Loading...
Friday

Mwanachuo ashikiliwa na polisi akituhumiwa kutoa maneno ya kichochezi dhidi ya Rais na Mkuu wa Majeshi

Jeshi la polisi mkoani Arusha linamshikilia mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Tengeru aliyejulikana kwa jina la Harold Mmbando (23) mkazi wa Arusha kwa kosa la kutoa taarifa za uchochezi dhidi ya Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein na Mkuu wa Majeshi, Davis Mwamunyange pamoja na kusambaza ujumbe wa maneno makali juu ya viongozi hao.

Akiongelea tukio hilo, Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 17 mwaka huu majira ya saa 3 asubuhi. Alisema kuwa mwanafunzi huyo alitoa taarifa za uchochezi kuhusu mkuu wa majeshi.

"Mtuhumiwa huyo aliandika maneno haya, 'Mwamunyange pindua nchi haiwezekani wote wawe nje halafu hakuna aliyepewa mamlaka ya kukalia kile kiti,' hayo ndiyo maneno aliyoyasema mtumiwa huyo," alisema Mkumbo.

Aidha aliongeza kuwa mbali na maneno hayo pia mtuhumiwa huyo alisambaza ujumbe mwingine wenye maneno yafuatayo,"Dr Shein akiuawa kama Karume sitashangaa wala kustuka naomba mungu mauaji ya kisiasa yaliyotokea Zanzibar yawe kwa viongozi wa kisasa hasa watawala na sio wananchi wa kawaida,” hayo ndio maneno aliyoyaandika mtuhumiwa huyo kupitia mitandao ya kijamii wa Faccebook.

Mkumbo alisema kuwa mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika, huku akitoa rai kwa watu wote wanaotumia mitandao ya kijamii kuitumia pasipo kukiuka sheria na taratibu. Alitumia muda huo pia kutoa onyo kali kwa yeyote atakayebainika anatumia mitandao vibaya na kusema kuwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Wakati hayo yakiendelea, mshtakiwa wa kesi ya kumtukana Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,  John Pombe Magufuli ndugu Isaac Emily (40), mkazi wa Olasiti jiji Arusha, inatarajiwa kuanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Juni 5 mwaka huu katika mahakama ya hakimu mkazi Arusha.
  • Taarifa ya Woinde Shizza
 
Toggle Footer
TOP