Taarifa ya Waziri Kivuli kuhusu zoezi la kuwabaini "watumishi hewa" serikalini

Waziri Kivuli Ofisi Ya Rais (Utumishi) na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi wa Upinzani Bungeni, Ruth Hiyob Mollel (Mb) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam leo

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI-KUHUSU WATUMISHI HEWA 05.04.2016

Ndugu waandishi wa habari,

Takriban wiki mbili zilizopita, yaani tarehe 15 Machi, 2016, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. John Pombe Magufuli, aliwaagiza Wakuu wa Mikoa yote ya Tanzania Bara kusimamia zoezi la kuhakiki watumishi wa umma katika Mikoa yao kwa lengo la kubaini wanaoitwa ‘watumishi hewa.’Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, zoezi hili limekwishafanyika na kubaini takriban ‘watumishi hewa’ 1850 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.

Hii sio mara ya kwanza kwa Serikaliya Tanzania kufanya uhakiki wa watumishi wa umma ili kuondoa watumishi hewa. Itakumbukwa kwamba, mwaka 1993 Serikali ilisimamisha kwa muda utaratibu wa kulipa mishahara ya watumishi wa umma kwa kuipitishia kwenye akauntizao benki. Badala yake, Serikali ilihakiki watumishi wa umma kwa kuwalipa mishahara yao kupitia dirishani, yaani malipo ya moja kwa moja kwa watumishi husika. Watumishi ambao hawakujitokeza kuchukua mishahara yao dirishani walihesabika kuwa ni ‘watumishi hewa’ na majina yao yaliondolewa katika ‘payroll.’

Hata hivyo uhakiki huo ulishindwa kuondoa tatizo la ‘watumishi hewa’ambalo liliendelea kuwa sugu katika utumishi waumma.

Uhakiki mwingine wa watumishi wa umma ulifanyika mwaka 2006 na mwaka 2011.Jitihada za Serkali ya awamu ya nnenazo hazikufua dafu. Serikali iliendelea kupoteza mabilioni ya fedha kutokana na malipo ya mishahara na marupurupu ya watumishi hewa.

Aidha, kama sehemu ya jitihada za kuondoa tatizo hili, tangu miaka ya katikati ya tisini, Serikali ilianzisha mfumo wa taarifa za utumishi na malipo ya watumishi wa umma uitwao Lawson. Chini ya mfumo huu, taarifa za watumishi wa umma ambao utumishi wao umekoma kwa sababu yoyote ilezinapoingizwa katika kumbukumbu za mahala pao pa kazi, hupelekwa moja kwa moja Hazina kwa ajili ya hatua zaidi kama vile kuwaondoa katika ‘payroll’ na kuandaa malipo yao ya pensheni, kiinua mgongo, n.k. Kwa sasa mfumo wa Lawson umepelekwa katika mikoa na halmashauri zote za wilaya katika Tanzania Bara. Mfumo huu pia umeshindwa kuondoatatizo la watumishi hewa.

Ndugu waandishi wa habari,

Sababu kubwa ya kushindikana kutatuliwa kwa tatizo la watumishi hewa ni kukosekanakwa uadilifu katika mfumo mzima wa utumishi wa umma. Watumishi hewa ni tatizo la kutengenezwa kwa makusudi. Mabilioni yanayopotea kila mwaka kutokana na malipo ya watumishi hewa yanakwenda kwenye mifuko binafsi ya viongozi na watendaji hao.

Hawa ndio ambao wamehakikisha kuwa jitihada zote za nyuma za kupambana na tatizo hili hazifanikiwi. Na hawa ndio watakaohakikisha kuwa jitihada za sasa za Mhe Rais Magufuli zinakwama. Viongozi na watendaji hawa wa Serikali hawapo katika ngazi za chini za utumishi wa umma wilayani na mikoani peke yake. Wako katika ngazi zote katika mfumo mzima wa utumishi wa umma.

Ndio maana licha ya kelele na jitihada zote, licha ya taarifa rasmi za kila mwaka za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuonyesha ukubwa na upana wa tatizo hili, hakuna kiongozi wala mtendaji wa idara ya Serikali au taasisizake yeyote ambaye amewajibishwa kutokana na idara au taasisi yake kukutwa imelipa mishahara ya watumishi hewa.

Ukweli huu unashuhudiwa hata na jitihada za sasa za Rais Magufuli. Kwa kadri tunavyofahamu, hakuna kiongozi au mtendaji wa Serikali au taasisi wa ngazi yoyote ambaye amewajibishwa kwa sababu ya kuwa na watumishi hewa. Aidha, zoezi la uhakiki limefanywa na wahusika wa tatizo lenyewe. Kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa, Wakuu wa Mikoa ndio wakuu wa utumishi wote wa umma katika mikoa yao.

