Loading...
Tuesday

Maalim Seif anawindwa? Polisi yamwita kwa mahojiano

Jeshi la Polisi Zanzibar litamhoji Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad Ijumaa ya wiki hii kuhusu masuala mbalimbali ambayo hata hivyo, hayakuwekwa wazi.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Makame alisema jana: “Natambua kuwa wasaidizi wangu watazungumza naye Ijumaa. Wao ndiyo wanajua watamhoji nini.”

Alipoulizwa kuhusu mahojiano hayo, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi naye hakuweka wazi badala yake alisema kuna masuala mengi ambayo ofisi yake inahitaji kuyafahamu kutoka kwa Maalim Seif.

Hii ni mara ya kwanza kwa Maalim Seif kuhojiwa na polisi tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu ambao kwa Zanzibar ulirejewa Machi 20, baada ya ule wa Oktoba 25 mwaka jana kufutwa.

Maalim Seif ambaye kabla ya uchaguzi huo alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alipinga kurudiwa kwa uchaguzi huo msimamo ambao pia ulichukuliwa na chama chake.

Kiongozi huyo amekuwa akitoa matamko kadhaa ya kuwashawishi wananchi kupinga utawala wa Serikali iliyopo madarakani.

Akiwahutubia wafuasi wake huko Pemba hivi karibuni, Maalim Seif alisema Serikali ya CCM imeanza kutikisika kutokana na vikwazo vinavyoendelea kuwekwa na wahisani pamoja na hatua ya chama chake CUF kutowatambua viongozi wake pamoja na Serikali.

“CCM wajue wamekalia kuti kavu, siku yoyote wataanguka... tufanye kazi mpaka haki yetu tuhakikishe imerudi na wenzetu hawana safari ya kudumu,” alisema.

Aliwataka wanachama wake kuonyesha kwa vitendo kutoitambua Serikali ikiwamo kukataa kulipishwa kodi za ovyovyo pamoja na kujitenga na viongozi wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Mfano tunaweza kuamua siku fulani kuanzia saa sita, tunasimamisha vyombo vyote vya usafiri na siku nyingine tunaamua kupiga honi Zanzibar nzima kuonyesha hatuitaki Serikali ya CCM,” alisema huku akishangiliwa na umati uliofurika katika ofisi za chama hicho.

Mapema jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alisema kuwa amesikia juu ya wito huo lakini hakuwa amepata taarifa rasmi kutoka kwa mkuu wake.

“Nimesikia kama mlivyosikia ninyi,” alisema na kuongeza: “Nimeelezwa pia hata leo Kamishna wa Polisi Zanzibar alikuwa na mahojiano naye.”

Kuhusu hilo Kamishna Makame alisema: “Sijaonana wala kuzungumza naye leo. Hiyo si kweli.”

Juzi, wakati akizindua ripoti ya Uvunjifu wa Haki za Binadamu uliofanyika visiwani humo kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema wanazo taarifa za Serikali kutaka kuwakamata viongozi waandamizi wa chama hicho na kuwashikilia.

Alisema wamebaini mpango wa kukamatwa kwao na kuwekwa kwenye Mahakama za bara ili kuwanyamazisha Wazanzibari.


Juzi gazeti la MwanaHALISI Online lilichapisha habari ifuatayo...
TAARIFA zimevuja. Wanasiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanatajwa kushinikiza Jeshi la Polisi kumkamata Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF)

Taarifa hizi zinathibitishwa na Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Zanzibar ambaye amesema;

“Tunazo taarifa kwamba, kuna wanasiasa wameliagiza Jeshi la Polisi kuandaa mashtaka kwa ajili ya kumshitaki Maalim Seif Sharif Hamad kwamba alipokuwa Pemba alifanya maandamano bila ya kibali wakati hakukuwa na maandamano yoyote.”

Mazrui amesema hayo leo wakati wa Uzinduzi wa Taarifa ya Uvunjwaji wa Haki za Binadamu Zanzibar kwa mwaka 2015/2016 uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

“Viongozi hao wamepangiwa kukamatwa na kuletwa katika magereza ya Tanzania Bara kwa lengo la kuwanyamazisha Wazanzibar ili wasipaze sauti zao kupinga utawala wa kidkteta uliowekwa madarakani kwa nguvu za dola kinyume na matakwa ya kidemokrasia ya wananchi wa Zanzibar,” amesema.

Akizungumzia uzinduzi wa Taarifa ya Uvunjwaji wa Haki za Binadamu Zanzibar 2015/2016 amesema, CUF inajiandaa kuchukua hatua kutokana na uharibifu uliofanywa na Serikali ya CCM visiwani humo.

Mazrui akimwakilisha Maalim Seif kwenye uzinduzi wa ripoti hiyo amesema, nakala ya ripoti hiyo pia watamkabidhi Rais John Magufuli kwa lengo la kujua kilichofanyika na kinachofanyika Zanzibar.

“Baada ya hatua ya leo ya uzinduzi wa taarifa hii, CUF kimejiandaa kuchukua hatua ikiwemo ya kumuandikia rasmi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh, Dk. John Magufuli na kumkabidhi nakala ya taarifa hii ili ajue kinachofanyika nchini na hasa akiwa Amiri Jeshi Mkuu,” amesema Mazrui.

Hatua nyingine zitakazochukuliwa na CUF ni pamoja na kuiwasilisha taarifa hiyo pamoja na vielelezo vyote katika Jumuiya, Taasisi za Mashirika ya Kimataifa yanayotetea haki za binadamu ulimwenguni ili kuchukua hatua zao.

“Pia tutaiwasilisha taarifa pamoja na vielelezo vyote katika Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora hapa nchini ambayo hata katika mkutano wa Geneva ilitambuliwa uwepo wake,” amesema na kuongeza.

“Na katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) pamoja na taasisi nyingine zinazoshughulikia masuala ya haki za binadamu hapa nchini.”

Mazrui amesema “ Hatua nyingine itakayofuatwa ni kufungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kuhusiana na matendo yanayohusisha Jeshi la Polisi visiwani Zanzibar.

Hatua nyingine itakayochukuliwa ni CUF kukamilisha taratibu zitakazoiwezesha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuanzisha uchunguzi dhidi ya watu wenye dhama mbalimbali ambao wamehusika kuchochea, kutoa au kusimamia maagizo yaliyoepelekea makosa dhidi ya ubinadamu na makosa yaliyoilenga jamii ya watu fulani.
  • MwanaHALISI Online
 
Toggle Footer
TOP