Loading...
Tuesday

WM Majaliwa uhakiki wa CAG wabaini madeni hovyo na ya mashaka ya watumishi kwa serikaliJAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA WAZIRI MKUU

WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amesema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), anafanya uhakiki wa madeni yanayodaiwa serikali na watumishi na kubaini madudu.

Amesema madai mengine yameonyesha mashaka ambapo amewataka wakurugenzi wa Halmashauri na Wakaguzi wakuu wa ndani kujiridhisha ukweli wa madai hayo kabla ya kuyafikisha serikalini kwa ajili ya malipo.
“Madai mengine yanatia mashaka, sisi hatuhitaji kuletewa madeni ya hovyo hovyo ni vyema Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakaguzi wa ndani wakajiridhisha kabla kuyapeleka serikalini kwa ajili ya malipo. Madeni mengine ya ajabu, mfano unakuta mtumishi mmoja anaidai serikali sh. milioni 30, jambo ambalo ni gumu hata kama alihamishwa haiwezekani kufikia kiwango hicho, pia kuna baadhi ya majina yamejirudia mara nne,” amesema.
Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa alipotembelea Hospitali hiyo wakati akiwa katika ziara ya kikazi iliyolenga kukabidhi msaada wa vifaa tiba alivyovitoa kwa ajili ya hospitali hiyo .

Amesema kuwa serikali italipa madeni yote inayodaiwa baada ya kumaliza kuyafanyia uhakiki, hivyo aliwaomba watumishi kuwa na subira wakati serikali ikiendelea zoezi la kuyahakiki ili kuweza kulipa deni sahihi inalodaiwa.

Awali akisoma taarifa ya Idara ya afya kwa Waziri Mkuu, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Dk. Japhet Simeo amesema idara ya afya inakabiliwa na madeni ya watumishi ambayo ni sh. milioni 109,662,483.

Amesema madeni hayo yametokana na likizo, matibabu, uhamisho wa ndani na nje ya wilaya, gharama za mizigo kwa watumishi waliostaafu, ambapo halmashauri imejipangia utaratibu wa kulipa madeni hayo pindi inapotokea fedha kutoka serikali kuu.

Hata hivyo kasi ya mtiririko wa fedha ni ndogo ukilinganisha na mahitaji halisi ya maslahi ya watumishi ambapo Halmashauri inawapongeza na kuwapongeza watumishi wa Idara ya afya kwa kuendelea kuwa wavumilivu na kuwahudumia wananchi.

Dk. Simeo amesema halmashauri inawapongeza Rais Dk. John Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa kwa juhudi kubwa wanazozifanya kuongeza mapato nchini, ambapo wana matumaini kuwa watumishi wataboreshewa maslahi na stahiki zao ili kuchochea motisha kiutendaji.

Katika hatua nyingine Dk. Simeo alizungumzia upatikanaji wa dawa, alisema ambao umeongezeka kutoka asilimia 30 mwaka jana na kufikia asilimia 80 mwaka huu dawa muhimu katika vituo vyote vya kutolea huduma ambavyo viko 32.

Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa akizungumza baada ya kukabidhi msaada wa shuka kwa wazazi wanaosubiri kujifungua na waliojifungua kwenye hospitali ya wilaya ya Ruangwa Aprili 11, 2016. Kushoto ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na wapili kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa mkoa Lindi, Mzee Mtopa.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA WAZIRI MKUU

MKE WA WAZIRI MKUU ATOA MSAADA WA MASHUKA KWA AKINAMAMA WALIOJIFUNGUA

MKE wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa amefanya ziara katika Hospitali ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi na kutoa msaada wa mashuka kwa akinamama waliojifungua.

Pia ametumia fursa hiyo kuwapongeza madaktari na wauguzi wa Hospitali ya wilaya ya Ruangwa kutokana na kuwahudumia vizuri wananchi na kuwaomba waendelee kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa maadili ya kazi yao.

Mke wa Waziri Mkuu ameyasema hayo jana wakati alipotembelea wodi ya akinamama waliotoka kujifungua na kufurahishwa na hali ya utoaji huduma hospitalini hapo, ambapo aliwasisitiza kuendelea moyo huo kwa sababu wao ndio wamebeba dhamana ya afya za wananchi.
“Nimefurahi kukuta wazazi wanahudumiwa vizuri na wenyewe wamekiri kwamba huduma zinazotolewa hospitalini hapa ni za kuridhisha, tofauti na tulivyozoea kusikia wagonjwa wakiwalalamikia wauguzi, hivyo ni jambo la kujivunia, hongereni sana” amesema.
Mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika wodi hiyo Hamisa Rashid ambaye amelazwa katika wodi hiyo amesema alifikishwa hospitalini hapo wiki mbili zilizopita akiwa katika hali mbaya na ameweza kuhudumiwa vizuri na sasa anakaribia kutoka.
“Mimi nilikuwa sijitambui, siwezi kufanya kitu chochote lakini baada ya kuletwa hospitalini hapa madaktari kwa kushirikiana na wauguzi wamenihudumia vizuri na sasa naweza hata kwenda chooni mwenyewe na bila msaada wao mimi ningekuwa nimepoteza maisha kutokana na hali yangu ilivyokuwa,” amesema Hamisa.
Mbali na kutoa msaada huo wa mashuka pia ametoa baiskeli mbili kwa ajili ya wanawake wawili walemavu lengo likiwa ni kuwawezesha kufanya shughuli zao za kijamii kwa urahisi.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Rehema Omary amemshukuru mke wa Waziri Mkuu kwa msaada huo, ambapo alimuomba Waziri Mkuu, Majaliwa awawezeshe kwenda kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na walemavu ikiwemo michezo.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amewataka watumishi wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuachana na utendaji kazi wa mazoea kwa sababu umepitwa na wakati.

