Loading...
Wednesday

Msajili Hazina atupilia mbali maombi ya Halmashauri ya Jiji kuhusu UDA vs Simon Group Ltd

MSAJILI wa Hazina ametupilia mbali maombi ya Halmshauri ya Jiji la Dar es Salaam ya kutaka kurudishiwa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) kwa kusisitiza kuwa Kampuni ya Simon Group ina hisa halali katika shirika hilo.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaac Mwita, alikaririwa na vyombo vya habari jana akimtaka Msajili kukadhibidhi shirika hilo kwa uongozi wa Jiji kwa madai kuwa Simon Group walinununua shirika hilo kinyume cha taratibu.

Msajili alisema pia serikali haina mpango wa kuuza hisa zake za asilimia 49 inazomiliki katika shirika hilo.

Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam waliomba wapewe hisa hizo za serikali ikiwa hawatarudishiwa hisa za Simon Group.

Akizungumza na Nipashe ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Habari wa ofisi ya Msajili wa Hazina, Gerard Chami, alisema kuwa ofisi yake haiwezi kubadilisha mkataba wa umiliki wa Uda.

“Msajili anakamata hisa za serikali ambazo ni mali ya Watanzania, hazihusiani kwa namna yoyote na hisa asilimia 51 za Jiji ambazo walishaziuza kwa kampuni ya Simon Group. Tunashangaa wanapotaka tuingilie mambo yao ambayo kimsingi hatuhusiki,” alisema Chami.

Chami alieleza kuwa kulikuwa na kesi iliyokuwa mahakamani baina ya Jiji na kampuni ya Simon Group Ltd. Iliamuliwa Simon Group ilipe Sh. bilioni 5.5 ili kununua hisa za Jiji na alifanya hivyo na kwa mazingira hayo, Msajili hadi sasa anamtambua kama mwanahisa mwenza wa Uda.

Alifafanua kuwa hakuna namna ambayo Msajili atajihusisha na hisa hizo kwa kuwa siyo wajibu wake bali anachotakiwa kumtambua mwanahisa mwenzake ambaye kwa sasa ni kampuni ya Simon Group.

“Suala hili linachukuliwa kisiasa zaidi, lakini ukweli unajulikana kwani ni sawa mtu alikuwa na mali yake akaamua kugawa sehemu na kumpa mwingine aliyehitaji kwa wakati huo, lakini kwa sababu zake kile alichogawiwa akaamua kuuza kwa mtu mwingine, ni vigumu kurudi kwa sasa kumweleza aliyegawa awali kugawa tena na hisa zake," alifafanua.

“Yeyote aliyeuziwa hisa hizo sisi tunamtambua ndiye mwanahisa mwenza, tunachojua kwa sasa kampuni ya Simon Group ndiye mwanahisa mwenza kwa kuwa alishamaliza kulipa kwa kutekeleza amri ya mahakama,” alisema.

Alibainisha kuwa hisa asilimia 49 za serikali ina hiari nazo kama ni kuuza kwa faida au kwa ajili ya kupeleka fedha katika eneo jingine lenye maslahi ya jamii na siyo kwa Jiji linavyotaka kumpa mwanahisa mwenza katika shirika hilo.

Meya Mwita alisema juzi kuwa Baraza la Madiwani la Jiji la Dar es Salaam liliazimia katika kikao chake kuwa fedha zaidi ya Sh. bilioni 5.5 zilizolipwa kwa Jiji na kampuni ya Simon Group kwa ajili ya kununuliwa hisa zisirudishwe hadi tathmini ya kina itakapofanyika na kujiridhisha kuwa hadaiwi chochote kwa kutumia mali mbalimbali za Uda kwa maslahi yake.

Pia waliunda kamati ndogo ya wajumbe watatu ambao ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea na Mwanasheria wa Jiji, Jumanne Mtinangi kwa ajili ya kufuatilia suala hilo.

Naye Ofisa Habari wa Simon Group, Deus Buganywa, alisema jana hawajapokea barua yoyote kuhusiana na kutakiwa kurejesha hisa hizo baada ya kuulizwa juu ya sakata hilo la UDA.
  • Imenukuliwa kutoka kwenye gazeti NIPASHE
 
Toggle Footer
TOP