Loading...
Thursday

Mwl. Mndeme: MC Pilipili - Nimeota ndoto mchana nikikusikiliza kuhusu kodi

Kuna mambo magumu kuyaamini lakini kuota ndoto mchana ukiwa unamsikiliza mtu ni jambo la kufikirisha. 

Leo mchana nilikutana na kauli ya mmoja wa washerekeshaji au waongoza matukio (MaMC) maarufu hapa mjini ajulikanaye kama MC Pilipili. Kauli yake hiyo imewekwa kwenye ukurusa wa Youtube wa Millard Ayo na inapatikana HAPA. Katika kauli hiyo MC Pilipili anazungumzia kitendo cha Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuwataka MaMC waanze kulipa kodi. 
Kwa maelezo yake, MC Pilipili anaonesha kwamba kitendo hicho ama kinawaonea wanaotoa huduma hizo kama yeye au kinatoa tafisri ya kutothamini juhudi zao za kujiajiri kama vijana. 
Rafiki yangu MC Pilipili anasema kwamba wao wamejitahidi kujiajiri kwa kutumia vipawa vyao hasa kwa kuwa hawakuweza kufanya vizuri sana kwenye masomo na hivyo kubaki na chaguo la kutumia vipawa vyao vya kuzaliwa kujiajiri. Pamoja na kwamba hajatoa kauli ya kuonesha kwamba wasitozwe kodi kabisa, lakini anaonesha kwamba kama ni lazima wao kulipa kodi basi “wafikiriwe kukatwa kidogo” ili waweze kuendelea kukidhi mahitaji yao ya kulipa kodi za nyumba kule  “Mbezi isiyo na foleni” na “kutanua mjini”. 
MC Pilipili anasema kwamba kipato wanachokipata kwa kazi hizi kinawasaidia wao kusaidia familia zao na hivyo sio sahihi sana waanze kulipa kodi kwa kipato hicho. Kama vile haitoshi, anawataka TRA wawawekee bei elekezi ya huduma wanazotoa ili waweze kuwa na kiwango kinachoeleweka cha kulipa kodi.
http://4.bp.blogspot.com/--cNTsCBVqU0/UjHf-MIoGqI/AAAAAAAAlXs/JHM1h5r5OBU/s640/5.jpg
Nilifurahishwa sana na kauli hii kwani kaongea jambo ambalo ni wazi “ana mzigo au uchungu nalo” sana lakini alilitoa moyoni kwa “lugha ya kikomedi” na hivyo kuonekana anachekesha. Zaidi ya yote, hoja ya wao kufikiriwa kukatwa kodi kidogo, ameijenga kwenye dhana kwamba wanasaidia nchi kuleta maendeleo na kutoa ajira kwa vijana wengine wanaofanya kazi zinazoendana na majukumu hayo. Sijajua ni kitu gani TRA wameongea na kina MC Pilipili na wamewataka walipe kiasi gani cha kodi lakini inatia moyo kuona TRA wanatoka “ndani ya boksi kongwe la kodi” na kupanua wigo wa ukusanyaji kodi. Kwa miaka mingi mfumo wetu wa kodi umekua ukiwabana watu waliojariwa katika sekta binafsi tu kama vile watumishi wa umma, wenye biashara zilizosajiliwa, waliojariwa katika taasisi zinazofahamika kisheria, na katika makampuni binafsi. Kwa kufanya hivyo, waajiriwa hawa wamekua wakibeba mzigo mkubwa wa kodi ya mapato kwa niaba ya maelefu wengine wenye shughuli zenye vikipato vikubwa kama washereheshaji, wenye kumbi za sherehe, na wapambaji lakini hawalipi kodi.
Ndoto ya Mchana

