Kumbe walijitahidi kumzuia Kitwanga asiingie Bungeni ile siku

[...] Imedaiwa kuwa muda mfupi kabla ya kuingia bungeni juzi asubuhi katika siku anayodaiwa kuingia bungeni akiwa amelewa, (aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles) Kitwanga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Misungwi alizuiwa (kuingia) mara tatu na mbunge mwenzake kutoka Mwanza, Richard Ndassa wa Jimbo la Sumve (CCM) lakini hakutaka kusikia ushauri huo.

Akizungumza na Nipashe jana, Ndasa alisema alijaribu kadri alivyoweza kumzuia (Kitwanga) asiingie bungeni na badala yake kuondoka kabisa eneo hilo lakini ilishindikana.

Alisema yeye (Ndasa) alimuona Kitwanga ana kila dalili kuwa amelewa na ndiyo maana alijaribu kumsihi asiingie bungeni, lakini hakuwa tayari baada ya kusisitiza kuwa “yuko sawa kabisa”

Akielezea zaidi, Ndasa alisema alimuuliza Kitwanga kwa lugha ya Kisukuma; “Ole sawa ielelo?" akimaanisha “uko sawa leo”, naye akamjibu pia kwa lugha ya Kisukuma: “Nale sawa gete” akimaanisha yuko sawa kabisa.

“Unajua Kitwanga nakaa naye kiti cha jirani, sasa wakati anaingia asubuhi nikamuona hayuko sawa. Nikamuuliza na alinijibu kwa kifupi, kisha akaenda mbele kukaa tayari kwa kujibu maswali,” alisema Ndassa.

Ndasa alisema hata baada ya kipindi cha Bunge kumalizika asubuhi, alikutana na Kitwanga nje ya viunga vya Bunge na kujaribu kumshika mkono ili kumuondoa na eneo la Bunge, lakini alimkimbia.

Ndassa alisema aliamua kumfuata dereva wa Kitwanga na kumwambia amchukue na kumuondoa kwenye viwanja hivyo vya bunge, lakini Kitwanga hakuwa tayari kuingia ndani ya gari.

“Unajua mimi ni Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM mkoa wa Mwanza, hivyo nilijitahidi sana kumzuia jana (juzi) lakini nilishindwa… na wakati akiwa getini ndipo alipoitwa na Waziri Mkuu ofisini na jioni mkasikia taarifa ya Rais Magufuli,” alisema Ndassa.

[...] Mbunge wa Bukoba Mjini (CHADEMA), Wilfred Lwakatare, alisema alimpongeza Rais Magufuli kwa kuchukua uamuzi huo haraka, huku akibainisha kuwa bado kuna mawaziri wengine nane ambao anaamini wataungana na Kitwanga kwa kuwa wameonyesha dalili zote kuwa ni 'mizigo'.

"Kitwanga ni sehemu ya matatizo ya serikali nzima ya CCM. Hivyo ndivyo walivyolelewa. Huyu ni mmoja tu, tutaendelea kuwaona wakiwajibishwa kwa sababu Rais ana mtazamo wake, si wa taasisi," alisema.

"Hizi ndizo tabia zao, na alipowanyima semina elekezi aliharibu zaidi. Na bado kuna mawaziri wengine nane hivi wataondoka madarakani kwa utaratibu huu huu,” alisema Lwakatare ambaye aliongeza kuwa alisoma na Kitwanga katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) miaka ya 1986-1988 na kwamba kadri amjuavyo, wakati huo hakuwa mnywaji wa kiwango cha kuingia kazini akiwa amelewa.