Loading...
Sunday

Mwasisi wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya hajasahau aliposhtakiwa kwa Nyerere, Sokoine

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ataendelea kuishi kwenye mioyo ya watu wengi kwa namna alivyoongoza nchi huku Kamishana mstaafu wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, George Timbuka akikumbuka alivyoshtakiwa kwa Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Kwanza.

Mpambanaji huyo wa dawa za kulevya aliyestaafu mwaka 2004 anasema kitu ambacho hatakisahau na kinaendelea kumuumiza katika maisha yake ni jinsi alivyopelekwa kwa Mwalimu Nyerere kwa madai alikuwa akimnyanyasa mfanyabiashara mmoja maarufu mkoani Mbeya wakati huo.

Akizungumza katika mahojiano maalumu hivi karibuni, Timbuka alisema alipoitwa Ikulu alifurahi akidhani, kwa rekodi yake, alikuwa anakwenda kupandishwa cheo lakini alipofika alikumbana na mashtaka ambayo hakuwahi hata kuyafikiria.

“Nakumbuka siku hiyo nilikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Mbeya (RCO), nikajulishwa kuwa naitwa na Rais, Ikulu Dar es Salaam. Kipindi hicho kwa vyeo vyetu, ilikuwa mtu ukiitwa na Rais ujue kuna mambo mawili; ama kupandishwa cheo au kufukuzwa kazi, na kwa kuwa nilikuwa najiamini kuwa sina kosa nililolifanya, nikajua naenda kupandishwa cheo,” anasimulia.

“Hata nilipoondoka nyumbani nilimuaga mke wangu kuwa naenda Ikulu asiwe na wasiwasi na yeye hata alipoulizwa na wenzake ‘Timbuka yuko wapi’, aliwajibu ‘mume wangu ameenda kupandishwa cheo’,” anasema.

Timbuka anasema hali haikuwa kama alivyotarajia badala yake alipofika Ikulu aliwakuta Mwalimu Nyerere; aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine pamoja na maofisa wengine wa Ikulu. Katika kikao hicho, Timbuka anasema alielezwa sababu ya kuitwa kwake kuwa ni kuhusu tuhuma za unyanyasaji dhidi ya mfanyabiashara (jina limehifadhiwa kwa sababu hajapatikana).

Kamishna huyo mstaafu alielezwa kwamba alikuwa akimnyanyasa mfanyabiashara huyo kwenye biashara zake hivyo alitakiwa kutoa utetezi wake kwa nini asichukuliwe hatua.

“Niliumia sana huyu mfanyabiashara tulimkamata kwa tuhuma za kuhujumu uchumi, alikuwa na mali za magendo nyingi, sisi kama polisi tulitimiza wajibu wetu,” anasimulia.

Timbuka ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya Jeshi la Polisi ikiwamo ya Kamanda wa Polisi mikoa ya Shinyanga, Lindi na Mkoa wa Kipolisi wa Tazara alisema wakati anaitwa, Tume iliyoundwa na Sokoine ilishamaliza kazi ya kuwachunguza yeye na viongozi wa ngazi ya mkoa na wilaya ya Mbeya na ripoti ilishawasilishwa kwa Waziri Mkuu ambaye aliipeleka pia kwa Mwalimu.

Kamishna Timbuka anasema baada ya Mwalimu Nyerere kusikiliza kesi hiyo alimuona hana kosa na akaamuru arudi nyumbani.

“Hata pale aliponiambia nirudi bado sikuamini, nikamuuliza Rais nirudi wapi? Akaniambia Timbuka rudi nyumbani kwako ukaendelee na kazi yako Mbeya, hapa nimegundua kuwa hukuwa na kosa lolote,” alisema Timbuka.

Anasema kilichomuuma sana ni kwa jinsi kesi hiyo ilivyopelekwa mpaka kwa Rais wakati angeweza kushtakiwa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa, Mkuu wa Jeshi la Polisi au hata kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, lakini alishangaa kwa nini utaratibu haukufuatwa.

Timbuka ambaye amewahi pia kufanya kazi Benki Kuu ya Tanzania (BoT) akiwa Mkuu wa Upelelezi akishughulikia makosa ya kughushi alisema tukio jingine kubwa ambalo analikumbuka ni pale alipowezesha kukamatwa kwa kiwanda cha kutengeneza dawa za kulevya kilichokuwa eneo la Kunduchi, Dar es Salaam na watuhumia kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa.

Anachojivunia

Timbuka anasema anajivunia kuwa mwanzilishi wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini kwani ameijenga na kazi zake zinaendelea kufanyika na kutambuliwa ndani na nje ya Tanzania.

“Inanipa faraja kuona Tume sasa inafahamika ndani na nje ya nchi, lakini kubwa zaidi kazi yake inaonekana, ninachoweza kusema tu ipewe meno zaidi ili iweze kuchunguza, kukamata na kushtaki.”

Kesi mahakamani

Akifafanua kipengele cha utaifishaji vielelezo vya kesi za dawa za kulevya pindi zifikishwapo mahakamani, Timbuka anasema hilo bado ni tatizo linalohitaji kutafutiwa njia mbadala ya kulitatua.

Akitolea mfano wa nyumba moja iliyoko eneo la Mbezi Beach, Dar es Salaam ambayo ilikutwa na mtambo wa kutengeneza dawa hizo, anasema haikutolewa mahakamani kama kielelezo.

“Licha ya wahusika kuhukumiwa kifungo jela, ilitakiwa hata ile nyumba itaifishwe, lakini ilishindikana kwakuwa haikutolewa mahakamani kama kielelezo,” alisema Timbuka na akatoa wito kwa wapelelezi wa kesi za dawa za kulevya kuendelea kuisoma vyema sheria, ili wasitoe mwanya kwa wahalifu hao kubakia na mali zinazotokana na uhalifu wao.

“Mtu akikamatwa na dawa za kulevya hata kama ni kwenye gari, nyumbani hivyo vyote ni vielelezo vinatakiwa vifikishwe mahakamani na Mahakama ndiyo itatoa uamuzi wa kutaifisha au la, kulingana na utetezi utakaotolewa,” anafafanua.

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP