochapishwa gazetini, "Siri za Kikwete, IPTL zafichuka"

Kaimu Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan African Power Solutions (T) Limited Bwn. Joseph O. R. Makandege (katikati). Kulia ni Mkurugenzi wa uendeshaji wa IPTL Bwn. Parthiban Chandrasakaran na kushoto ni msaidizi wa mwenyekiti mtendaji Bwn. Rajiv Bhesania
Makampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan Africa Power Solutions (T) Limited (PAP), tumesononeshwa sana na taarifa iliyochapishwa na gazeti la kila wiki la MwanaHALISI katika toleo namba 332 la tarehe 28 Machi 2016 lenye kichwa cha habari, “Siri za Kikwete, IPTL zafichuka”; iliyoambatana na nukuu katika ukurasa wake wa mbele inayosomeka “…hadi ndani ya jumba jeupe (Ikulu kwenyewe), Singasinga alitembeza mlungula.

Taarifa hiyo iliyojaa uongo pamoja na kashfa nzito ya rushwa kwa IPTL/PAP na kwa viongozi waandamizi wa serikali ya awamu ya nne na wengine ambao bado wamo katika serikali hii ya awamu ya tano, imediriki kudai kwa kunukuu maneno yafuatayo,….. “Sethi alitoa rushwa kila mahali, ikiwamo Ikulu, ili kufanikisha mpango wake huo….Alihonga kila mtu. Alitoa rushwa kwa kila aliyeona faili la Escrow. Hadi maofisa wa Ikulu na viongozi waandamizi kutoka wizara ya fedha……..hadi ndani ya jumba jeupe (Ikulu kwenyewe), Singasinga alitembeza mlungula. Ni BoT pekee, ambako hakuhonga au kuombwa rushwa.”

Tungependa kukanusha taarifa hizi za shutuma ya rushwa ambazo ni za uongo na uzushi mtupu wenye lengo la kuichafua IPTL na wamiliki wake akiwemo Mwenyekiti Mtendaji, Bw. Harbinder Singh Sethi. Taarifa hizi zisizo na chembe ya ukweli ndani yake zinalenga kuchafua sifa ya Ikulu ambayo ni taasisi nyeti hapa nchini kwa kuihusisha na upokeaji rushwa ambayo ni kosa la jinai kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi yetu.

Isitoshe taarifa hizi zimejaa habari za uongo zilizobuniwa kwa nia na madhumuni maovu ya kuichafua sifa za kampuni za IPTL/PAP na mwenyekiti wake Bw. Harbinder Singh Sethi pamoja na kuwachonganisha dhidi ya wananchi wa Tanzania kwa kuwahadaa na kuwaaminisha Watanzania kuwa IPTL/PAP inaendeshwa kwa misingi ya rushwa na udanganyifu, hivyo basi haistahili kufanya biashara hapa nchini.

Awali ya yote, tungependa kuutarifu umma wa Watanzania kwamba tuhuma za rushwa ni tuhuma nzito na wala siyo za kunyamaziwa kabisa. Rushwa ni moja kati ya makosa makubwa ya kijinai ambayo vyombo vya dola vinatilia maanani sana. Hivyo basi, kampuni ya IPTL/PAP haiwezi kukaa kimya wakati tuhuma kama hizi zikiendelea kuchapishwa dhidi yake, huku ikiwahusisha viongozi waandamizi wa serikali, bila ya gazeti husika pamoja na mwandishi wa taarifa hizo kutoa udhibitisho wowote wa tuhuma hizo.

IPTL/PAP tunaamini kwamba taratibu zote za kukabidhiwa kampuni ya IPTL (ikiwemo mali na madeni halali) zilifuatwa. Tunaamini katika utawala wa sheria ambayo inazingatia haki za kila mtu. Hivyo basi, haitakuwa busara kuendelea kunyamazia vitendo vya kiovu vya kuichafua kampuni yetu vinavyofanywa na baadhi ya vyombo vya habari kwa kisingizio cha “uhuru wa kutoa maoni” au “uhuru wa vyombo vya habari”. Kama vyombo vya habari walivyo na uhuru wao, vivyo hivyo IPTL/PAP kama kampuni ina uhuru wa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria za nchi bila ya kubughudhiwa. Kwa kutuhumu IPTL/PAP au viongozi wake kutoa rushwa, bila kuthibitisha, ni kuihujumu kampuni ili isiweze kutekeleza majukumu yake ya kuchangia ukuwaji wa uchumi wa nchi yetu.

Joseph O. R. Makandege (ADVOCATE)
(Katibu na Mshauri Mkuu wa Sheria)
KAIMU MWENYEKITI MTENDAJI
Independent Power Tanzania Limited / Pan African Power Solutions (T) Limited.