Loading...
Friday

Gazeti la Raia Mwema la Mei 18, 2016 lilichapisha, "Magufuli awatisha mawaziri wawili"

RAIS Dk. John Magufuli ameonyesha kukerwa zaidi na utendaji kazi wa mawaziri wawili kiasi cha kuwafokea katika kikao maalumu cha mawaziri cha hivi karibuni, Raia Mwema, limeelezwa.
Mawaziri hao ambao katika utawala wa awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete walikuwa katika wadhifa wa naibu mawaziri, walijikuta katika mtihani huo mbele ya mawaziri wenzao wengine kadhaa waliobaki vinywa wazi.

Vyanzo vya kuaminika vya gazeti hili vimeeleza kuwa Rais Magufuli anataka mawaziri wake wawe mfano wa utendaji bora kwa watumishi wote wa serikali na kwamba, kwa sasa kuna mawaziri, mbali na hao wawili aliowafokea, ambao anaona hawaendi na kasi yake.

“Ni mazingira ambayo mawaziri hawakuyazoea kwamba Rais anawaambia moja kwa moja kwa majina, anafoka akisema anaweza kuwafukuza wakati wowote….mawaziri wamezoea mara kwa mara wanapofanya uzembe au makosa wanaonywa kwa staili tofauti ni kama ya kistaarabu hivi. Sasa huyu bwana mkubwa hana mchezo, aliwataja kabisa,” kinaeleza chanzo chetu cha habari ambacho licha ya kututajia majina ya mawaziri hao, hatutaweza kuwataja hapa moja kwa moja kwa sasa.

Mawaziri hao ambao ni wabunge wa kuchaguliwa majimboni kwa upande wa Tanzania Bara wanaongoza wizara nyeti ambazo zinasimamia sekta mtambuka, wizara ambazo zinagusa sehemu ya ahadi za mabadiliko alizonadi Magufuli wakati akigombea urais katika kampeni za mwaka jana.
Raia Mwema halijaweza kufahamu kwa kina makosa ya kiutendaji yaliyomsababisha Magufuli kuwatisha mawaziri hao na wengine ambao wanaonekana kutomridhisha mpaka sasa.

Chanzo chetu cha habari kinamnukuu Rais Magufuli katika sauti yake ya kufoka akisema; “Wewe (anataja jina la waziri) na mwenzako (anamtaja jina pia) nitawatumbua.” Magufuli aliteua baraza lake la kwanza la mawaziri Desemba mwaka jana katika staili ya aina yake, ambapo baadhi ya wizara zilikosa mawaziri licha ya majina ya wizara hizo kutajwa hadharani, sambamba na naibu mawaziri wake.

“Magufuli anataka atoe mfano kwa mawaziri wengine kwamba wao si watu maalumu sana. Kama wanavyotumbuliwa wengine, nao pia wanaweza kutumbuliwa,” kilifafanua chanzo chetu cha habari.
Miongoni mwa wizara ambazo ziliachwa viporo bila kuwa na mawaziri katika uteuzi huo wa kwanza kwa maelezo kuwa “hawajapatikana/wanatafutwa”, ambazo hata hivyo, mawaziri wake si sehemu ya mawaaziri waliofokewa na Rais Magufuli ni pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango ambayo waziri wake ni Dk. Philip Mpango; Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi inayoongozwa na Profesa Joyce Ndalichako; Wizara ya Maliasili na Utalii inayoongozwa na Profesa Jumanne Maghembe na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inayoongozwa na Profesa Makame Mbarawa.

Tangu aingie madarakani Rais Magufuli, baadhi ya viongozi wanamwelezea mkuu huyo wa nchi kuwa ni msema kweli, asiyetaka unafiki na kwamba pale unapokosea anaweka wazi na hata kama unapofanya vizuri si “mchoyo” wa kupongeza, na moja ya mifano inayotolewa inamhusu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, ambaye Februari mwaka huu, alipongezwa na Rais Magufuli kwa uchapa kazi.

Katika kumpongeza, Rais Magufuli aliweka bayana mbele ya hadhira iliyohudhuria mazungumzo kati yake na wazee wa Jiji la Dar es Salaam kwamba; Makonda anafanya kazi nzuri na isishangaze watu kama atapanda cheo na katika kutekeleza kauli yake hiyo, mwezi mmoja baadaye, yaani Machi mwaka huu, alimteua Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“…Unaweza kuona namna Magufuli anavyotaka mambo yanyooke. Ukifanya kazi atakupongeza kwa moyo wote lakini ukivuruga…hana mchezo na wewe, anakutumbua tu,” alisema mmoja wa viongozi waandamizi serikalini (jina linahifadhiwa).

Mmoja wa viongozi maarufu kukutwa na hasira ya Magufuli ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango-Malecela, ambaye aliondolewa kwenye wadhifa huo baada ya kutoa taarifa zisizo za kweli kuhusu suala la watumishi hewa walioko serikalini.

Kilango ambaye alikuwa ameteuliwa na Magufuli kushika wadhifa huo katika kipindi cha mwezi mmoja tu kabla ya kutumbuliwa, alikuwa amesema kwamba mkoa wake hauna wafanyakazi hewa; jambo lililokuja kubainika baadaye kuwa halikuwa la kweli.

Hata hivyo, tayari wapo mawaziri wengine kadhaa walioonja adha ya kasi ya Magufuli. Mawaziri hao walikumbana na adha hiyo baada ya kushindwa kuwasilisha fomu za tamko la rasilimali na madeni na kuziwasilisha katika Ofisi za Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Kwa agizo la Magufuli, Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa aliwataja hadharani kwa majina mawaziri hao na kuwataka kuwasilisha fomu hizo ndani siku moja, Februari 26, 2016, saa 10 jioni.
“Mheshimiwa Rais ameelekeza mawaziri ambao hawajajaza tamko la rasilimali au hati ya ahadi ya uadilifu wafanye hivyo na kuzirejesha kabla saa 12 jioni na Waziri ambaye atashindwa kutekeleza agizo hili atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye nafasi yake,” alisisitiza Waziri Mkuu katika tamko lake hilo.

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP