Taarifa ya Wizara ya Aprili 4, 2016 kuhusu hali ya ugonjwa wa kipindupindu

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO


TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 4 APRILI, 2016

Ndugu wanahabari,

Kila wiki serikali kupitia Wizara yangu imekuwa ikitoa taarifa ya mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu na hatua zinazochukuliwa kudhibiti ugonjwa huu. Aidha pia kila mwisho wa mwezi, majumusiho hufanyika na kutolewa taarifa. Hadi kufikia tarehe 4 April 2016, jumla ya wagonjwa 20,294 wametolewa taarifa, na kati ya hao 320 wamepoteza maisha

Kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka, mwenendo wa Kipindupindu unaashiria kuwa idadi ya wagonjwa inaongezeka nchini. Mwezi Januari kulikuwa na wagonjwa 2,272, na mwezi Machi kulikuwa na wagonjwa 2,956. Hili ni ongezeko la asilimia 30.1%. Hata hivyo, baadhi ya mikoa imeonyesha uendelevu wa kupungua kwa idadi ya wagojwa wa Kipindupindu kwa robo ya kwanza. Mikoa hiyo ni pamoja na Simiyu, Rukwa na Mbeya. Takwimu hizi za nchi nzima zinaashiria kuwa juhudi za kupambana na ugonjwa wa Kipindupindu zinahitaji kutekelezwa na kusimamiwa kikamilifu na mikoa na wilaya zote nchini baada ya Wizara yangu kutoa maelekezo na miongozo stahili. Vile vile, napenda kusisitiza kwamba hata Mikoa ambayo haina wagonjwa ni lazima wachukue hatua za tahadhari kuzuia maambukizi mapya, na ile mikoa ambayo ina wagonjwa iendelee kusimamia kikamilifu udhibiti wa mlipuko.

Katika mwezi Machi, jumla ya wagonjwa wapya walioripotiwa nchi nzima walikuwa 2,956, na vifo vilikuwa 53. Takwimu za mwezi Machi (tarehe 5 Machi hadi 3 Aprili) zinaonyesha idadi ya wagonjwa imeongezeka kwa asililmia 59.5% ikilinganishwa na idadi ya wagonjwa wa mwezi Februari (1,853). Mikoa ya Tanga, Pwani na Mtwara haikuwa imeriporti wagonjwa mwezi wa Februari lakini mwezi huu wa Machi imepata wagonjwa wapya. Aidha katika kipindi hiki cha mwezi mmoja kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wapya kwenye mikoa ya Geita, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, na Dodoma. Idadi ya wagonjwa kutoka mikoa ya Simiyu, Mbeya na Iringa imepungua kati ya Februari na Machi 2016.

Kwa upande wa takwimu za kila wiki (weekly report), idadi ya wagonjwa wa Kipindupindu walioripotiwa kwa wiki ya kati ya tarehe 28 Machi hadi 3 Aprili 2016 imepungua kwa asilimia 37.2 ikilinganishwa na idadi ya wagonjwa walioripotiwa kati ya tarehe 21 hadi 27 Machi 2016. Kwa wiki hii ya tarehe 28 Machi hadi 3 Aprili 2016 kulikuwa na jumla ya wagonjwa wapya 430 na vifo saba (7). Idadi ya vifo kwa wiki hii imeongezeka kutoka vifo vinne vilivyoripotiwa katika wiki iliyopita. Kwa wiki hii mikoa iliyopata wagonjwa wengi zaidi ni Kilimanjaro (128), Mara (102), Morogoro (67), Geita (46), Mwanza (40) na Dar es Salaam (31). Halmashauri kumi zilizoongoza kwa idadi ya wagonjwa wapya wiki hii ni Same (74), Tarime Vijijini (52), Moshi Vijijini (44), Mvomero (27), Rorya (26), Ilemela (25), Korogwe Mjini (25), Morogoro Vijijini (25), Chato (24) na Tarime Mjini (20). Ugonjwa wa Kipindupindu hadi sasa haujaripotiwa kutoka mikoa ya Njombe na Ruvuma. 