Aidha, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Serikali za Mitaandio waajiri wa watumishi katika halmashauri zao. Kwa sababu hiyo, Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri wanahusika moja kwa moja na uwepo wa watumishi hewa katika mikoa na katika halmashauri za serikali za mitaa. Na hawa ndio ambao wamepewa jukumu na Rais Magufuli la kuwabaini watumishi hewa katika maeneo yao.

Kwa kutoa taarifa zinazoonyesha uwepo wamaelfu ya watumishi hewa katika mikoa na halmashauri zao, viongozi na watendaji hawa sasa wamejitia hatiani kwa kuonyesha kuhusika kwao na tatizo hili. Tunasubiri kuona hatua zitakazochukuliwa naMhe Rais Magufulidhidi ya Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa halmashauri ambao, kwa makusudi au kwa uzembe wao, wamesababisha kuwepo kwa watumishi hewa katika mikoa na halmashauri zao.

Ndugu waandishi wa habari,

Lipo tatizo la pili ambalo limechangia kuwepo au kukua kwa tatizo la watumishi hewa katika utumishi wa umma. Tatizo hilo ni udhaifu mkubwa wa Tume ya Utumishi wa Umma ambayo ndio Tume Rekebu yenye jukumu la kuhakiki raslimaliwatu katika utumishi wote wa umma. Kwa mujibu wa taarifa rasmi zilizotolewa na Tume hiyo kwa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa hivi karibuni, Tume hiyo inakabiliwa na matatizo makubwa yanayokwamisha utendaji kazi wake.

Kwa mfano, Tume hiyo haina watumishi wa kada mbali mbali, vitendea kazi vya aina mbali mbali kama vile magari, kompyuta na vifaa vingine vya ofisi. Na katika mwaka huu wa fedha, Tume ya Utumishi wa Umma imepatiwa 9.3% ya fedha iliyotengwa kwenye bajeti kwa ajili yake. Katika mazingira haya, Tume hiyo imeshindwa kabisa kutekeleza majukumu ya kuhakiki watumishi wa umma katika maeneo mbali mbali ya nchi yetu.

Tatizo la tatu ambalo limechangia kuwepo au kuongezeka kwa watumishi hewa ni kutokuwepo kwa mfumo mmoja wa rasilmali watu unaojumuisha na kuunganisha mifumo mingine yote. Kwa mfano, kwa utaratibu wa sasa, mfumo wa kusajili uzazi na vifo uliopo chini ya RITA haujaunganishwa na mfumo wa utumishi wa umma wala na mifumo ya hifadhi ya jamii kama vile NSSF, LAPF, PSPF, n.k.

Kwa sababu ya mifumo hiyo kuwa inajitegemea, yaani ‘stand-alone systems’, taarifa zinazoingizwa katika mfumo mmoja hazipelekwi katika mifumo mingine. Kwa mfano, taarifa za vifo zinazotolewa na RITA haziingizwi katika mifumo ya utumishi wa umma wala ya hifadhi ya jamii ili majina ya wahusika yaweze kuondolewa katika ‘payroll’ na orodha za malipo ya pensheni au kiinua mgongo. Matokeo yake ni kuwepo kwa watumishi hewa, yaani watumishi ambao wameshafariki dunia lakini taarifa zao hazijapelekwa kunakohusika na wanaendelea kulipwa mishahara na Serikali.

Kambi ya upinzani inaishauri Serkali kufanya yafuatayo;
  1. Wakurugenzi Watendaji naMakatibu Tawala wa mikoa wanaosababisha watumishi hewa wakati mfumo wa kuwaondoa upo, wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
  2. Tume ya Utumishi wa Umma wapewa watumishi wa kutosha, magari na vitendea kazi ili watekeleze jukumu lao la kuhakiki watumishi wa Umma nakutoa taarifa kwa mamlaka hususika.
  3. Serikali iunganishe mifumo ya rasilmali watu inayojitegemea “Stand alone systems”. Namba ya kitambulisho cha taifa iunganishwe na mfumo wa vizazi na vifo, mfumo wa malipo serkalini, mfumo wa malipo ya pensheni, mfumo wa mlipa kodi nk. Hivyo mtumishi anapofariki, kustaafu au kuacha kazi mfumo wa Lawson nilioutaja hapo juu unamwondoa mara moja katika orodha ya watumishi wa Serkali.
Ndugu wanahabari, Serkali ikizingatia mapendekezo hayo, watumishi hewa itakuwa ni historia katika nchini na fedha zinazopotea kwa sasa zitatumika kwa miradi ya maendeleo. Kupanga ni kuchagua.

Mungu ibariki Tanzania.

RUTH HIYOB MOLLEL (MB.)

WAZIRI KIVULI & MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI)