Loading...
Tuesday

Tanzania inajenga njia ya umeme itakayounganisha Kenya na Zambia – WM Majaliwa

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania ina mpango wa kujenga njia ya umeme kutoka Mbeya hadi Zambia kupitia Tunduma ili kupunguza tatizo la umeme linaloikabili nchi hiyo.

“Serikali ya Tanzania inajenga njia ya umeme ya msongo wa KV 400 kutoka Iringa - Dodoma – Singida – Shinyanga ambayo ni sehemu ya mradi mkubwa wa umeme unaolenga kuunganisha Zambia, Tanzania na Kenya,” amesema.

Amesema upembuzi yakinifu kwa ajili KV400 kutoka Iringa hadi Mbeya umekwishakamilika tangu mwaka 2012, na hivi sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili kuunganisha kipande cha kutoka Mbeya na gridi ya Taifa ya Zambia. 

Waziri Mkuu ambaye anahudhuria mkutano huo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli, ametoa ufafanuzi huo leo mchana (Jumanne, Mei 24, 2016) wakati akichangia hoja kwenye mjadala wa wakuu wa nchi na Serikali uliohusu Nishati na Mabadiliko ya TabiaNchi kwenye ukumbi wa mikutano cha kimataifa wa Mulungushi. 
 
Amesema ili kukabiliana na changamoto ya nishati barani Afrika, nchi za bara hili zinahitaji kuwa na fedha ama mitaji, teknolojia ya kisasa na wataalamu wenye ujuzi wa kutosha jambo ambalo amesema ni gumu kulikamilisha kila nchi peke yake. 

Amesema ili kukaribisha wawekezaji kwenye sekta ya umeme, Tanzania inafanyia marekebisho sheria zake ili kuruhusu uwekezaji kwenye sekta hiyo. 

Akizungumzia kuhusu hali ya nishati Tanzania, Waziri Mkuu alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na gesi asilia yenye ujazo wa futi trilioni 57.25 (tcf), makaa ya mawe yenye uhjazo wa tani bilioni 1.9 (asilimia 25 imevumbuliwa), umeme wa nguvu ya maji wa gigawati 4.7 ambazo ni asilimia 12 tu ndiyo inatumika. Pia alisema Tanzania ina deposits za urani yenye ujazo wa ratili milioni 200 (200 million pounds), joto la ardhini (geothermal) linaloweza kuzalisha umeme wa megawati zaidi ya 5,000. “Hivyo ni mbali na vyanzo vya umeme utokanao ua upepo na jua,” alisema. 

Akizungumzia kuhusu usambazaji wa umeme vijijini, Waziri Mkuu alisema Tanzania kupitia REA imefanikiwa kusambaza umeme kwenye asilimia 52 ya vijiji vyote na inatarajia kufikia asilimia 90 ifikapo mwaka 2025. 

Akishiriki mjadala huo, Makamu wa Rais wa Nigeria, Bw. Yemi Osinbajo alisema bara la Afrika linahitaji kuwa na vyanzo vikubwa vya umeme kama kweli linataka kufanikiwa kukamilisha kuwa na viwanda vya kutosha. 

“Hatuwezi kuwaza kuwa na viwanda vingi wakati tukitegemea umeme wa nguvu ya jua peke yake… huu unahitaji uwekezaji mkubwa na eneo kubwa la kuweka mitambo,” alisema. 

Akishiriki mjadala huo, Makamu wa Rais wa Nigeria, Bw. Yemi Osinbajo alisema bara la Afrika linahitaji kuwa na vyanzo vikubwa vya umeme kama kweli linataka kufanikiwa kukamilisha kuwa na viwanda vya kutosha. 

“Hatuwezi kuwaza kuwa na viwanda vingi wakati tukitegemea umeme wa nguvu ya jua peke yake… huu unahitaji uwekezaji mkubwa na eneo kubwa la kuweka mitambo,” alisema. 

Naye Waziri Mkuu wa Msumbiji, Bw. Carlos Agostinho do Rosário alisema masuala ya nishati yanahitaji uwekezaji mkubwa kwa hiyo akashauri makampuni kuungana kwenye uwekezaji na kuibua miradi ambayo ina tija (feasible and viable). 

Waziri Mkuu amefuatana na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Asantu Kijaji, wachumi kadhaa pamoja na wataalamu wa sekta ya fedha. 

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MEI 24, 2016.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Waziri wa Ulinzi wa Zambia, Christopher Mulenga baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Keneth Kaunda uliopo Lusaka Mei 23, may 2016 ambako leo atamwakilisha Rais John Magufuli kwenye mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya Watanzania baada ya kuwasili kwenye hoteli ya Intercontinental iliyopo Lusaka baada ya kuwasili Mei 23, 2016 amabako leo atamwakilisha Rais John Magufuli kwenye mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Rais wa Zambia, Edgar Lungu katika Mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika – ADB kwenye Kituo cha Mikutano cha Mlungushi kilichopo Lusaka Zambia, Mei 24, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri Mkuu wa Msumbiji, Carlos Agostino do Rosario katika Mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika – ADB kwenye Kituo cha Mikutano cha Mlungushi kilichopo Lusaka Zambia , Mei 24, 2016.
Rais wa Zambia, Edgar Lungu akifungua Mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika – ADB kwenye Kituo cha Mikutano cha Mlungushi kilichopo Lusaka Zambia , Mei 24, 2016.Kushoto kwake ni Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa ambaye alimwakilisha Rais John Magufuli kwenye mkutano huo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika – ADB kwenye Kituo cha Mikutano cha Mlungushi kilichopo Lusaka Zambia , Mei 24, 2016. Wengine pichani kutoka kushoto ni Makamu wa Rais wa Nigeria, Prof. Yemi Osinbojo, Rais wa Chad, Idriss Debyo, Rais wa Zambia, Edgar Lungu na Waziri Mkuu wa Msumbiji, Carlos Agostino do Rosario
Wasanii wa Lusaka wakicheza ngoma ya asili ya Zambia katika mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika – ADB uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Mlungushi Zambia Mei 24, 2016. Tanzania iliwakilishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

  • Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
 
Toggle Footer
TOP