Loading...
Tuesday

Kiwanda cha Wachinda Dodoma chafungwa kwa kuchinja na kusindika nyama ya punda

Baraza la Taifa la usimamizi wa mazingira (NEMC) limekifungia kiwanda cha Huwa Cheng Company Limited kilichopo mjini Dodoma na kukitoza faini ya shilingi milioni 200 baada ya kubaini kiwanda hicho kinajihusisha na usindikaji wa nyama ya punda, jambo ambalo ni kinyume na utamaduni wa watanzania huku mazingira ya shughuli hiyo yakiwa hatarishi kutokana na uchafu unaozalishwa kuzagaa kwenye makazi ya watu.

Mabishano makali yalizuka baina ya wamiliki wa kiwanda husika ambao ni raia wa China na maofisa wa NEMC, yaliyochukua muda mrefu, kabla ya maofisa hao kutoa tamko la kufungwa kwa kiwanda hicho.

Kiwanda hicho ambacho kwa siku kinadaiwa kuchinja punda wasiopungua 200, inaelezwa kuwa kinaharibu kizazi cha wanyama hao ambao uzao wake unatajwa kuwa ni mdogo hali inayotishia idadi ya wanyama hao ambao kwa Kanda ya Kati hutumiwa katika kazi mbalimbali.

Mohamed Hamis ambaye ni meneja msaidizi wa kiwanda hiki ambaye amezungumza kwa niaba ya raia hao wa Uchina, anasema nyama hizo za punda zinasafirishwa kwenda kuuzwa nchini China.

Wakazi wa mji wa Dodoma wanatupa lawama kwa mamlaka za mkoa kutobaini kiwanda hicho na kukichukulia hatua huku kukiwa na taarifa ya nyama hizo kuzagaa na kuuzwa katika maeneo mbalimbali ya mji huo hasa kwenye mabaa na migahawa ya vyakula. [via GSengo blog]
 
Toggle Footer
TOP