Wakati namsikiliza MC Pilipili kwa mara ya pili ili nimwelewe vizuri, ghafla nipata usingizi mzito na muda huohuo kujikuta napotelea ndotoni. Nikiwa ndotoni nikajikuta mwenye mawazo mengi na ya kusumua sana. Nikajikuta nawaza hali ya maisha ya mtumishi wa umma kama mwalimu, daktari, polisi, wahadhiri wa vyuo vikuu, wakufunzi, madereva, mafundi mchundo, na wengine wengi. Nilifikiria kiwango chao kidogo cha mshahara kinachokatwa kodi kubwa kila mwezi huku wakiwa na wingi wa majukumu ya kutunza familia, kusomesha watoto wao, kusaidia ndugu zao wasio na uwezo, kulipa kodi kubwa za nyumba, na mengine mengi. Niliwaza jinsi makundi haya yamekua yakihenyeka siku zote huku wakiwa hawana uwezo wa kujipatia huduma bora kutokana na ufinyu wa kipato chao. Niliwafikiria watumishi hawa ambao wengi wao hawajawahi kuwa na mawazo yaliyotulia huku wakihangaika na mambo kadha wa kadha ya kuwasaidia waweze kujikimu angalau kwa mahitaji ya lazima kimaisha.
Nikiwa huko ndotoni kwenye dimbwi la mawazo na nimeinamisha kichwa chini, nikageuka mkono wa kushoto na kuwaona kundi kubwa la waajiriwa wa sekta rasmi na wengi wao wakiwa na nyuso za huzuni, wanatokwa jasho jingi, na wamechoka kama waliotoka kutembea umbali mrefu.  Wengi wao uvaaji ulikua duni sana kwa maana ya uduni wa mavazi na yalipitwa na wakati huku yakiwa hayana mvuto. Niliwasikia wakiongelea uchache wa mavazi yao, kwamba makazi yao ni duni, na maisha ya wengi wao yamejaa adha, kadhia, bughudha, “stress”, na kukosa furaha. Nilimsikia mmoja akisema yeye kafanya kazi miaka 20 akikatwa kodi lakini hajawahi kuona maji ya bomba na mwingine akisema hajawahi kuona maajabu ya kuishi nyumba yenye umeme.
http://2.bp.blogspot.com/-KYwAZ3GbmCU/UxSdKyyRzII/AAAAAAAAC_A/8JiJeZ7U-Sc/s1600/1.jpg
Wakati nawasikiliza waajiriwa hawa wanaokatwa makato makubwa kila mwezi kwa kodi ijulikanayo kama “Pay as You Earn” (PAYE) yaani “Lipa kodi kulingana na kiwango cha mapato yako”, nikasikia watu wanacheka upande wangu wa kulia kama vile watu walio kwenye sherehe. Nilipogeuka kuwatazama nikukutana na sura za “mastaz” wengi na miongoni mwao niliona MaMC wengi niliowahi kukutana nao kwenye sherehe na mmoja wao alifanana na MC Pilipili. Huyu aliyekua anafana na MC Pilipili alikua akifanya komedi kuwachekesha wenzake na wao walikua “wanamtunza” kwa “noti nyekundu” na zingine za “kijani zinazofanana na dola zinazotumika Zimbabwe”. Ghafla nikawaona MaMC wakijitahidi kutangaza majina yao na huduma zao kwenye radio na runinga. Ikatokea skrini kubwa mbele yangu ikionesha kwa wakati mmoja mitandao ya kijamii kama mablogu, twita, fesibuku, instagramu na mingine. Picha na maaandishi yao mengi yalilenga kuonesha uzuri wa kazi zao na ubora wa maisha wanayoishi. Zikaja picha zao wakiwa wamevaa suti kali na za kisasa na mitupio mingine ya ukweli tena wakibadilisha mitotko karibu kwa kila tukio. Zikaja picha zikiwaonesha wako ndani ya magari yao ta kifahari huku “wanajipika selfie”. 
Nikaona sura za MaMC wengi ambazo zimezagaa mitandaoni “wakila bata” maeneo nyeti ndani na nje ya nchi. Picha zingine zilionesha wakiwa viwanja vya ndege wakipaa toka eneo moja kwenda lingine ndani na nje ya nchi “kutanua” na kwenya matukio. Ghafla wakaanza kutoa shuhuda kila mmoja zinazosisitiza vijana kutong’ang’ania ajira rasmi na badala yake wajitokeze kujiajiri kama wao kwani kufanya hivyo “inalipa” na mafanikio ni waziwazi na ya haraka.
Nikawasikia wakibishana kati yao ni nani anapata matukio mengi kwa wiki ya kuendesha na nina anapata mshiko wa ukweli kwa kila tukio. Mmoja akasema yeye kwa wiki analala mara 2, mwingine tatu, na mwingine akasema yeye hataki zaidi ya matukuio mawili kwa wiki kwani yanamtosha. Mmoja akasema yeye bei ya chini ni milioni 2 kwa tukio pamoja na mafuta ya gari lake; mwingine akasema hata laki 5 kwake sawa tu kwani halali wiki nzima; mwingine akasema bila milioni na laki tano hafanyi kazi; na wengine walikua wanatabasamu tu. Nikiwa bado sjiui iwapo nimesimama au nimekaa wakati nawatazama, nikageuka tena mkono wa kushoto na kukutana na sura za wale waajiriwa walijichokea kila mmoja akitazama pay-slip yake ya mshahara.
http://www.bongo5.com/wp-content/uploads/2014/08/MC-Pili-Pili-akifanya-yake-3-530x353.jpg
Nikawaona wakiwa wanaelezea ugumu wa maisha wanaoishi huku wengi wakisema wanaishi maeneo ya Kibangu, Msewe, Ununio, Tandale, Kijenge Juu, Sombetini, Mabatini, na vijiji vya Kintinku, Maneremango, Igugumo, na Mbagala Kuu. Wengi wakawa wanaelezea kuwa hununua mavazi mapya mara moja au mbili kwa mwaka wakati wa sikukuu za kidini. Wengine wakasema hawajawahi kwenda likizo wala kuwaza juu ya jambo hilo. 
Kundi kubwa likasema hawajawahi hata kupanda basi kwenda mkoani na ndege huwa wanazisikia tu na kuziona zinaporuka mawinguni huku wakiwa hawana hakika kama kwa udogo wake mtu anaweza kuingia ndani. Nilisikia baadhi yao wakisema hawajawahi kutoka nje ya wilaya zao kwenda mijini na hawajawahi kuwaza kupanda ndege kwani wanahisi siku wakipanda watapotea. 
Kundi moja likasema wanawaza kufanya kile kilichofanywa na “Wasabato Masalia” kama namna ya kuwasaidia angalau kuona viwanja vya ndege vikoje. Wengine walikua wanauliza umeme ni nini, maji ya bomba yanasukumwa na nini kuingia ndani, na kwa nini nyumba za watu wa “Mbezi isiyo na foleni” zinadekeza uchafu kwa kujengewa vyoo ndani.
Nilipotazama mbele yangu kwa mbali nikamuona mtu mwenye sura kama ya Utumbuaji Majipu amekaa kwenye kiti kipya na meza ndogo viliyochongwa na fundi seremala wa keko. Pembeni yake alikua kasimama mtu anayefanana na Kamishna Mkuu wa TRA akijibu maswali.  Huyu Mzee aliyefanana na Mtumbuaji Majipu alikuwa anapiga mahesabu kwenye daftari la mistari huku akitumia kalamu aina ya biki. Nikasikia anamuuliza yule aliyefanana na mkuu wa TRA:
  • Kwani huyu anayepata mshara wa shilingi 720,000 unamkata shilingi ngapi kwa mwezi?” Akajibu, PAYE yake ni Shilingi 101,900.
  • “Je huyu wa 4.2M kwa mwezi ambaye ni wa cheo cha juu kabisa katika utumishi wa umma unamkata shilingi ngapi?” Akajibu PAYE yake ni shilingi 1,145,900.
  • Akauliza tena, “Je, huyu MC wa kiwango cha kati mjini ana matukio kwa wastani mangapi kwa mwizi?” Akajibu matukio manne hadi kumi.
  • Akauliza tena, “Je kwa wastani huwa anacharge kiasi gani kwa kila tukio?” Akijibu, kati ya shilingi laki 7 hadi milioni 2
  • Akamuliza kwa mara ya mwisho, “Hivyo kwa wastani anapata shilingi ngapi kwa mwezi?” Akasema kati ya milioni 2,800,000 kipindi cha sherehe chache na Milioni 20,000,000 kipindi cha msimu wa sherehe nyingi.
  • Akamuliza, “hawa MaMC huwa unawatoza kodi kiasi gani?” akajibu, bado tunajadiliana nao tuone kama watakubali kulipa kodi ili tuwapangie kiwango.


