Uamuzi wa TFF wa kuzishusha madaraja timu 4 zilizopanga matokeo
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Kamati yake ya Nidhamu hatimaye imemaliza kesi iliyochukua takribani wiki tatu ya kupata uamuzi dhidi ya madai ya mechi za ligi daraja la kwanza, kwa kuzishusha daraja timu zote zilizotuhumiwa (Geita Gold, Polisi Tabora, JKT Kanembwa na JKT Oljoro) baada ya kuzikuta na hatia ya kupanga matokeo katika mechi za mwisho za Ligi Daraja la Kwanza Bara.

Maamuzi hayo yaliyotangazwa leo na makamu mwenyekiti wa kamati hiyo Wakili Jerome Msemwa yamezishusha JKT Kanembwa iliyoshushwa hadi Ligi ya Mkoa, wakati Geita, Polisi Tabora na JKT Oljoro zimeshushwa hadi Daraja la Pili.

Msemwa amesema aliyekuwa kipa wa Simba ambaye anaitumikia kwa mkopo Geita, Dennis Richard amefungiwa miaka 10 kujihusisha na soka pamoja na faini ya Sh. Milioni 10 baada ya kushikwa na hatia kuwa katika mpango wa upangaji matokeo adhabu ambayo pia imemkumba kipa wa JKT Kanembwa Mohamed Mohamed.

Naye kocha msaidizi wa Geita, Choki Abeid ameshushiwa rungu la adhabu kali kwa kufungiwa maisha baada ya kushikwa na hatia na kamati hiyo.

“Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Geita (GEREFA), Salum Kurunge, Mwenyekiti wa klabu ya Geita Gold, Cosntantine Moladi na Katibu wa klabu ya JKT Kanembwa Basil Matei wameachiwa huru na Kamati ya Nidhamu baada ya kutokutwa na hatia katika shauri hilo,” alisema Msemwa.

Aidha Msemwa amesema Wengine waliofungiwa miaka 10 na faini ya Sh. Milioni 10 ni Refa na refa wa akiba wa mechi kati ya Polisi na Oljoro ambazo nazo zilishikwa na hatia mbalimbali kutokana na maelezo waliyoyatoa kwa kamati yake.

Refa wa mchezo kati ya Kanembwa na Geita Gold, naye amefungiwa maisha sawa na Kamisaa wa mchezo huo na Kocha Msaidizi wa Geita, Mwenyekiti Yussuf Kitumbo na Katibu, Alex Kataya wa Chama cha Soka Tabora (TAREFA), Kocha msaidizi Polisi Tabora na Mwenyekiti Oljoro.

Kwa upande wa Katibu wa klabu ya Polisi Tabora, Alex Kataya, Katibu wa klabu ya JKT Oljoro, Hussein Nalinja, mtunza vifaa wa klabu ya Polisi Tabora, Boniface Komba, na Meneja wa timu ya Polisi Tabora, Mrisho Seleman, wameachiwa huru na Kamati ya Nidhamu ya baada ya kutokutwa na hatia.

Hata hivyo Kamati hiyo imefungua milango kwa wahukumiwa kukata rufaa endapo watabaini maamuzi hayo hayakuwatendea haki ambapo sasa kwa mujibu wa matokeo hayo ni wazi kwa mujibu wa kanuni Mbao FC ya Mwanza iliyomaliza nafasi ya nne ndiyo inayoweza kuchukua nafasi ya kupanda Ligi Kuu.