Pia amesema amefurahishwa na kitendo cha wagonjwa kukiri kuwa wanahudumiwa vizuri tofauti na hospitali zingine hivyo kuwataka kuendelea na ari hiyo ya kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi mkubwa.

Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea soko kuu la mji wa Ruangwa kukagua hali ya chakula na bei zake Aprili 11, 2016. Alikuwa katika ziara ya jimbo lake la uchaguzi la Ruangwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na mabingwa wa soka wa mkoa wa Lindi , timu ya Namungo FC ya Ruangwa baada ya kukabidhiwa kombe la ubingwa huo na kuzungumza nao kwenye uwanja wa michezo wa Ruangwa akiwa katika ziara ya jimbo lake la uchaguzi, Aprili 11, 2016.
Wanawake wa Ruangwa wakimshangilia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakti alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Chama cha Walimu mjini Ruangwa Aprili 11, 2016.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA WAZIRI MKUU

Duka la dawa lajengwa katika ndani ya Hospitali ya wilaya ya Ruangwa

WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa duka la dawa katika hospitali ya wilaya ya Ruangwa ambalo litatoa fursa kwa wilaya nyingine kama Kilwa, Nachingwea na Liwale kufuata dawa katika duka hilo.

Ujenzi wa duka hilo la dawa ndani ya wilaya ya Ruangwa umefadhiliwa na Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) na unakadiriwa kugharimu sh milioni 55 mpaka kukamilika kwake ambapo kutasaidia kuboresha upatikanaji wa dawa hospitalini hapo na katika hospitali zingine zilizoko katika wilaya za jirani.

Waziri Mkuu, Majaliwa amesema mbali na ujenzi wa duka la dawa pia hospitali hiyo inatarajiwa kujengewa uzio ili kuepusha vitendo vya uhalifu vinavyoweza kutokea kutokana na hospitali hiyo kukosa uzio.

Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa duka la dawa katika Hospitali hiyo.
“Nataka hapa ndio iwe bohari ya dawa, watu kutoka Kilwa, Nachingwea na Liwale wawe wanafuata dawa na vifaa tiba katika duka la dawa lililoko ndani ya Hospitali ya wilaya ya Ruangwa, pia kujengwa kwa duka hili kutasaidia kumaliza tatizo la upungufu wa dawa,” amesema.
Amesema mkakati uliokuwepo ni kuhakikisha vifaa tiba na dawa vinapatikana hospitalini hapo ili kuwawezesha wagonjwa kupata huduma bora.

“Kinachomuuma ni kuona akinamama, akinababa, vijana na wazee wangu wanakwenda hospitali na kuambiwa vipimo hakuna, hivyo nitahakikisha ifaa tiba vyote vinapatikana,”.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa HHalmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Dk. Japhet Simeo amemshukuru Waziri Mkuu kwa juhudi mbalimbali anazozifanya ikiwemo kutafuta wafadhili mbalimbali wanaoendelea kusaidia utoaji wa huduma za afya hospitalini hapa.
“Mpaka sasa kuna mradi wa ujenzi wa uzio wa hospitali ya wilaya, ujenzi wa duka la dawa, ukarabati wa majengo na upanuzi wa hospitali na tunamuomba aendelee kuwashirikisha wadau mbalimbali katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali yetu ya wilaya,” amesema.
Dk. Simeo ameongeza kuwa kwa kupitia Waziri Mkuu, Majaliwa wameweza kupata vifaa tiba mbalimbali vyenye thamani ya zaidi y ash. Milioni 100 kutoka umoja wa kampuni unaotengeneza vinywaji baridi nchini ambavyo jana walikabidhiwa na Meneja wa MSD, kanda ya Mtwara, Helman Mng’ong’o.

Amesema licha ya kupata vifaa hivyo, pia walipokea vifaa tiba kutoka shirika la VSO vyenye thamani ya sh. milioni 32 ambavyo vitatumika katika kusaidia watoto waliozaliwa kabla umri haujatimia.

Dk. Simeo alitaja vifaa tiba hivyo kuwa ni ni mashine ya kusaidia kupumua, mashine ya kusaidia kuhifadhi joto la mototo, mashine nyingine ni za kusafishia watoto waliopaliwa na mashine ya kusaidia kujua kiwango cha hewa ya oxygen ndani ya mishipa ya damu ya watoto hao.

Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na wanwake wa Ruangwa baada ya kuzungumza nao kwenye ukumbi wa Chama cha Walimu mjini Ruangwa Aprili 11, 2016.

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP