Loading...
Thursday

Taarifa ya SSRA: Serikali yaanza kulipa deni la Mifuko a Hifadhi ya Jamii; Maoni ya kuunganisha mifuko

Serikali imevalia njuga swala la deni la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Hadi kufika mwezi Machi, 2016 tayari Serikali ilikuwa imeshalipa Jumla ya Bilioni 173.11 kwa Mfuko wa PSPF. Mfuko huo umeweza kulipa Hundi 49,467 ambapo kati ya hizo hundi 46,000 ni za pensheni za kila mwezi kwa wastaafu na Hundi 3,467 ni za madai mapya ya Pensheni. Taarifa zinaonesha kwamba Serikali imedhamiria kulipa deni lote la michango ifikapo June 2016.

Kuhusu hati Fungani (Non cash Bond) taarifa zinaonyesha kwamba mifuko ambayo ilikuwa bado kuridhia hati ya Makubaliano (deed of settlement) hivi sasa imeridhia. Serikali inatarajia kutoa Hati Fungani (non-cash bond) ya Shilingi Trilioni 2.6 yenye riba ya asilimia 6.5 kwenda PSPF. Hati Fungani hii itaiva kwa muda tofauti ili kuwezesha mfuko kukidhi mahitaji yake ya malipo ya mafao. Hati fungani hizi zitaiva kwa vipindi tofauti tofauti. Yaani kuna hati fungani za miaka 3, miaka 5, miaka 7, miaka 10 na kuendelea.

MIRADI YA UWEKEZAJI

Mamlaka kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania kwa mujibu wa Kifungu cha 6(2)(c) cha Sheria Na.8 ya mwaka 2008 ikisomwa pamoja na kifungu cha 40 na kifungu cha 48 Mamlaka ilikamilisha kaguzi za Mifuko kwa mwaka 2015. Kaguzi hizi zimepelekea Mamlaka kwa kushirikiana na Benki Kuu kufanya kaguzi maalumu (Special Inspection) kwenye majengo na milki za Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii ikiwa

ni pamoja na Mfuko wa NSSF. Kaguzi hizi zimeanza toka mwezi Januari 2016. Huu ni ukaguzi wa kina sana hivyo unatarajiwa kuchukua kati ya miezi 6 hadi 9 kulingana na upatikanaji wa taarifa zinazohusika. Hata hivyo wakati kaguzi zikiendelea Mifuko iliyovuka viwango vya uwekezaji tayari imezuiwa kuendelea kuwekeza katika maeneo hayo. Taarifa ya ukaguzi maalumu, itakapokamilika itasaidia Serikali kuchukua hatua stahiki. Tunaomba kuwaondoa wasiwasi wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kuwahakikishia kwamba michango yao ipo salama na Mamlaka inazifanyia kazi kero zao kwa bidii kubwa.

Maoni ya wadau kuhusu kuunganisha Mifuko

Mamlaka inaendelea kupokea maoni ya wadau kuhusu namna bora ya kuunganisha Mifuko. Tayari Mamlaka imeshafanya vikao 6 vya wadau kuhusu swala hilo. Mamlaka inaendelea na mikutano ya wadau ili kuhakikisha kwamba maamuzi ya jambo hili pamoja na mengine kama hayo, yanazingatia utaalamu, mapendekezo ya wadau na hivyo kuwa na mfumo wa Hifadhi ya Jamii wenye tija na Manufaa kwa Wanachama na Sekta kwa ujumla.

Takwimu za Sekta kwa kipindi kinachoishia Juni 2015
Wanachama milion 2.1
  • Rasilimali = shilingi Trilioni 8.78 
  • Michango = shilingi Trilioni 1.9 
  • Mafao yaliyolipwa = shilingi Trilioni 1.36 
  • Uwekezaji = shilingi Trilion7.1 
  • Wastaafu = 89, 532 
Deni la pensheni limepungua toka asilimia 58 ya pato la Taifa mwaka 2010 hadi asilimia 25 mwaka 2015.

Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inalipa mafao ya muda mrefu kama vile;- fao la Pensheni ya Uzee, Mirathi na Ulemavu. Kwa upande wa mafao ya muda mfupi Mifuko inalipa mafao ya;- Uzazi, Elimu, Afya, Mazishi na Kuumia kazini pamoja na huduma zingine kama vile Mikopo ya makazi, elimu na mikopo ya kuanza maisha baada ya kuajiriwa.

