Loading...
Monday

Waziri apendekeza kuondoa VAT kwa nyumba za NHC zinazouzwa chini ya milioni 40/=

Wizara ya Ardhi imependekeza kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), kwa nyumba zisizozidi Sh40 milioni zinazouzwa na taasisi za umma.

Waziri wa Ardhi, William Lukuvi aliieleza Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuwa ameshapeleka pendekezo kwa Baraza la Mawaziri kuondoa kodi hiyo kwenye nyumba zinazouzwa na Shirika la Nyumba (NHC) na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) iwapo zitauzwa kwa gharama isiyozidi Sh40 milioni ili kuwapatia wananchi unafuu.

“Nilipowauliza wataalamu wangu kikomo cha nyumba ya bei nafuu ni shilingi ngapi, walinitajia Sh49.9 milioni, lakini niliona haiwezekani. Ndiyo maana nilipendekeza serikalini VAT iondolewe kwenye nyumba zisizozidi Sh40 milioni,” alisema Lukuvi. 

Wajumbe wa kamati hiyo kwa umoja pia waliikomalia wizara hiyo kuisimamisha kwa muda Mamlaka ya maendeleo ya mji wa Kigamboni (KDA), kwa sababu haipatiwi fedha za kutosha na mradi husika unasuasua.

Lukuvi aliomba kupatiwa Sh61.83 bilioni katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo, ikiwa ni ongezeko la Sh7.2 bilioni kutoka kwenye bajeti ya mwaka 2015/2016.

Aliwaambia wajumbe wa kamati hiyo kuwa kati ya Sh61.83 wanazohitaji, Sh16.35 bilioni zitatumika kulipa mishahara ya watumishi wa wizara hiyo. Wizara hiyo inaomba kutumia Sh25.48 bilioni kutoka katika fungu hilo kwa ajili ya matumizi mengineyo, ambayo yanajumuisha Sh10 bilioni za kuziwezesha halmashauri kusimamia upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Atashasta Nditiye alisema baada ya kusikiliza mapendekezo hayo wataanza kuijadili leo kwa kina kuona iwapo ni halisi au la.
 
Toggle Footer
TOP