Loading...
Monday

Taasisi zatii agizo la serikali na kuachana na benki za kibiashara

MASHIRIKA na taasisi zote za serikali zimetii agizo la serikali la kufunga akaunti zake katika benki za biashara na kuhamisha fedha zilizoko katika akaunti hizo kwenda akaunti walizoamriwa kufungua Benki Kuu (BoT).

Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki kuwa baada ya kutoa agizo hilo na kuwapa muda kukamilisha kufunga akaunti hizo, mashirika na taasisi zote zaidi ya 200 walianza mchakato ndani ya muda husika.

Alisema mpaka sasa kuna taasisi au mashirika chini ya 50 ambayo hayajakamilisha uhamishaji wa akaunti hizo kwa sababu mbalimbali ikiwemo zilizo katika mikoa ambayo hakuna tawi la BoT.

Alifafanua kwamba si rahisi kwa mashirika yote kufanikisha hatua zote ndani ya muda waliopewa, kwa kuwa baadhi ya mashirika, ufunguzi wa akaunti ni lazima ufanyike kwa uamuzi wa bodi ya wakurugenzi.

Mafuru alisema akaunti nyingine za mashirika na taasisi hizo, ziko katika akaunti za muda maalumu katika benki hizo za biashara, hivyo kabla ya kuzifunga na kuhamisha fedha husika, kutahitajika majadiliano kati ya shirika au taasisi husika na benki yake.

Februari mwaka huu ambao ulikuwa muda wa kukamilisha kuhamisha akaunti, Msajili wa Hazina aliwataka watendaji wakuu wote wa mashirika na taasisi za serikali kufuata maelekezo matano ya kufunga akaunti zao katika benki za biashara na kuhamishia fedha hizo BoT.

Katika agizo la kwanza, watendaji hao walitakiwa kufungua akaunti ya mapato yao kwa aina ya fedha za mapato wanayopokea; Kama ni za kigeni au shilingi za Tanzania, katika tawi la karibu yao la BoT haraka iwezekanavyo.

Baada ya kufungua akaunti hizo, watendaji hao wametakiwa kuelekeza makusanyo yote ya fedha za ofisi zao ikiwemo fedha za ruzuku zinazotoka serikalini kwenda katika akaunti mpya zilizofunguliwa katika matawi ya BoT.

Agizo la tatu la Serikali kwa watendaji hao ni kuhamisha fedha zote zilizobakia katika akaunti zao zilizoko katika benki hizo za biashara na kupeleka katika akaunti mpya zilizoko BoT.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uhusiano pekee kati ya mashirika hayo na benki za biashara itakuwa akaunti itakayohifadhi fedha za uendeshaji ambayo imetakiwa kuwa na fedha zinazotosha uendeshaji wa shughuli za taasisi zao kwa mujibu wa matarajio ya matumizi yao ya kila mwezi.
 
Toggle Footer
TOP