UMRI WA KUISHI BAADA YA KUSTAAFU

Umri wa kuishi baada ya kustaafu umeongezeka kufikia miaka 20.8 kwa wanaume, na miaka 22.2 kwa wanawake. Hali hii itaendelea kuwa nzuri zaidi kadiri ya miaka 2 inavyoongezeka ambapo kwa kipindi cha miaka 50 ijayo umri wa kuishi baada ya kustaafu kwa wanaume itakuwa miaka 22.9 na wanawake miaka 24.9.

VIWANGO VYA PENSHENI

Pensheni imeboreshwa kutoka wastani wa asilimia 67 hadi asilimia 72.5. Hata hivyo kwa Mifuko inayolipa mkupuo wa asilimia 50 viwango vya pensheni kwa mwezi ni asilimia 27 ya mshahara. Hiki ni kiwango cha chini sana, kiwango kinachotakiwa kimataifa ni asilimia 40.

UIMARA WA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII

Tathmini inaonesha kwamba Mifuko imeimarika. Mifuko inauwezo kwa kustawi hadi kufika mwaka 2085 na 2075 kwa mfuko wa NSSF na PPF. Tathmini inaonesha kwamba Mfuko wa LAPF na GEPF una uwezo wa kufika Zaidi ya mwaka 2058 na 2047. Na iwapo vikokotoo vyao vitarekebishwa Mifuko hii itaweza kufika mwaka 2085. Hali kadhalika iwapo Mfuko wa PSPF utapokea michango ya kabla ya 1999 na kufanya marekebisho yanayopendekezwa kwa GEPF na LAPF Mfuko huu utadumu hadi mwaka 2075. Vilevile Mfuko huu utaimarika iwapo mafao yatarekebishwa au michango kuongezwa hadi kufika asilimia 28 badala ya asilimia 20. Suala hili litategemea zaidi utashi wa wadau.

GHARAMA ZA UENDESHAJI MIFUKO 

Kwa ujumla Mifuko imeonekana kuwa na Gharama kubwa ya uendeshaji. Kuwepo kwa gharama kubwa za uendeshaji kutazorotesha utendaji wa Mifuko. Hivyo kwenye jambo hili Mamlaka imeandaa kanuni za kushusha gharama za uendeshaji. Mifuko yote haitaruhusiwa kuwa na gharama inayozidi asilimia 10 kuanzia July 2016. Sheria zinazoruhusu Mifuko kutumia asilimia 15 zimeingizwa kwenye mchakato wa marekebisho.

KUINGILIANA KWA MAFAO

Tathimini imeonesha kuwa ukiacha Mafao ya muda mrefu, NSSF wanatoa mafao la Bima ya Afya pamoja na Fao la Kuumia Kazini wakati uo huo, Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) hutoa huduma za bima ya afya. Vilevile Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) nayo inashughulisha na fao la kuumia kazini. Mamlaka inashughulikia suala hili ili kupunguza gharama kwa waajiri na kuboresha mafao kwa wanachama.

UWIANO WA WACHANGIAJI NA WASTAAFU

Tathimini inaonesha kuwa kila mfuko upo katika kiwango chake cha ukuaji. Kiwango cha idadi ya wanachama kufikia 1.95 milioni wakati idadi ya wanaopokea pensheni kufikia 97,428. Hii ni uwiano wa wanachama 20 kwa mstaafu mmoja. Hiki ni kiwango kizuri kwa sekta. Hata hivyo Mifuko yenye wastaafu wengi hasa PSPF na PPF inapaswa kuongeza wanachama wake mara dufu.

Hitimisho

Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa ushirikiano mkubwa tunaopata toka kwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu; Wizara ya Fedha na Uchumi; Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Wzee; Benki Kuu ya Tanzania; Vyama vya Wafanyakazi; chama cha Waajiri; vyombo vya habari pamoja na wadau wote kwa ujumla.

Mwisho, Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii inapenda kuwatoa hofu wanachama na wadau wengine wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwamba Sekta ipo imara. Iwapo kuna malalamiko, ushauri au maoni yoyote kuhusiana na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii tafadhali msisite kuwasiliana na Mamlaka ili yapatiwe ufumbuzi mapema iwezekanavyo. 
Toggle Footer
TOP