Yule Mzee aliyekua na Sura ya Utumbuaji Jipu akaweka kalamu yake ya biki juu ya meza kisha akatabasamu na kumtazama yule aliyefanana na Mkuu wa TRA usoni na kumwambia taratibu, “Nakupa siku mbili ukirudi niambie umechagua nimtumbue nani na nimtumuaje kati ya wewe na hawa MaMC”. Nikamtazama yule mzee na kumwambia kwa sauti kubwa, “Wewe Mh unayefanana na Baba Mtumbua Majipu, ni kwa nini hili jipu unaliweka kiporo na kulibonyeza taratibu wakati tayari linadondosha usaha?” Nilipomaliza kukawa na ukimya na ghafla nikamuona mwalimu mmoja wa shule ya msingi kutoka lile kundi la upande wa kushoto akiuliza:
  • “Ninyi MaMC kwa nini mwapenda kuturingishia kuhusu mapato yenu na maisha ya anasa munayoishi lakini hamupendi kulipa kodi kama sisi?
  • Kwa nini mumewafanya wamiliki wa vyombo vya habari kusahau kabisa kutualika kuongelea kazi na majukumu yetu kwenye vyombo vya habari ili jamii ijue na badala yake tunawaona na kuwasikia niniyi tu kila siku mukielezea mulivyofanikiwa na munavyotanua”?
  • Inakuwaje leo mulalamike kwamba muna kipato kidogo wakati ninyi musiolipa kodi mwaishi kama malaika wakati sisi walipa kodi twaishi kama mashetani?


Kilichoniuma kwenye ndoto hii ni kwamba kabla yule Mzee aliyekua na Sura ya Utumbuaji Jipu hajanijibu wala wale MaMC waliokua wakimsikiliza yule mwalimu wa shule ya msingi hawajasema neno, nilishtuka na kujikuta naandika malaka.
Imeandikwa na Mwalimu MM

Unaweza kumwandikia kupitia mmmwalimu(at)gmail.com

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP