Loading...
Monday

Hoja kuhusu tija ya kuuzungusha Mwenge wa Uhuru kwa sasa


KWA mara ya kwanza Mwenge wa Uhuru uliwashwa Tanganyika Desemba 9 mwaka 1961. Alexander Nyirenda ndiye aliyepandisha Mwenge juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro kama ishara ya Uhuru na Mwanga.

Mwenge uliwashwa kama ishara ya kuangaza ndani na nje ya nchi kuleta matumaini pale yalipopotea, kuleta upendo kwenye uadui na kuleta heshima kwenye chuki.

Tangu kuasisiwa kwa Mwenge wa Uhuru umekuwa ni utamaduni wa kukimbiza mwenge kila mwaka katika mikoa na wilaya mbalimbali za Tanzania.

Utamaduni huu wa kukimbiza mwenge umeendelea kwa muda mrefu tangu ulipoasisiwa hadi mwaka huu ulipozinduliwa tena mkoani Morogoro na Makamu wa Rais Bi. Samia Suluhu Hassan.

Ni ukweli usiopingika kuwa maudhui ya kuwa na Mwenge wa Uhuru yalikuwa bora zaidi wakati wa uhuru na tunapaswa kuyaenzi. Na tukumbuke kuwa Tanzania ndiyo nchi pekee duniani yenye utamaduni huu wa kukimbiza mbio za mwenge kama taifa.

Kwa mantiki ya makala hii, ningependa tujiulize maswali kidogo. Je, maudhui ya Mwenge wa Uhuru wakati wa uhuru na wakati wa sasa yapi bora? Je, kuna haja ya kuendelea kuukimbiza kila mwaka?

Hapa kumekuwa na mijadala mingi mitaani yenye kuleta hisia mbalimbali huku wengine wakiona ni bora Mwenge uendelee kukimbizwa kila mwaka huku wengine wakiona hakuna tija kuendelea kuukimbiza.

Binafsi ni mmoja wa wale wasioona tija ya kukimbiza mwenge kila mwaka hasa katika nyakati hizi ambapo maudhui yake yamebadilika.

Kama tulivyoona hapo awali, maudhui makubwa ya Mwenge yalikuwa kuonyesha ulimwengu ya kuwa sasa tuko huru na kuwatia moyo wale wengine ambao hawakuwa huru wakati huo ili waweze kupigana kwa dhati na kuweza kupata uhuru wao kama taifa.

Maudhui ya mwenge kwa wakati huo yalikuwa dhairi kabisa na yalifikiwa lengo lake kikamilifu.

Baada ya kuwa na Mwenge wa Uhuru ilitupasa kama taifa kudhihirisha uhuru wetu kwa kupambana kwa juhudi za dhati kabisa kuleta maendeleo endelevu kwa taifa letu.

Ilitupasa kama taifa kuweka kipaumbele kwenye kilimo, elimu na uongozi bora ili kuweza kuzitumia rasilimali zetu kwa wote na hii ndiyo ingekuwa ishara bora ya kuonyesha kuwa uhuru wetu umekamilika.

Kila mwaka tunafanya jitihada kubwa za kukimbiza mwenge kila kona ya nchi yetu na huko kote wakimbizaji wa mwenge huona taabu, shida na umaskini wa hali ya juu wanaopata Watanzania wavuja jasho. Lakini cha kusikitisha kabisa hali za Watanzania sisi maskini bado hazibadiliki ilhali tunakimbiza mwenge kila mwaka.

Tija ya mwenge wetu itakuja pale ambapo maisha ya Watanzania yataweza kubadilika na kuona manufaa ya rasilimali zao zikitumika kwa ajili ya kila mwananchi. Cha kusikitisha, kwa sasa uzalendo unaonyweshwa na wakimbiza mwenge siyo ule walionao viongozi wetu walio katika nafasi nyeti za kuweza kujineemesha wao na familia zao.

Kila kukicha tunasikia vile rasilimali zetu zinaporwa na wawekezaji kutoka nje kwa sababu ndio tunaoamini watatuletea maendeleo kwenye maboksi.

Hivi leo changamoto za nchi yetu tumezibatiza jina na kuziita ‘Jipu’ hivyo basi leo tuna majipu kwenye ardhi kubwa iliyochukuliwa na wawekezaji wasioitumia. Wanyama pori wanauawa kila kukicha ili wachache wajinufaishe, viongozi wanajilimbikizia mali na kuzificha nje ya nchi na mambo kadha wa kadha.

Sasa huu mwenge tunaokimbiza kila mwaka unaleta tumaini gani? Unamulika upendo gani na kuonyesha uhuru gani kama kila siku tunaona wachache wananeemeka kwa migongo ya wengi maskini?

Kinachonitia simanzi zaidi katika ukimbizaji wa Mwenge huu wa Uhuru wananchi maskini ndio ambao hushurutishwa tena kuchanga kwa ajili ya mwenge huo kwa nguvu na manyanyaso makubwa.

Kama hivi ndivyo, mwenge una tija gani kwa wananchi wake?

Mwenge wa uhuru huzunguka sehemu mbalimbali Tanzania kuzindua miradi mbalimbali iwe mikubwa au midogo. Hapa ndipo huwa napata mashaka kidogo. Kwanini tutumie gharama kubwa kukimbiza mwenge nchi nzima tukikwa na makundi lukuki ya watu wanaotumia gharama kubwa kwenda kuzindua miradi tu.

Kama nia hasa ni kuzindua miradi iliyoanzishwa, kwanini tusitumie viongozi wetu kama wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi, viongozi wa vijiji na kata? Viongozi hawa ndio wanaofahamu fika miradi yote ilianzishwa sehemu zao, lakini kwanini wao wasifanye kazi hii mpaka ifanywe na mwenge?

Nchi yetu kwa sasa inakumbwa na majipu mengi ambayo yanahitaji kutumbuliwa kwa kiasi kikubwa.

Majipu ya umaskini vijijini na mijini ni mengi watu wanashindwa kupata maisha bora na nafuu kama wanavyoahidiwa. Pengo kati ya walionacho na wasionacho ni kubwa kiasi kwamba Watanzania wengi wanajihisi wakiwa katika nchi yao.

Viongozi tuliowachagua kwa kura nyingi wanapigania maslahi yao kwanza kuliko maslahi ya wananchi waliowachagua. Maendeleo ya dhati katika nchi yetu hayaaminiwi kuletwa na wananchi wake bali kwa kukaribisha wageni kutoka nje wanaokuja kupora rasilimali zetu kwa jila la uwekezaji.

Elimu yetu bado inaendelea kuzorota na kuwa duni ilhali sasa tumeambiwa elimu ni bure. Lakini ubora wa elimu unaonekana au ni bora kila mwafunzi apate bora elimu na sio elimu bora na yenye tija?

Kilimo kwa sasa kimetupiwa kisogo kabisa wakulima wadogo hawathaminiki kama vile wanavyothaminiwa wakulima kutoka nje ambao ni wawekezaji.

Jitihada za kumkomboa mkulima ni ndogo kuanzia kutoa pembejeo za kilimo, kupanga bei bora, kuweka masoko imara na kutoa elimu endelevu kwa wakulima kwa kutumia maofisa ugani na kilimo ambao wengi wao wako mijini wakijifungia katika ofisi zao wakiogopa kwenda mashambani.

Changamoto hizi na nyingine nyingi zimekuwa ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku na mwenge tangu umeanza kukimbizwa umezitatuaje ili kudhihirisha uhuru wetu ama tumekuwa tukifanya kwa mazoea tu kwa sababu mwenge unapaswa kukimbizwa?

Kama nia yetu ni kuuenzi mwenge wa uhuru kila mwaka, basi uwe unawashwa siku ya kukumbuka ya Uhuru Desemba 9. Hii itapunguza gharama kubwa ambazo zinatumika kila mwaka kwa ajili ya mwenge. Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kupunguza gharama katika sehemu mbalimbali, basi na hili litizamwe kwa jicho la dhati kabisa ili kuona tija ya mwenge huu kwa sasa.

Kama nia ya kukimbiza mwenge huu ni kuuenzi uzalendo wa nchi hii basi tuanze kubadilika sisi wenyewe na kutenda haki kwa taifa letu na kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya kila Mtanzania.

Haileti mantiki kuona tunaongelea uzalendo kwenye mwenge wakati kuna watu wachache wanaoishi paradiso wakiwa ndani ya Tanzania kwa kutumia migongo ya wavuja jasho maskini.

Ni imani yangu ya dhati kabisa maudhui imara ya kuwashwa mwenge wetu wakati wa uhuru ni kumulika nchi yetu na kutangazia uhuru, amani na upendo kwa wanyonge na maskini ili waweze kukombolewa katika dhiki na mateso yao.

Kama miaka inavyozidi kusonga mbele dhiki, mateso na umaskini kwa Watanzania zinazidi kutamalaki hata tukiuwasha mwenge kila siku itakuwa ni kazi bure kwani haumkomboi mtu kama dhamira za wenye dhamana ya nchi yetu imekufa.

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP