Loading...
Sunday

Makonda azipa benki 6 siku 21 zibaini na kurejesha fedha za watumishi bandia

Paul Makonda
Paul Makonda
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amezitaka benki mbalimbali nchini kutoa ushirikiano kwa serikali ili kubaini akaunti zilizokuwa zinatumika kuweka mishahara kwa watumishi bandia, pamoja na kuwabaini wote waliohusika katika malipo hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini humo, Makonda amesema kuwa hadi sasa mkoa huo una watumishi bandia zaidi ya 280, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 3 zimekuwa zikitumika kuwalipa.

Makonda amesema:
Kwa hiyo tunazitaka benki zote, na nimeshawaandikia barua, tutawapa idadi ya pesa ambazo tunazidai, karibu benki sita. Kwa hiyo:-
  • Benki zisaidie serikali ya mkoa wa Dar es Salaam kujua ni nani aliyekuwa anaingiza pesa kwenye hizi akaunti

  • Benki iisaidie serikali ya mkoa, ni nani aliyekuwa anachukua hizi kwenye hizi akaunti kwa sababu tunafahamu, hakuna akaunti yoyote ya benki unaweza kuitumia mtu tofauti na mhusika.

  • Kama hakuna aliyekuwa anachukua hizo pesa, maana yake hizi pesa zetu ziko benki. Ninaziomba ndani ya siku 21 nizipate hizo pesa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. 
Makonda amezitaka benki hizo kukamilishwa mambo hayo na amezipatia majina na namba zote za akaunti za watumishi waliokuwa wananufaika na ubadhirifu huo. Amesema kufanya hivyo pia anazisaidia benki kutambua watumishi wa mabenki wasio waaminifu.

Amezitaja benki 6 kuwa ni NMB ambapo zilipitishwa zaidi ya shilingi bilioni 2.8, CRDB milioni 400, NBC milioni 141, DCB milioni 85, Standard Chartered milioni 2 na Community Bank milioni mia moja na tisini na nne.


 
Toggle Footer
TOP