Loading...
Monday

Baraza la Madiwani jijini la Dar yabatilisha uuzwaji wa hisa za UDA

Wajumbe wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wamebatilisha uuzwaji wa hisa za halmashauri ya jiji, asilimia 51 ya hisa zilizopo katika shirika la Usafirishaji la Jiji la Dar es Salaam (UDA) na kuzirejesha kwenye Mamlaka ya jiji hilo kutoka kwa mmiliki wa sasa hisa hizo, Kampuni ya Simon Group Limited (SGL), baada ya kubaini kuwa mnunuzi wa hisa hizo ambaye ni kampuni ya SGL, hakufuata taratibu katika mchakato wa kuzinunua na kubainika kuwepo kwa udanganyifu mkubwa katika umiliki wake.

Akitangaza mbele ya wanahabari jijini Dar, Mstahiki Meya wa Jiji hilo, Isaya Mwita amesema hakuna kumbukumbu zozote zinazoonesha kuwa mwanahisa mwenza wa Halmashauri ya Jiji katika UDA, yaani Msajili wa Hazina aliridhia Halmashauri ya Jiji kuuza hisa kwa mtu mwingine. 

Hapo awali, Halmashauri ya Jiji ilikuwa inamilikia asilimia 49 ya hisa huku Kampuni ya Simon Group Limited ikimiliki asilimia 51,

“Sisi kama Jiji tumeona ni busara. Hazina hawafanyi biashara, serikali haifanyi biashara, kazi yake ni kukusanya kodi. Wanaweza kuamua kwa makusudi wakachukua zile hisa 49 ili kuondoa mgogoro huo ambao hauna tija, wakamkabidhi Simon Groups halafu sisi tukabaki na hisa zetu 51 tukaendelea kuwahudumia Wanadaresalam. Ni hatari sana kama shirika, sisi tukajiondoa wakati huo wakati sisi ndiyo tunaosimamia shughuli za usafirishaji jijini Dar es Salaam, ”amesema Mwita.

Mwita ambaye pia nia Diwani wa Kata ya Vijipweni kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema hisa hizo pia ziliiuzwa bila ya kuzingatia sheria ya Manunuzi ya Umma (Public Procurement Act) kutokana na Kampuni ya SGL kutokuwa mwanahisa katika ununuzi wa hisa zisizogawiwa (unallocated shares) jambo analodai ndiyo sababu hisa hizo zilirudishwa, na sasa wanashangaa tena kampuni hiyo kuzipewa.

Sanjari na makosa hayo, pia Mwita ambaye ni meya anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa kutetea katiba ya Wananchi (UKAWA) ameendelea kutaja makosa yaliyofanywa katika uuzaji huo ni hatua ya kutofanyika kwa uthamini wa mali za shirika la UDA kabla ya kuuzwa shirika hilo.

Amesema baada ya Baraza la Madiwani kubaini upungufu huo wajumbe hao waliazimia kuwa fedha zilizolipwa kwa Halmashauri ya jiji na Kampuni ya SGL kwa ajili ya kununua shirika hilo zisirudishwe mpaka pale tathimini itakapofanyika na kujiridhisha kuwa kampuni ya Simon haidaiwi kitu baada ya kubainika kuwa kampuni ya SGL ilitumia mali za UDA kujinufaisha.

Madiwani hao waliridhuia pendekezo la kuundwa kwa kamati ndogo ili ifanye kazi ya uchunguzi wa kina kuhususiana na ubatilishaji wa uuzwaji hisa za Halmashauri ya jiji.

Mwita amewataja wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni Halima Mdee ambaye ni Mbunge wa Kawe, Abdallah Mtolea ambaye ni mbunge wa Kinondoni pamoja na Jummane Mtinangi ambaye ni Mwanasheria wa Jiji.

Mwenyekiti wa Simon Grops Limited, Simon Kisena ameiambia TBC kuwa atatolea ufafanuzi suala hilo mbele ya wanahabari wakati mwingine.
 
Toggle Footer
TOP