Ndugu wanahabari,

Wizara inapenda kutoa pongezi kwa Mikoa na Wilaya zinazoendelea kutoa taarifa sahihi na kwa wakati pamoja na juhudi za kudhibiti ugonjwa huu. Ninaendelea kusisitiza kuwa ni lazima kwa Mikoa na Wilaya kutoa taarifa ya wagonjwa wapya wa Kipindupindu kwa kuzingatia mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa ujulikanao kama “Integrated Disease Surveillance and Response (IDSR)”, ambao unasimamiwa na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Utoaji wa taarifa sahihi na kamili (ikiwa pamoja na linelists) kwa wakati utasaidia kuweka mikakati ya upesi ya kudhibiti ugonjwa huu usisambae kwa kasi na kuleta madhara zaidi.

Ndugu wanahabari,

Wizara inasisitiza kuwa kwa wakati huu wa masika, uwezekano wa kuongezeka kwa ugonjwa wa Kipindupindu ni mkubwa, hivyo ni lazima wananchi wazingatie kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira. Kama tunavyoelekeza mara kwa mara, ni marufuku kwa watu kutitirisha maji taka ovyo, na pale hilo litakapofanyika basi hatua za kisheria zitachukuliwa. Aidha tunawasihi viongozi mbalimbali wa ngazi zote; za vitongoji, vijiji, kata na tarafa kusimamia kikamilifu sheria ya Afya ya Mazingira hususan wakati huu wa mvua za Masika. Tukumbuke kwamba kipindupindu kinahitaji juhudi kubwa zifanywe na wananchi na viongozi wa ngazi mbalimbali, hivyo tushirikiane kuhakikisha tunaepuka kuchafua vyanzo vya maji. Aidha, Serikali kupitia Wizara yangu na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea na juhudi za kutoa miongozo, maelekezo na ufuatiliaji juhudi za kudhibiti ugonjwa huu likiwemo zoezi la ugawaji wa dawa kwa ajili ya kutakasa maji (Chlorine tablets, mfano waterguard) katika mikoa iliyoathiriwa zaidi na Kipindupindu.

Ndugu wanahabari,

Nahimiza yafuatayo yazingatiwe katika kudhibiti magonjwa ya milipuko;
  1. Utoaji wa taarifa mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya pale wanapoona wagonjwa wana dalili za magonjwa ya milipuko.
  2. Kutilia mkazo usafi wa mazingira kwa ujumla kama Ofisi ya Rais – TAMISEMI inavyoelekeza. Kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, ni budi tushirikiane katika kufanya usafi wa mazingira kwani hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti ugonjwa huu.
  3. Watumishi wa afya waendeelee kutoa tiba kwa wagonjwa wa Kipindupindu kwa uadilifu na kwa kuzingatia miongozo inayotolewa. Aidha waendelee kutoa elimu kwa wananchi ya kujiepusha kupata maambukizi.
  4. Juhudi za udhibiti wa kipindupindu zifanyike kwa ushirikishwaji wa karibu wa viongozi wa kijamii, hususan viongozi wa kidini na wa kimila
  5. Viongozi na Watendaji katika ngazi mbalimbali waendelee kuchukua tahadhari (Preparedness) kwa magonjwa haya na mengine yatokanayo na Mvua za Masika.
  6. Wamiliki wote wa vyombo vya usafiri wanaagizwa kutoa taarifa mara moja kwenye kituo cha afya kilichopo karibu pindi umuonapo abiria anayetapika au kuharisha.
Hitimisho

Wizara inaendelea kutoa wito kwa wadau wote katika ngazi zote kushirikiana kwa pamoja katika jitihada za kutokomeza ugonjwa wa Kipindupindu. Aidha, Wizara inaendelea kuwashukuru wataalamu wa sekta husika, Mashirika ya Kimataifa, Watumishi, Mikoa na Halmashauri pamoja na waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kwa kuendelea kushirikiana katika suala zima la kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu.