Loading...
Sunday

Haya! Kashfa ya mkataba wa Ranch ya Taifa

Mkataba usio na masilahi kwa Taifa ulioandaliwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kuipa kampuni ya Overland Livestock Multiplication & Embryo Transfer umiliki wa Ranchi ya Mzeri iliyoko Tanga umetiwa saini licha ya mamlaka za kisheria kuukataa.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru ambaye ni msimamizi wa mashirika yaliyokuwa chini ya Shirika Hodhi la Taifa (CHC), walishauri mkataba huo ufanyiwe marekebisho ili uwe na masilahi kwa Taifa, lakini katika mazingira tata ulitiwa saini na kampuni hiyo ikapewa umiliki kwa miaka 66.

Novemba mwaka jana, Narco na Overland walianzisha kampuni ya kuendesha ranchi hiyo iitwayo Ovenco Ranches Limited. Narco imetoa ardhi yenye ukubwa wa hekta 20,000 sawa na asilimia 30 ya hisa huku Overland ikichangia mtaji wa Dola 15 milioni za Marekani (Sh3.2 bilioni), mifugo, mashine pamoja na vifaa mbalimbali vyote vikiwa sawa na asilimia 70 ya hisa.

Katika tovuti yake, kampuni hiyo inaonyesha imejipanga kuzalisha mitamba ya ng’ombe wa nyama na wa maziwa 7,000 wenye sifa za kijenetiki ili kusaidia sekta ya mifugo nchini.

“ORL inatarajia kuzalisha mitamba kwa kutumia njia za kawaida na teknolojia za juu kama vile In-vitro Production Embryo Transfer (IVP-ET),” inaeleza tovuti hiyo.

Kampuni ya Overland kutoka Australia inafanya kazi kwa kushirikiana na Kampuni ya Animal Breeding Services (ABS) ya New Zealand.

Mafuru alipoulizwa kuhusu utaratibu uliotumika kuibinafsisha ranchi hiyo alisema anaufahamu mkataba huo lakini aliukataa kwa vile ulikuwa na vipengele visivyoeleweka.

“Huo mkataba uliletwa kwetu lakini tukagundua hauna masilahi kwa Taifa tukawarudishia waurekebishe na hawajarudi mpaka leo. Ulikuwa na vipengele vingi havieleweki. Sasa kama wanaendelea na kazi, watapambana na vyombo vya dola, mimi kama Msajili wa Hazina kazi yangu ni kuhakikisha mkataba uko sawa.”

Masaju alipoulizwa kuhusu mkataba huo alisema: “Tulishauri kama sheria inavyotaka, kwa hiyo hao waliopewa ushauri walifuata au hawakufuata ndiyo waulizwe. Waulizeni kama waliufuata ushauri wangu au hawakufuata.”

Meneja Mkuu wa Miradi wa Ovenco Ranches Ltd, Dk Sharif Hamad alipotafutwa alisema hana nafasi ya kuzungumzia suala hilo, lakini Mwenyekiti Mtendaji wa Ovenco, Faisal Awadh alisema kama kuna matatizo kwenye mkataba, Msajili wa Hazina awaondoe kwenye uwekezaji huo.

“Hakuna mgogoro wowote, hakuna shida kwenye mkataba na kazi inaendelea kama kawaida. Ila kama wao wamekwambia kuna mgogoro ungewauliza mgogoro wa aina gani. Kuna mashamba ya ranchi 129, hakuna hata mwekezaji mmoja aliyejitokeza kuwekeza, ni sisi tu tumejitokeza. Hiyo migogoro wanayotaka kuianzisha sisi haitusumbui. Mwambie Msajili wa Hazina, kama anaona huo mkataba umeingiwa kimakosa, sisi tunaondoka… Watu wengi wamewekeza kwenye biashara hiyo wameshindwa wameondoka.”

Awadh alisema, mazingira ya uwekezaji kwenye mifugo kwa Tanzania ni magumu kiasi kwamba wawekezaji wengi wanaondoka lakini wao wamebaki wakivumilia.

“Mkataba umepita kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mara mbili na umerekebishwa na alitoa barua ikisema mkataba uridhiwe. Mnajua hawa wawekezaji kutoka New Zealand na Australia wanaondoka? Kuna ng’ombe 7,000 wako pale na kuna meli inaingia Septemba italeta ng’ombe.

“Kuna wawekezaji wengi tu wanaondoka. Jiulize kwa nini nchi za wenzetu kama Botswana, Zimbabwe, Kenya wanaendelea vizuri. Iulize Wizara ya Kilimo na Mifugo, mbona mpaka leo tunaagiza ng’ombe nje ya nchi? Tuna ng’ombe 26 milioni, mbona tunaagiza nyama na maziwa kutoka nje?”

Utata wa uwekezaji

Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya Narco zinadai kuwa mkataba huo ulishinikizwa na ‘mamlaka za juu’ bila kufuata sheria za ununuzi na kanuni za uwekezaji.

“Suala hili lilifanyika tangu Agosti mwaka jana wakati nchi inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu. Ni wakati ambao hata Baraza la Mawaziri lilikuwa linaelekea kuvunjika na kulikuwa na shinikizo la wakubwa,” kilisema chanzo chetu ndani ya Narco.

Mtoa taarifa alisema katika majadiliano ya mkataba huo, Bodi ya Narco ilitaka Kampuni ya Overland ipewe hekta 10,000 pia ipewe miaka 33 ya kumiliki ardhi hiyo kwa majaribio, lakini kulikuwa na shinikizo kutoka ‘juu’ la kumilikisha ranchi hiyo kwa miaka 99.

“Kulikuwa na mvutano mkubwa, ikabidi suala hilo lifikishwe kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye alibadilisha baadhi ya vipengele kikiwamo cha kuvunja mkataba kama mwekezaji hatatimiza masharti,” alisema.

Hata hivyo, AG Masaju alisema: “Sijawahi kushinikizwa na kusaini mkataba wowote na wala kwa jambo lolote lile.”

Habari zinasema baada ya mvutano mkali, iliamuliwa Kampuni ya Overland ipewe miaka 66 ya umiliki wa ardhi hiyo.

NARCO

Meneja wa Masoko Narco, Immanuel Mnzava alisema uwekezaji huo ulifanyika kwa lengo zuri japokuwa ulitokana na shinikizo kutoka ngazi za juu.

“Ranchi ya Mzeri inaendeshwa kwa ubia kwa uwekezaji wa kisasa kwa sababu hatukuwa na mtaji wa kutosha. Mambo mengine siwezi kukueleza hadi Meneja Mkuu aje ataeleza, lakini kulikuwa na shinikizo kutoka ngazi za juu,” alisema.

Narco ni miongoni mwa mashirika yaliyowekwa chini ya Tume ya Rais ya Ubinafsishaji Mashirika ya Umma (PSRC) na baadaye CHC na sasa chini ya Msajili wa Hazina.

Mwaka 2006, Baraza la Mawaziri liliagiza Narco igawanye maeneo yake sehemu mbili kwa mita 2,500 hadi 4,000 na vitalu vigawanywe kwa wafugaji wazalendo na eneo linalobaki libaki kuwa la mfano kwa wananchi wanaozunguka.

Vitalu hivyo vilitolewa kwa wawekezaji wazawa kwa njia ya ushindani. Kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kuna vitalu 121 vilivyogawanywa kwa wawekezaji hao, wengi wao wakiwa watu mashuhuri.

“Mchakato ulikuwa wazi kwani mwekezaji alitakiwa kuja na barua ya Serikali za Mitaa, wizara na taarifa zake za fedha. Wamepewa vitalu hivyo kwa miaka 33 kisha itaangaliwa upya,” alisema Mnzava.

Kaimu Meneja Mkuu wa Narco, Bwire Kafumu alisita kuzungumzia suala hilo kwa kina kwa maelezo kwamba vyombo vya dola vinachunguza mkataba huo.

“Mimi hapa ninakaimu tu nafasi, siyo ‘General Manager’. Suala la Mzeri na Overland liko kwa Msajili wa Hazina na mamlaka nyingine zinachunguza. Msajili wa Hazina ndiye mwenye dhamana na mashirika yote ya umma. Kuna mamlaka nyingine pia zinashughulikia. Tuwe na subira tu, siwezi kueleza maana nitakuwa naingilia,” alisema Bwire.

Hata hivyo, alisisitiza, “Siyo kila mara katika uwekezaji kunakuwa na ushindani, kama amepatikana mwekezaji na ana sifa anapewa tu.”

Bwire alikaimishwa nafasi hiyo, Desemba mwaka jana baada ya aliyekuwa Meneja Mkuu, Dk John Mbogoma na bodi yote ya wakurugenzi kusimamishwa kazi na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba kutokana na kutoridhishwa na usimamizi wa ujenzi wa machinjio ya kisasa katika eneo la Ruvu.

Kuhusu utata huo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola alisema: “Takukuru tunafanya uchunguzi, inawezekana upo, lakini mpaka nifuatilie ili kujua kama kweli upo.”

 
Toggle Footer
TOP